Dar es Salaam. Baada ya kubainika kuwa mifungo ya Ramadhan na Kwaresma ingeanza kwa pamoja, mlevi mmoja alipita mitaani akiyumba na kubwata: “Makobe (wasiofunga) mwaka huu imekula kwenu… mwaka huu mtaandamana! Leo ndio tutakujua wewe unaitwa Jimmy au Juma…
Mwaka huu utatafuta pa kujificha usipaone!” Alitembea na chupa yake mtaa mzima akirudia bwato lake kuhakikisha ujumbe unamfikia kila mmoja.
Nilichomwelewa ni kuwa ‘makobe’ walizikataa dini zao walipokutwa wanakula. Mkristu aliyefumaniwa akisosomola kipindi cha Kwaresma aliikana dini yake na kudai kuwa yeye ni Muislamu, kadhalika Muislamu aliyefumaniwa wakati wa mfungo wa Ramadhan alijisingizia kuwa Mkristo. Ndiyo maana alitoa mfano wa mtu aliyetumia majina mawili; wakati wa mfungo wa Ramadhan alijiita Jimmy na Kwaresma akageuka Juma!
Kwa mshtuko mkubwa siku moja kabla ya mifungo hii kuanza, niliona kundi la wakazi wa Buza wakiandamana. Nikadhani yale maneno ya mlevi yametimia. Kwa udaku nilimfuata shuhuda mmoja aliyelifuatilia tukio kwa umakini. Jamaa kwa utulivu alinivuta kando na kunipa kisa kilichonifikirisha sana.
Jamaa alidai kuwa alikuwa akienda kupanda basi Buza Kanisani ili awahi kwenye mishe zake za kila siku mitaa ya Keko. Lakini alipofika kituoni akakutana na askari waliomwambia hana haki ya kusimama pale. Kwa woga alisogea kando ambako wenzake walimwambia kuwa kituo kimehamishwa. Wapi? Akaambiwa “Kwa Mama Kibonge”, mahala ambapo ingembidi alipie boda kufika.
Ngoja kidogo nikupe stori ya Buza, maana wengine mkisikia jina hilo tu mnakumbuka “Kwa Mpalange”! Katika miaka ya Tisini Buza haikuwa na barabara ya kueleweka. Tulilazimika kutoka saa kumi za alfajiri (au usiku?), tukatembea kwa miguu (wenyewe tuliita “kupiga kwato”) hadi Tandika Davis Corner. Hapo ndipo tuligombea mabasi ya kutupeleka katikati ya Jiji.
Kutokana na msitu uliotanda wakati huo, majambazi yaliyosakwa huko mjini yalikuwa yakija kujificha kwenye msitu huu. Kitisho hicho kilitufanya waenda mjini wote tuwe tukisubiriana pale Buza Kanisani, na baada ya kazi tulikutana Tandika kwenye baa maarufu ya enzi hizo, Davis Corner saa moja za jioni tayari kwa marejeo. Si unaona? Baa si kwa kulewa tu, hata mambo ya maana hufanyika. Mbona nyie mnakesha “mpirani” na sisi hatusemi…
Basi bwana, tuliendelea hivyo kwa muda hadi tukapata ukombozi. Wakati ule msafirishaji mkuu Jijini ilikuwa kampuni ya UDA. Lakini kwa kuwa barabara haikupangiwa ruti, hatukupata usafiri. Hata hivyo zilikuwepo daladala na “Chai Maharage” zilizofanya kazi zaidi nje kidogo ya Jiji. Hizi zikagundua chimbo la Buza, hivyo tukapata ahuweni ya kupunguziwa nusu safari. Kwato zetu zikawa zikiishia Abiola.
Kuingia Buza bado kilikuwa kipengele. Kutoka Abiola ilikuwa ni lazima ushuke bondeni, uvuke maji kisha upande kilima kikali ndipo uiñgie Buza Kwa Mama Kibonge. Watu wakajenga daraja la magogo na hatimaye tukaanza kufikiwa na daladala moja iliyochoka na kupigwa marufuku ya kuonekana mjini.
Nauli yake haikuwa elekezi, unatazamwa umati unaohitaji kusafiri miksa na hali ya hewa. Kukiwa na manyunyu nauli inaongezeka.
Picha linaanza saa mbili za usiku, mvua inanyesha. Daladala kubwa lisilo na breki limepaki Tandika.
Kitendo cha mpiga debe kutamka “Buz…” kinatosha kulijaza basi kwa sekunde chache, abiria wakaning’inia mlangoni na madirishani. Pamoja na kutangaza nauli kuwa Alfu (wakati huo ni kubwa sana) kwa kila kichwa, mpiga debe haridhiki na kujaa kwa basi (anadai inayojaa ni ndoo ya maji tu). Anaendelea kuita.
Baada ya ugomvi na abiria, dereva anaanza safari ya kwenda Buza. Kutokana na ubovu wa njia, ngoma inakwenda kama inayosindikiza harusi hadi Abiola. Hapa sasa ndio unaingia bondeni palipokuwa na mkondo mkorofi wa maji. Basi linashuka mpela mpela mpaka darajani, linasimamia kwenye gia (kumbuka halina breki). Kabla ya kupanda, dereva anahakikisha ameshapiga gia namba moja kwa jinsi mlima ulivyotisha.
Sikumbuki ni mara ngapi ambapo basi liliishiwa pawa na kupindukia bondeni. Lakini huo ndio uliokuwa usafiri wetu. Baadaye barabara ilikarabatiwa, ikapigwa lami, na baadaye zaidi tukaunganishwa na ruti za kila kona ya mji. Tukapata wawekezaji wa Shule za Msingi na Sekondari, Hospitali kubwa, maghala yaliyopokea uwanja wa ndege na bandari, vituo vya kujaza mafuta na gesi na kadhalika. Hapa sasa na sisi tukawa sehemu ya wakazi wa Dar es Salaam.
Sasa kuhamishia kituo Kwa Mama Kibonge ni kukata mawasiliano na kuongeza gharama bila sababu za msingi. Fikiria mgonjwa anayetoka Tandika kwenda Hospitali ya Aga Khan Buza ateremshwe kwa Mama Kibonge, halafu alipie bajaji ya kumalizia safari. Fikiria adha wanayopata wanafunzi, kisha fikiria wafanyakazi wa kima cha kati na chini. Kuna awezaye kumudu nauli ya shilingi 120,000/= kwa mwezi? Nauli tu!
Huyo bado hajapeleka watoto shule wala hospitali, hajakula yeye wala familia yake, hajalipa kodi ya nyumba. Tunamuongelea Mtanzania wa namna gani? Lakini kwa nini wasiambiwe tatizo ni nini? Kama ni uwekezaji basi mtu atawekeza ukweni, je, stendi zitamfuata? Kama kituo kingehamishiwa Sigara tusingeshangaa, maana huduma ingepatikana kote. Lakini kilichofanyika ni kulitenga eneo moja sawa na gereza la kisiwani.