SERIKALI imetoa kauli ya usalama na uthabiti wa miundombinu ya viwanja vya ndege nchini huku ikisema maboresho makubwa ya kiteknolojia yaliyofanyika yanawezesha safari za anga kuwa salama.
Katika kuhakikisha viwango vya kimataifa vinazingatiwa, Tanzania imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).
Msemaji amebainisha kuwa ukaguzi wa hivi karibuni wa ICAO umeonesha kuwa usalama wa anga nchini Tanzania umefikia asilimia 86, kiwango ambacho ni cha juu na cha kuridhisha kimataifa. Alama hizi zinajumuisha uwezo wa viwanja vyetu kuhimili changamoto za kimazingira na kiufundi wakati wote wa mwaka.
Serikali imewekeza shilingi trilioni 1.154 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kwa ajili ya miradi ya kimkakati kwenye viwanja vya ndege. Sehemu ya fedha hizi imeelekezwa katika mifumo ya mifereji ya maji, ukarabati wa barabara za kuruka na kutua (runways), na usimikaji wa taa za kuongozea ndege (AGL) ambazo zinawezesha ndege kutua hata kukiwa na hali mbaya ya hewa au giza.
Aidha amewataka waandishi wa habari wanapokuwa na masuala ya kitaalamu katika masuala ya anga wahoji wahusika ili wapate majibu badala ya kukurupuka.
Alisema hayo akizungumzia tukio la mwanahabari mmoja kuandika kitu bila weledi na kusababisha taharuki kuhusiana na suala la ndege ya ATCL kushindwa kutua Mwanza na kulazimika kutua kwa dharura uwanja wa ndege wa Kilimanjaro.
Msemaji huyo pia aligusia ukarabati unaoendelea katika viwanja vingine kama Moshi na Shinyanga, ambapo ujenzi unahusisha barabara za kuruka na kutua kwa kiwango cha lami na mifumo imara ya mifereji. Kwa mfano, mradi wa uwanja wa Moshi unahusisha ujenzi wa barabara za mzunguko na uzio wa usalama ili kuzuia muingiliano usio wa lazima wakati wa hali ya hewa duni. Hatua hizi zote ni sehemu ya mpango kabambe wa TAA wa kuhakikisha viwanja vyote 61 nchini vinakuwa na usalama wa asilimia 100.
Serikali imewahakikishia wasafiri na mashirika ya ndege kuwa miundombinu ya anga nchini ipo imara na salama. Tuzo za kimataifa za ubora na usalama ambazo JNIA na KIA zimezipokea ni uthibitisho tosha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kudhibiti vihatarishi vya usalama wa anga.