FEDHA ZA MIRADI YA KIMKAKATI NI KICHOCHEO CHA AJIRA NA UCHUMI JUMUISHI

SERIKALI imejipanga kupeleka fedha kwenye miradi mbalimbali ya kimkakati ili wananchi waendelee kufaidika, ikiwemo kupata ajira katika sekta binafsi na serikalini.

‎Akizungumza Februari 26, 2026 wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa barabara ya Ntendo – Kizungu wenye urefu wa kilomita 25 kwa kiwango cha lami mkoani Rukwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu, amesema kuwa fedha zinazotolewa na Serikali zinalenga kuwanufaisha wananchi moja kwa moja kupitia fursa za ajira na kukuza kipato.

‎Ziara hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Rukwa, ambapo Waziri Sangu alisisitiza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha uwekezaji unaofanyika unaleta tija kwa wananchi wa maeneo husika.

‎Aidha, ametoa wito kwa mkandarasi wa mradi huo, China Geo Engineering Ltd, kuhakikisha kuwa ajira zinazohitaji wazawa zinatolewa kwa kipaumbele kwa wananchi wanaozunguka mradi huo ili waweze kunufaika moja kwa moja na utekelezaji wake.

‎Waziri Sangu amesema kuwa lengo la Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kujenga uchumi imara, shindani na jumuishi unaowagusa wananchi wote.

‎“Tunaposema uchumi jumuishi ni kwamba fedha zinazokuja kwa wananchi ziweze kuzalisha ajira kwa wananchi wazawa,” amesema Waziri Sangu.

‎Katika hatua nyingine, ameitaka kampuni hiyo kuzingatia Sheria za Kazi katika utoaji wa ajira, ikiwemo kuhakikisha wafanyakazi wanaostahili wanapelekewa michango yao katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) pamoja na michango ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa mujibu wa sheria.

‎Kaimu Meneja Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Rukwa Mhandisi Joseph Gimonge, amesema kuwa utekelezaji wa mradi unaendelea vizuri ambapo hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 53.37.

‎Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Mha. Gimonge alieleza kuwa kazi zinaendelea kulingana na mpango uliopangwa, ambapo kwa hatua zilizofikiwa zinaendelea vizuri kulingana na maendeleo ya mradi.

‎Kwa upande wao, wananchi wa Kata ya Muze, Kijiji cha Kizungu, wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kupeleka fedha za ujenzi wa barabara hiyo katika awamu ya kwanza. Wamesema mradi huo umekuwa na manufaa makubwa kwao kwani umechangia kupatikana kwa ajira kwa wakazi wa eneo hilo pamoja na kukuza kipato chao.

‎Wananchi hao wameeleza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha usafirishaji na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo lao.