Ndege Iliyobeba Pesa Mpya Yaanguka barabarani, Watu 15 Wafariki

Global Publishers
February 28, 2026
0 Comments

Watu 15 wafariki dunia baada ya ndege ya kijeshi aina ya Hercules ya Jeshi la Anga la Bolivia kuanguka kwenye barabara yenye shughuli nyingi katika mji wa El Alto Ijumaa jioni, wakati wa hali mbaya ya hewa. Taarifa hizo zimetolewa na vyombo vya habari vya ndani pamoja na Wizara ya Ulinzi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, ndege hiyo ya mizigo ilikuwa ikisafirisha noti mpya za fedha kwenda maeneo mbalimbali ya nchi hiyo wakati ilipoanguka karibu na mji wa La Paz, ambao ni makao ya kiutawala ya Bolivia.

Video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha hali ya taharuki katika eneo la tukio, huku umati wa watu ukikusanyika karibu na mabaki ya ndege. Baadhi yao walionekana wakikusanya noti za fedha zilizokuwa zimetapakaa barabarani. Mamlaka za eneo hilo zilionekana zikitumia maji ya shinikizo la juu kuwatawanya watu waliokuwa wakizagaa karibu na eneo la ajali.

Picha zilizorushwa na vyombo vya habari vya ndani zilionyesha ndege ikiwa imeharibika vibaya pamoja na magari kadhaa yaliyokuwa barabarani wakati wa ajali. Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa El Alto ulifungwa kwa muda kufuatia tukio hilo.

Hata hivyo, maafisa hawajathibitisha rasmi iwapo kulikuwa na majeruhi au vifo vinavyohusiana na ajali hiyo, huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo chake.