Othman: Mazungumzo kutafuta mwafaka Zanzibar yamepiga hatua

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema kuna hatua kubwa ya mafanikio kuhusu mazungumzo ya kisiasa ya kutafuta suluhu ya mgogoro uliopo Zanzibar.

Vyama vya ACT- Wazalendo na Chama cha Mapinduzi (CCM) vipo katika mazungumzo ya kutafuta mwafaka wa kisiasa baada ya uchaguzi wa Oktoba 29,2025, uliolalamikiwa na chama hicho kikuu cha upinzani visiwani humo.

Mazungumzo hayo yanaongozwa na Othman, Juma Duni Haji (mwenyekiti mstaafu wa ACT -Wazalendo) huku CCM wakiwakilishwa na marais wastaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Dk Ali Mohamed Shein.

Akizungumza leo Ijumaa Februari 27,2026 na waumini wa Kiislamu katika Msikiti wa Arafa Mombasa Mjini Unguja, Othman amesema mazungumzo hayo yatasaidia kuiondoa  Zanzibar kwenye mifarakano ili isonge mbele.

Othman ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu amesema Zanzibar imejaaliwa kuwa na neema kubwa na watu wake wengi ni Waislamu, hivyo haipaswi kuifikia hatua ya kuharibikiwa kutokana na migogoro isiyotafutiwa Suluhu.

“Uislamu ni neema kubwa ya kuwa na pahala pa kukimbilia kufuata miongozo mbalimbali ya quran na mwendendo wa Mtume Muhammad (S.A.W) kutafutia ufumbuzi wa migogoro na mizozo inayojitokeza ili waumini na wananchi kwa jumla waendelee kuwa kitu kimoja.

“Si jambo jema, kwa baadhi ya watu wakiwamo viongozi kudharau juhudi za kutafuta suluhu licha ya kwamba hiyo ndio njia sahihi iliyowekwa na Mungu,” amesema Othman.

Kwa mujibu wa Othman, Zanzibar bado kuna viongozi wenye hekima na baada ya kutokea mzozo wa kisasa, Mungu kawaelekeza kusaidia kutafuta suluhu kwa yaliyotokea kisiwani humo.

Amewataka Waislamu na wananchi kwa jumla kuendelea kuiombea dua Zanzibar ili iendelee kuwa salama kuepusha maafa makubwa yasije yakatokea.

Amesema fikra za viongozi hao zimeelekeza kutengenezwa suluhu itakayoweza kuifaa Zanzibar kwa muda mrefu, hivyo amewataka wahusika kuwa na nia ya dhati kuhusu jambo wanalolisimamia ili Wazanzibari kuishi katika neema.

Imamu wa msikiti huo, Sheikh Ali Yunus amehimiza waumini wa Kiislamu kutafuta suluhu pale kunatokea tofauti miongoni mwao, akisema ndio njia iliyoelekezwa na kuridhiwa na Mungu.

Sheikh Yunus amesema hatua hiyo inajenga umoja ambao ndio nguzo tegemezi na Waislamu wanapokuwa kitu kimoja Mungu hujaalia ufumbuzi wa mambo yao, hivyo ikitokea wanazozana hawatafanikiwa.