Shinyanga. Zaidi ya wananchi 200 wa Tarafa ya Mjini, Manispaa ya Shinyanga, wametoa kero zao kupitia kliniki ya kusikiliza kero na migogoro iliyofanyika wilayani Shinyanga ikilenga kupunguza changamoto hizo.
Wakizungumza katika kliniki ya kusikiliza kero na migogoro ya wananchi iliyoanza jana na leo Februari 27, 2026, kwenye Viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, baadhi ya wananchi wamesema itawawezesha kupata haki zao.
Katika kliniki hiyo, migogoro ya ardhi imeongoza kutokana na wananchi wengi kutokuwa na uelewa wa masuala ya ardhi, hali ambayo imekuwa ikisababisha wananchi wengi kukosa haki zao kwa kudhurumiwa na watu wenye uwezo mkubwa.
Ally Salum, mkazi wa Mtaa wa Majengo, Manispaa ya Shinyanga amesema kero yao kubwa ni kukosa sehemu ya kupita kutokana na watu kujenga na kuziba njia hali ambayo imekuwa kero na kusababisha migogoro.
Mkazi mwingine wa Mtaa wa Butengwa, Gaudencia John amesema ameshindwa kuendeleza maeneo yake kutokana na mgogoro wa ardhi ambao umedumu zaidi ya miaka minane bila kupatiwa mwafaka na anaamini kilio chake kitapata ufumbuzi.
“Tumefika hapa kueleza kero zetu ili Serikali itusaidie, tayari mkuu wa wilaya ametusikiliza mmoja mmoja na watalaamu wake, tumeonesha nyaraka zote muhimu tunasubiri kwenda eneo la mgogoro pande zote mbili,” amesema Gaudencia.
Akisikiliza kero na migogoro ya wananchi, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro amesema kliniki hiyo imelenga kuwapatia wananchi fursa ya kueleza changamoto zao moja kwa moja kwa Serikali pamoja na kutafuta suluhu za haraka na za kudumu.
Amesema changamoto kubwa iliyojitokeza wakati wa kliniki hiyo ni uwepo wa migogoro mingi ya ardhi, ikiwamo mipaka ya mashamba, umiliki wa viwanja na matumizi ya ardhi ambayo imeonekana kuathiri ustawi wa jamii na kuchelewesha maendeleo ya wananchi wengi.
Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Leila Chipanyanga amesema jumla ya migogoro waliyopokea ni 78 na kwamba wanaendelea na mchakato wa utatuzi wa migogoro huku akibainisha kuwa wananchi wengi hawajui taratibu za kutatua migogoro ya ardhi.
Shughuli ya kusikiliza kero na kushughulikia migogoro ya ardhi lilianza tangu mwaka 2025 na walifanikiwa kupokea migogoro 258 ikiwamo ya mashamba, mipaka na viwanja.