Raoma, Vodacom Wazindua Mfumo wa Kidijitali ‘SOMO’ Chini ya Kampeni ya Twende Zetu Darasani

Taasisi isiyo ya kiserikali ya RAOMA Foundation kwa kushirikiana na kampuni ya teknolojia na mawasiliano ya Vodacom Tanzania Plc leo wamezindua mfumo mpya wa kidijitali wa elimu unaoitwa SOMO, chini ya kampeni mpya ya Twende Zetu Darasani.

SOMO ni mfumo wa kidijitali ulioundwa mahususi na Vodacom Tanzania Plc ili kusaidia ufundishaji na ujifunzaji wa masomo yote kwa kuzingatia mtaala wa elimu wa taifa. Mfumo huu unamuwezesha Mwalimu kufundisha wanafunzi walio katika maeneo mbalimbali nchini kwa wakati mmoja.

Mfumo huu unalenga kuimarisha juhudi zilizopo katika sekta ya elimu, kuunganisha shule na walimu kupitia teknolojia na kutoa zana shirikishi kwa wanafunzi na walimu, ili kuhakikisha elimu ya kisasa, yenye ubora na ya kidijitali inapatikana kwa kila mwanafunzi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, muwakilishi wa Naibu Waziri wa Elimu Wanu Ameir Hafidh, Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, wa Wizara ya Elimu Prof. Ladslaus Mnyone alisema;

“Tukiwa tunaelekea kufikia Dira ya Maendeleo ya 2050 ya kuwa uchumi wa dola trilioni moja za Marekani, tunatambua kuwa elimu ndiyo msingi mkuu wa mafanikio hayo. Kupitia matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika ufundishaji na ujifunzaji, tunaongeza fursa za elimu, tunaimarisha ubora wake na tunawaandaa watoto wa Kitanzania kuwa na maarifa na stadi zitakazochochea maendeleo ya taifa letu. Napenda kuwapongeza Rauma Foundation pamoja na Vodacom kwa ushirikiano huu muhimu. Mfumo huu umebuniwa na wataalamu wetu wa ndani kwa ajili ya kuwahudumia watoto wa Kitanzania, haya ni mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu,”

Taasisi ya RAOMA inashirikiana na Vodacom Tanzania, ili kuhakikisha ndoto za wanafunzi mbalimbali mashuleni zinatimia kupitia teknolojia. Ushirikiano huu ni mfano wa jinsi sekta binafsi inaweza kusaidia kuboresha huduma za elimu nchini.

“Tunaendelea kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, TAMISEMI pamoja na wadau wengine wa maendeleo na sekta binafsi, ili kuhakikisha mfumo huu unafika kila shule na kufanikisha elimu bora kwa kila mwanafunzi,” alisema Mkurugenzi wa RAOMA Foundation Rahma Abdallah.

Kwa upande wake, Vodacom Tanzania ambaye ni Mkuu wa Bidhaa za Biashara na Suluhisho Ali Z. Ali alifafanua kwamba ubunifu huu ni mojawapo ya malengo ya kampuni hiyo ili kuipeleka Tanzania kwenye ulimwengu wa Kidijitali.

“Mojawapo ya malengo yetu ni kuipeleka Tanzania katika ulimwengu wa kidijitali, na hivyo sisi tumekuja na ubunifu wa mfumo huu wa kidijitali utakaowezesha Mwalimu mmoja kufundisha shule kadhaa au idadi kadhaa ya wanafunzi katika maeneo mbalimbali bila yeye kuwepo pale,” alisema Bw Ali.

Uzinduzi wa SOMO ni hatua muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea elimu jumuishi, ya kidijitali na yenye ubora, huku ukilenga kuandaa kizazi cha baadaye chenye ujuzi wa kidijitali na kinachoweza kushindana kimataifa.