Dar es Salaam. Kikao maalumu cha ushauri (DCC) Wilaya ya Moshi kimepitisha mapendekezo mawili ya kuanzishwa kwa halmashauri mpya ya Vunjo na kupandishwa hadhi kwa barabara mbili za wilaya kuwa za mkoa.
Mapendekezo hayo yamekuja baada ya ziara ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi akisisitiza maboresho ya kiutendaji na kuimarisha huduma kwa wananchi.
Kikao hicho kilichoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava kimependekeza kuanzishwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Vunjo ili kusogeza huduma za kiutawala na maendeleo karibu na wananchi.
Wilaya ya Moshi yenye majimbo matatu ya uchaguzi (Moshi Mjini, Moshi Vijijini na Vunjo), inahudumia maeneo mawili ya Manispaa ya Moshi na Halmashauri ya Moshi, inatarajiwa kugawanywa ili kuongeza ufanisi wa huduma za serikali na kuleta maendeleo kwa jamii husika.
Kuanzishwa kwa halmashauri hiyo mpya kunatokana na ombi la mbunge wa Vunjo, Enock Koola alilolitoa kwa Waziri Mkuu, Dk Mwigulu, aliyefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Februari 20, 2026.
Kutokana na ombi hilo, Waziri Mkuu alimwelekeza Naibu Waziri wa Tamisemi, Reuben Kwangila, kulishughulikia na kusimamia ukamilishaji wa hatua zote za mchakato ili kubaini kama eneo hilo linakidhi vigezo vya kuanzishwa kwa halmashauri.
Kwa mujibu wa mwongozo wa uanzishwaji wa mamlaka za Serikali za mitaa wa mwaka 2014, eneo linaloomba hadhi ya halmashauri linapaswa kutimiza masharti kadhaa ya kisheria na kiutawala, ikiwamo ridhaa ya wananchi kupitia mikutano halali ya vijiji, kata na baraza la madiwani.
Taarifa iliyowasilishwa kikaoni inaeleza kuwa tayari mikutano 78 ya vijiji, 14 ya kata (WDC) na mamlaka ya mji mdogo wa Himo imefanyika, ikihusisha wananchi 35,715 waliotoa maoni yao.
Mihtasari ya mikutano hiyo iliwasilishwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi.
Katika mikutano hiyo, wananchi waliridhia kwa asilimia 100 kuanzishwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Vunjo wakieleza kuwa hatua hiyo itarahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Hata hivyo, ilielezwa kuwa kati ya kata 16 zinazounda Vunjo, kata 14 zilifanya vikao vya WDC huku Njia Panda na Makuyuni zikiwasilisha maoni kupitia Baraza la Mamlaka ya Mji Mdogo wa Himo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava amesema kigezo kinataka uwepo wa angalau kata 20 huku Vunjo ikiwa na kata 16 kwa sasa, lakini akabainisha kuwa, kuna uwezekano wa kuongeza kata endapo mchakato utaidhinishwa.
“Ni kweli tuna upungufu wa kata nne, lakini upo uwezekano wa kuanzisha kata nyingine kama mchakato utakavyoelekeza. Lengo linaloangaliwa pia ni kusogeza huduma kwa wananchi katika eneo kwa ukaribu zaidi,” amesema.
Amesema pamoja na eneo la Vunjo kuwa na ukubwa usiokidhi kikamilifu kigezo cha kilomita za mraba 5,000, tathmini inazingatia vigezo vingine muhimu vinavyolenga kusogeza huduma karibu na wananchi.
“Sisi tutapeleka mapendekezo haya kwa Kikao Cha Ushauri Mkoa (RCC) na mamlaka za juu wataangalia kama vigezo tulivyonavyo vinakidhi kwa kiwango kinachoruhusu kuanzishwa kwa halmashauri,” amesema.
Mnzava amesema endapo halmashauri hiyo itaidhinishwa, kutahitajika pia mpango wa kujenga hospitali ya wilaya katika eneo husika sambamba na kuimarisha miundombinu ya kiusalama ikiwamo kituo kikuu cha polisi, Magereza na Zimamoto.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Shadrack Mhagama amesema msukumo wa hoja hiyo umeongezeka kufuatia tamko la Waziri Mkuu na maelekezo kwa Naibu Waziri wa Tamisemi kufafanua mchakato unaotakiwa kufuatwa.
“Tumezingatia michakato yote inayotakiwa. Tumeonesha vigezo mbalimbali vinavyohitajika na kwa asilimia kubwa vigezo muhimu vimefikiwa. Huenda visikidhi kwa asilimia mia moja, lakini maeneo muhimu tumeyafikia,” alisema Mhagama.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, John Meela, amesema mchakato huo ulianza mwaka 2021 na sasa umefikia hatua muhimu ya uamuzi.
Koola ambaye ni mbunge wa Vunjo, amesema wananchi wa Vunjo wamekuwa na kiu ya muda mrefu ya kuwa na halmashauri yao, akisisitiza kuwa hatua hiyo itasogeza huduma karibu na wananchi na kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo.