Waliohukumiwa kunyongwa kwa mauaji ya bodaboda waachiwa huru

Arusha. Mahakama ya Rufani imebatilisha adhabu ya kunyongwa hadi kufa iliyokuwa imetolewa dhidi ya Hamis Ernest na Renatus Simon, waliokuwa wamepatikana na hatia ya kumuua dereva wa bodaboda, Gervas Genus.

Kuachiwa kwao kumetokana na Mahakama ya Rufani kubaini kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha shitaka hilo bila kuacha shaka.

Uamuzi huo umetolewa Februari 27, 2026 na jopo la majaji watatu, Dk Mary Levira, Gerson Mdemu na Issa Maige na nakala ya hukumu kuwekwa kwenye tovuti ya Mahakama.

Katika hukumu yao, majaji hao walisisitiza kanuni ya msingi katika sheria ya jinai, kwamba mzigo wa kuthibitisha shtaka upo kwa upande wa mashtaka, na mshtakiwa hawezi kuhukumiwa kwa udhaifu wa utetezi wake, bali kwa nguvu ya ushahidi wa mashtaka.

Kwa mujibu wa kumbukumbu za kesi, marehemu Gervas, aliyekuwa akiishi na kaka yake, aliondoka nyumbani Aprili mosi 2015 kwenda kazini, lakini hakurejea.

Baada ya siku kadhaa za utafutaji, Aprili 11, 2015, mwili wa mtu aliyekatwa kichwa ulikutwa katika Msitu wa Bugulula, mkoani Geita.

Mwili huo ulikuwa umeanza kuoza na kutambuliwa kwa ma mavazi yaliyopatikana eneo la tukio.

Washtakiwa walifikishwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza wakikabiliwa na shtaka la mauaji wakidaiwa kutenda kosa hilo Aprili mosi 2015 katika msitu huo.

Upande wa mashtaka uliita mashahidi sita na kuwasilisha vielelezo sita.

Miongoni mwa ushahidi uliotolewa ni madai kwamba mrufani wa pili alikamatwa na kukiri kuhusika na mauaji, akidaiwa kuwaongoza polisi hadi eneo la tukio walikopata mabaki ya mwili, ikiwamo kipande cha mguu wa binadamu, fuvu la kichwa, shati na suruali ya jinsi zilizokuwa zimechakaa, pamoja na kipande cha kamba kilichodaiwa kutumika kumfunga marehemu.

Baba wa marehemu, aliyekuwa shahidi wa kwanza, alieleza kuwa alitambua mwili wa mwanawe kwa mavazi yaliyopatikana.

Hata hivyo, shahidi mwingine alidai kuwa nguo hizo zilikuwa zimechakaa kiasi cha kutotambulika kirahisi.

Daktari aliyechunguza mabaki alithibitisha kuwa fuvu lililopatikana lilikuwa la binadamu na chanzo cha kifo kilitajwa ni damu kuganda.

Washtakiwa walipofika kujitetea, walikana kuhusika na mauaji hayo.

Mrufani wa kwanza alidai kuwa alikamatwa Aprili 11, 2015 na kuhojiwa na polisi, lakini maelezo yaliyoandikwa hayakusomwa kwake.

Alikana pia madai ya kuwaongoza polisi hadi msituni kama ilivyodaiwa na mashtaka.

Mahakama Kuu iliridhika kwamba ushahidi wa upande wa mashtaka, ukiwamo maelezo ya onyo na maungamo ya ziada yaliyorekodiwa na Ofisa Mtendaji wa Kata, ulitosha kuthibitisha shtaka la mauaji bila shaka.

Ilitoa hukumu ya kifo kwa washtakiwa wote wawili.

Hata hivyo, katika rufaa yao, warufani waliwasilisha sababu 12 wakipinga hukumu hiyo.

Walipinga uhalali wa maelezo ya onyo wakidai yalirekodiwa nje ya muda wa kisheria bila kuongezewa muda.

Pia, walipinga maungamo yaliyorekodiwa na Ofisa Mtendaji wa Kata kwa madai kuwa hayakufuata taratibu za kisheria za kurekodi maungamo ya mahakamani.

Hoja kubwa ilihusu utambuzi wa marehemu. Mawakili wa warufani walidai kuwa mwili uliopatikana ulikuwa umeoza na haukuwa kamili, vilevile hakuna kipimo cha kisayansi kama DNA kilichofanywa kuthibitisha kuwa mabaki hayo yalikuwa ya Gervas Genus.

Aidha, mashahidi waliotajwa katika ripoti ya uchunguzi wa maiti kuwa walimtambua marehemu hawakuitwa mahakamani kutoa ushahidi.

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali aliitetea hukumu ya Mahakama Kuu akisema utambuzi kupitia mavazi ulitosha, akirejea uamuzi wa awali wa Mahakama ya Rufani ulioruhusu utambuzi wa marehemu kupitia mavazi yake.

Hata hivyo, alikiri kuwa maelezo ya onyo yalirekodiwa nje ya muda wa kisheria na kuomba yaondolewe kwenye ushahidi, akisisitiza kuwa hata bila maelezo hayo, maungamo ya ziada na ushahidi mwingine vilitosha kuthibitisha hatia.

Katika uchambuzi wake, Mahakama ya Rufani ilibaini dosari kadhaa katika ushahidi wa mashtaka.

Ilieleza kuwa shahidi aliyedai kutambua mavazi hakutoa maelezo ya aina ya nguo alizovaa marehemu siku ya tukio.

Zaidi, hakuna ushahidi wa kisayansi uliowasilishwa kuthibitisha utambulisho wa mwili.

Mahakama pia ilibaini kuwa maelezo ya onyo yalirekodiwa kinyume cha sheria na hivyo kuyaondoa kwenye ushahidi.

Kuhusu maungamo ya ziada, majaji walieleza kuwa marehemu hakutajwa kwa jina, bali alitajwa kama “dereva wa pikipiki,” hali iliyofanya isiwezekane kuthibitisha bila shaka kuwa aliyedaiwa kuuawa alikuwa Gervas aliyekuwa ametajwa katika mashtaka.

Aidha, kulikuwa na mkanganyiko kuhusu eneo la tukio, mashahidi wakitaja maeneo tofauti bila ufafanuzi wa kutosha.

Mahakama ilihitimisha kuwa mkanganyiko huo uliathiri kiini cha shtaka na kuacha mashaka yenye msingi.

Kutokana na mapungufu hayo, Mahakama ya Rufani iliruhusu rufaa, ikafuta hukumu na adhabu ya kifo iliyotolewa dhidi ya warufani na kuamuru waachiwe huru mara moja, isipokuwa kama wanashikiliwa kwa sababu nyingine halali za kisheria.