Morogoro. Wakati mvua zikiendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Dunstan Kyobya, ametaka miradi ya miundombinu kukamilika kwa wakati ili kuepusha wananchi kukwama kwenye shughuli zao za kiuchumi.
Jana Ijumaa, Februari 26, 2026 akiwa katika ziara ya kukagua hali ya barabara na madaraja, Kyobya amemuagiza mkandarasi anayejenga Daraja la Mto Mfuji lililopo Kata ya Masagati, Halmashauri ya Mlimba, kuhakikisha mradi huo unakamilika Machi 10, 2026.
Amesema haridhishwi na sababu zilizotolewa kuhusu kuchelewa kwa ujenzi huo, akisisitiza kuwa daraja hilo ni kiungo muhimu kwa wakazi wa eneo hilo, hususan wakulima na wafanyabiashara wanaolitegemea kusafirisha mazao na bidhaa zao.
“Daraja hili ni muhimu kwa uchumi wa wananchi wa Masagati na maeneo jirani. Hakuna sababu ya kuchelewesha mradi wa aina hii,” amesema Kyobya.
Akizungumzia hali ya miundombinu katika kipindi hiki cha mvua, amesema licha ya mvua kunyesha kwa wingi, barabara nyingi bado zinapitika, huku zile zilizoanza kuharibika zikifanyiwa matengenezo na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ili kuzuia usumbufu kwa watumiaji.
Meneja wa Tarura Wilaya ya Kilombero, Sadick Karume amesema katika ziara hiyo wamekagua pia miradi minne muhimu ikiwamo ujenzi wa makaravati matano katika Barabara ya Mlimba-Miembeni, Daraja la Isago linalounganisha Kijiji cha Mngeta na Isago, pamoja na daraja la muda la Mbasa lililopo Kata ya Mngeta.
Amesema lengo la ziara hiyo ni kutathmini utekelezaji wa miradi na kubaini changamoto zinazohitaji ufumbuzi wa haraka, hasa katika kipindi hiki cha mvua.
“Miundombinu hii imekuwa na changamoto kwa muda mrefu wakati wa masika, hali inayosababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi na wafanyabiashara. Jitihada hizi zinalenga kuhakikisha barabara zinakuwa salama na zinapitika muda wote,” amesema Karume.
Wakati huohuo, baadhi ya wananchi wa Halmashauri ya Mlimba wameishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ukarabati na matengenezo ya miundombinu wilayani humo, wakisema hadi sasa hakuna uharibifu mkubwa licha ya mvua zinazoendelea kunyesha.
Mmoja wa wananchi hao, Venance Lebel amesema mvua zinazonyesha ni za kawaida kwa eneo hilo, tofauti na miaka iliyopita, safari hii barabara, madaraja na makaravati vimehimili hali hiyo kwa kiwango kikubwa.
“Hali si mbaya kama ilivyokuwa zamani. Tunaona maboresho yameanza kuleta matokeo,” amesema Lebel.