Bunge lawaita wananchi kushiriki marathoni

MBUNGE wa Makete na Mwenyekiti wa Bunge Bonanza, Festo Sanga amewataka wananchi kujumuika na wabunge katika mbio za marathoni za Bunge zinazotarajiwa kufanyika Julai 18, mwaka huu.

Mbio hizo zinalenga kuchangia damu salama na kuimarisha afya.

Marathoni hiyo ambayo ni ya msimu wa tatu inatarajiwa kufanyika katika viwanja vya Jamhuri, Dodoma ikikutanisha wakimbiaji wa kilomita tano, 10 na 21 zikishirikisha wananchi, wabunge na wanariadha kutoka nje.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Sanga amesema kauli mbiu ya marathoni hiyo ni ‘Njoo Ukimbie na Mbunge Wako’ ni wito wa ushiriki kwa lengo la kuimarisha afya na uhusiano kati ya wabunge na wananchi.

Amesema wakimbiaji kutoka Kenya na Uganda walishiriki msimu uliopita na sasa wanatarajia kuwapo wanariadha kutoka Ethiopia kutokana na ubora wa mbio hizo ambazo zinasimamiwa kwa kukidhi ubora na wakimbiaji kuingia katika rekodi.

Aliongeza kuwa msimu huu wanatarajia kuandika rekodi kwa kuwa marathoni bora kwa malipo kwa washindi ambapo mshindi wa kwanza wa kilomita tano atajinyakulia kitita cha Sh5 milioni huku wa pili akipata milioni mbili na wa tatu Sh1 milioni.

“Mshindi wa kwanza kwa mbio za kilomita 10 atajipatia kitita cha Sh3 milioni, wa pili atapata milioni mbili na wa tatu atajishindia milioni moja wakati kilomita 21 mshindi wa kwanza Sh6 milioni, wa pili atapata milioni tatu na wa tatu milioni 1.5. Ni zawadi kubwa kuwahi kutolewa kwenye marathoni yetu na zinatolewa chini ya Spika Idd Zungu,” amesema  Amesema wameamua kuonyesha wapo pamoja na jamii kwa kuhakikisha wanatumia mbio hizo kuchangia damu salama ambapo washiriki watapata nafasi ya kutoa damu na wanatarajia kuvunja rekodi ya washiriki wa mbio hizo ambazo mwaka jana walikuwa na 5,200.

Mkurugenzi wa Silent Ocean, Mohamed Soloka ambao ndio wadhamini wa marathoni hiyo amesema: “Rais amekuwa muhimili mkubwa kwenye kuhamasisha michezo amekuwa chachu kuwahamasisha wanamichezo mbalimbali kujiweka sawa tunamshukuru kwa kuweza kutukumbusha na kutuhamasisha.  “Tumedhamini kwasababu sisi ni wafanyabiashara wa nchi nzima ni rahisi kuungana na Bunge kwa sababu tupo pamoja na wananchi, lakini pia kufikisha ujumbe kwa Watanzania.

“Bunge ni nguzo ya nchi, naamini Bunge Marathon msimu huu itakuwa bora kuliko misimu yote mitatu iliyopita.”

Soloka alitoa wito kwa wadau wa michezo na Watanzania wote kujitokeza kushiriki mashindano hayo kwa ajili ya kulinda afya.