Mtanzania adai kuteswa Uarabuni, aomba msaada kurejeshwa Tanzania

Dar es Salaam. Wakati Afrika Mashariki ikiendelea kufuatilia kwa hofu hatima ya mfanyakazi wa ndani kutoka Uganda, Vicky Ajok, anayekabiliwa na hukumu ya kunyongwa nchini Syria, simulizi nyingine ya maumivu inamhusu Mtanzania, Zaidatu Hasani Rashid, anayepitia mateso katika Falme za Kiarabu na sasa anataka kurudi Tanzania.

Zaidatu alisafiri Agosti 30, 2025 kwenda katika nchi hiyo akiwa na matumaini ya kujiongezea kipato kupitia kazi za ndani. Lakini ndoto zake zimegeuka kuwa mzunguko wa mateso, unyanyasaji na kunyimwa nyaraka zake muhimu, ikiwemo pasipoti.

Alipowasili Septemba 4, 2025, alianza kazi yake ya kwanza ya ndani. Ingawa mwanzoni aliona dalili za matumaini, baadaye hali ilianza kubadilika. Ingawa alijipa moyo akiamini changamoto alizokutana nazo huenda zilitokana na kutokuelewana na mwajiri wake.

Baada ya hapo mambo hayakwenda sawa. Alianza kuhesabu nyumba alizofanya kazi hadi kufikia sita; hakuna hata moja aliyodumu zaidi ya miezi miwili, ama aliomba alirudishwa ofisini au kurejea mwenyewe kwa hiari yake.

Katika kipindi chote hicho, hakulipwa mshahara wowote, kwa muda mfupi aliokuwa amefanya kazi.

Hali hiyo ilimlazimu kuzungumza na wakala wake na kumweleza kuwa kazi imemshinda, akitaka afanyiwe utaratibu wa kurejea Tanzania ili ajipange upya.

Hata hivyo, mipango hiyo ilikwama baada ya wakala wake kumpatia masharti ambayo yamegeuka kitanzi hadi sasa.

Akizungumza na Mwananchi akiwa huko Uarabuni, Zaidatu amesema miongoni mwa masharti aliyopewa ni kulipa gharama zote, ikiwemo nauli ya ndege kutoka Tanzania kwenda Uarabuni, vibali na gharama nyinginezo zinazozidi Sh2.4 milioni.

“Ni fedha ambayo siwezi kuipata, kwani sehemu zote nilizofanya kazi mishahara ilikuwa ikichukuliwa na ofisi (wakala). Kwa kuwa mambo yamekuwa magumu, niliomba wanipunguzie gharama na nyingine nitalipa nikifika Tanzania, ninachohitaji ni kufika kwanza nyumbani,” amesema.

Zaidatu, ambaye kwa sasa amepata hifadhi ya muda kutoka kwa raia wa Kenya, anayefanya shughuli za ndani Uarabuni, amesema mawakala wake wa Tanzania na wa Falme za Kiarabu wamemfungia milango na kuendelea kushikilia pasipoti yake kushinikiza warejeshewe gharama zao.

“Baada ya kuona hali inazidi kuwa ngumu, na kwa kuwa nilifuata utaratibu wa Serikali kuja huku, nilienda Ubalozini kueleza ninayopitia. Walizungumza na wakala wangu na kumtaka anisafirishe kurudi nyumbani kwa kuwa kazi imenishinda. Nilipofika ofisini kwa wakala wangu, alikataa akitaka hadi nirudishe gharama zao” amesema.

“Nimepata hifadhi ya muda wa wiki mbili kutoka kwa msamaria mwema, raia wa Kenya, katika eneo la Port Saeed, Dubai. Naomba msaada wa kisheria na kidiplomasia ili nirejeshewe pasipoti yangu, nilipwe haki zangu na kurejea nyumbani salama,” amesema Zaidatu

Mwananchi ilipozungumza na Kaimu Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Falme za Kiarabu, Mohammed Bakari Ameir kuhusu changamoto ya Zaidatu, amekiri kufahamu taarifa za binti huyo aliyefika ofisini kwake kueleza matatizo anayokumbana nayo.

