MKUU WA MKOA KATAVI AAGIZA UTII WA SHERIA ZA TASAC

Na Mwandishi Wetu,Katavi

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, ameagiza wadau wote wa usafiri majini na shughuli zinazohusiana na uendeshaji wa vyombo vya majini mkoani humo kuhakikisha wanatii kikamilifu sheria na taratibu zinazosimamiwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC).

Mrindoko ametoa maagizo hayo leo tarehe 27 Februari, 2026, alipokutana na watalaam wa TASAC waliopo mkoani Katavi kwa lengo la kufanya uhamasishaji na ufuatiliaji wa masuala ya usalama wa usafiri majini katika mialo iliyo katika mwambao wa Ziwa Tanganyika kwa wa mikoa ya Katavi na Rukwa.

Mrindoko ameelekeza kuwa vyombo vyote vya majini vinavyofanya shughuli za kiuchumi katika Ziwa Tanganyika upande wa mkoa wa Katavi vihakikishe vimesajiliwa kwa mujibu wa sheria, pamoja na kutumia vifaa okozi muda wote wa safari, na kuendeshwa kwa mujibu wa masharti ya leseni zao.

“Natoa wito kwa wamiliki na waendeshaji wa usafiri wa abiria na mizigo kuzingatia masharti ya leseni zao, udhibiti wa upakiaji kupita kiasi, uendeshaji unaozingatia hali ya hewa, pamoja na utaratibu wa ukaguzi wa mara kwa mara wa vyombo vyao,” alisema Mrindoko.

Kwa upande wake, Meneja Uhusiano kwa Umma wa TASAC, Bw. Saidi Mkabakuli alimshukuru Mkuu wa Mkoa na kueleza kuwa itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na mamlaka za Serikali mkoani humo katika kuimarisha usimamizi, ukaguzi, na elimu kwa wadau ili kupunguza ajali na kuongeza ufanisi wa huduma za usafiri majini.

Wakiwa mkoani Katavi, maafisa hao wa TASAC waliwakumbusha waendeshaji kuwa uzingatiaji wa sheria si hiari, bali ni wajibu wa kisheria unaolenga kulinda maisha na kuchochea maendeleo ya uchumi wa maeneo yanayotegemea usafiri majini.

Akizungumza wakati wa zoezi la uhamasishaji katika mialo ya Kirando na Ikola katika Ziwa Tanganyika, Afisa Mfawidhi wa TASAC Mikoa ya Rukwa na Katavi, Nahodha Optatus Kalolela alisema kuwa bado kuna changamoto za uzembe na kutofuata viwango vinavyowekwa kisheria, hali inayoweza kusababisha ajali na madhara makubwa kwa wananchi na mali zao.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko akipata maelezo kutoka kwa Meneja Uhusiano kwa Umma wa TASAC Said Mkubakuli wakati wa Timu ya TASAC ilipotembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huyo.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko akipata maelezo kutoka kwa Meneja Uhusiano kwa Umma wa TASAC Saidi Mkubakuli wakati wa Timu ya TASAC ilipotembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huyo.

Afisa Mfawidhi wa TASAC Mikoa ya Rukwa na Katavi, Nahodha Optatus Kalolela akizungumza na wasafirishaji na wavuvi katika Mwalo wa Ikola wakati walipokua katika ziara ya uhamasishaji na ufuatiliaji wa masuala ya usalama wa usafiri majini katika mwalo huo.

Afisa Mfawidhi wa TASAC Mikoa ya Rukwa na Katavi, Nahodha Optatus Kalolela akizungumza na wasafirishaji na wavuvi katika Mwalo wa Kirando wakati walipokua katika ziara ya uhamasishaji na ufuatiliaji wa masuala ya usalama wa usafiri majini katika mwalo huo.

Meneja Uhusiano kwa Umma wa TASAC, Bw. Saidi Mkabakuli akizungumza na wasafirishaji na wavuvi katika Mwalo wa Kirando wakati walipokua katika ziara ya uhamasishaji na ufuatiliaji wa masuala ya usalama wa usafiri majini katika mwalo huo.

Meneja Uhusiano kwa Umma wa TASAC, Bw. Saidi Mkabakuli akigawa vipeperushi kwa wasafirishaji na wavuvi wa Mwalo wa Ikola wakati walipokua katika ziara ya uhamasishaji na ufuatiliaji wa masuala ya usalama wa usafiri majini katika mwalo huo.