“Baada ya kumsikiliza, nilizungumza na ofisi yake na kushauri wamrudishe nyumbani kwa kuwa kazi imemshinda, na watafute mtu mwingine kuziba nafasi yake. Haya ni mambo yanayotokea mara kwa mara. Lakini utekelezaji haukufanyika na binti huyo hakurudi Ubalozini kueleza kama wamekataa,” amesema.

Balozi amesema mazingira hayo yanafanana na biashara; si kila jambo huzaa faida, wakati mwingine hupatikana hasara.

Hivyo, amesisitiza binti huyo arejeshwe nyumbani, na akifika Tanzania wakae na kuangalia namna ya kurejesha gharama zilizotumika.

Kwa upande wake, wakala aliyemsafirisha Zaidatu kutoka Tanzania, Anath Iterere amekiri kufahamu hali ya Zaidatu, lakini amesisitiza kuwa lazima alipe gharama walizotumia ili apatiwe pasipoti yake.

“Kwanza aliondoka ofisini, hatujui alipo kwa sasa. Arudi ofisini na alipe gharama tulizotumia ili tumpatie pasipoti yake aweze kurudi Tanzania,” amesema.

Naye wakala wake katika Falme za Kiarabu, aliyefahamika kwa jina la Aziza, amesema wanajua kazi imemshinda Zaidatu, lakini madai mengine hayana msingi wowote, isipokuwa wanachohitaji ni kulipwa gharama zao, akifanya hivyo pasipoti yake itarejeshwa.

“Paspoti yake iko salama, tunachohitaji ni kurejeshewa gharama zetu,” amesema.

Mwenyekiti wa Muungano wa Mawakala wa Ajira Tanzania nje ya nchi (TRAA), Abdallah Khalid amesema pale inapotokea mfanyakazi ameshindwa kazi kama ilivyomtokea Zaidatu, suluhu ni kampuni iliyomsafirisha kumrudisha nyumbani.

“Tunaweza kufika hadi serikalini, lakini mwisho wa siku kampuni iliyomsafirisha ndiyo inatakiwa kumrudisha Tanzania na kutafuta mfanyakazi mwingine kuziba nafasi hiyo. Hakuna namna nyingine,” amesema.

Zaidatu amesema katika kazi yake ya kwanza alipewa majukumu mazito bila mapumziko, huku akinyanyaswa kingono na mwajiri wake. Baada ya mwezi mmoja na siku 20, alirudishwa ofisini bila kulipwa mshahara na kuambiwa aanze kazi upya.

Amesema alihamishwa kutoka nyumba moja hadi nyingine. Katika baadhi ya nyumba, alidumu kwa siku chache tu kabla ya kurejeshwa ofisini bila maelezo.

Katika nyumba ya nne, amesema alipelekwa kufanya kazi ya kulea wazee bila uzoefu, jambo lililomlazimu kuomba kurejeshwa ofisini. Hata hivyo, kila aliporudishwa, alitakiwa aanze kazi upya bila kulipwa haki zake.

Akiielezea nyumba ya sita, Zaidatu amesema hapo ndipo alivunjika moyo kabisa.

Amedai alikuwa akiamka saa 10 alfajiri na kulala saa 8 usiku bila mapumziko ya kutosha, huku mshahara wake ukiendelea kuzuiwa ofisini.

Mbali na mazingira magumu ya kazi, amedai alinyimwa fursa ya kuwasiliana na familia yake nchini Tanzania, hata wakati binti yake alipokuwa amelazwa hospitalini.

Amesema usiku mmoja majira ya saa 2:30 alitolewa nje ya ofisi na kulazimika kukimbilia kituo cha polisi kwa hofu ya usalama wake, ambako alikesha nje hadi asubuhi kwa kukosa mahali pa kuishi.