Dabi ya rekodi, heshima, ubabe

NGOJA tuone itakuwaje? Yanga itaendeleza ubabe wake mbele ya Simba, au Wekundu wa Msimbazi watakataa unyonge na kufungua ukurasa mpya wa kurudisha heshima yao katika Dabi ya Kariakoo.

Huko mitaani tambo zinazoendelea kutoka pande zote ni ushindi, kwa maana nyingine ni kwamba “mpinzani hatoki”. Hii ni mechi ya 115 katika Dabi ya Kariakoo inayokwenda kuchezwa leo Jumapili kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar ambapo Yanga itakuwa mwenyeji wa Simba. Mechi hiyo itaanza saa 2:15 usiku.

Ingawa timu hizo mbili zimewahi kukutana visiwani hapa, mechi hizo zilikuwa za mashindano tofauti na Ligi Kuu, hivyo kwa timu itakayopata ushindi leo, itakuwa imejiwekea historia ya aina yake.

Pambano hilo ni la kwanza la Ligi Kuu Bara kwa msimu huu na la kwanza kwa vigogo hao kukutana Zanzibar kwa mechi ya Ligi Kuu. Awali timu hizo zimeshakutana mara sita kwa michuano yote kupigwa Amaan tangu 1975.

Rekodi zinaonyesha Yanga na Simba zilishakutana mara sita katika mechi za michuano ya Kombe la Mapinduzi, Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame Cup) na Ligi ya Muungano na katika mechi hizo Yanga imeshinda mbili na Simba mara nne ikiwamo ya Kagame, Ligi ya Muungano na mbili za Kombe la Mapinduzi fainali ya 2011 na nusu fainali ya 2017.

Kama zilivyo mechi za dabi, pambano hili linatazamiwa kuwa na ushindani kama kawaida.

Jambo ambalo ni rahisi kutabirika kwa mchezo huo ni kuteka hisia za mamilioni ya wadau na mashabiki wa mpira wa miguu Tanzania kabla, wakati ukiendelea na baada ya kumalizika.

Ni mchezo ambao ushindi una maana kubwa zaidi ya pointi tatu kwani huashiria ufahari na ubabe wa soka katika nchi kwa timu itakayopata matokeo ya ushindi huku ukiacha unyonge kwa ile itakayopoteza.

Matokeo ya ushindi yatafanya mbio za ubingwa zizidi kuwa rahisi kwa Yanga lakini kwa Simba, maana yake yataendelea kuiweka katika mbio kutokana na historia ya timu hizo mbili kutoangusha pointi kirahisi kwenye Ligi.

Ikiwa itapata ushindi, Yanga itaongeza pengo la pointi baina yake na Simba kufikia nane (8) kwani itafikisha pointi 31 kwa vile hivi sasa tayari imeshakusanya pointi 28 katika michezo 10 na ipo kileleni mwa msimamo wa ligi. Simba iliyo katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 23, ushindi kwenye mechi ya leo utaifanya ipunguze pengo la pointi baina yake na Yanga na JKT Tanzania zilizo juu yake kubakia mbili na hivyo kuyafanya matumaini yake ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu kuwa makubwa tofauti na iwapo ikipoteza.

Ikumbukwe msimu uliopita, kupoteza mechi mbili dhidi ya Yanga kulichangia kwa kiasi kikubwa Simba ikose ubingwa wa Ligi Kuu kwani msimu ulipomalizika ilikuwa imezidiwa kwa pointi nne huku.

Ni mchezo ambao unaweza kuifanya Yanga izidi kuboresha rekodi yake ya ubabe wa miaka ya hivi karibuni dhidi ya Simba ambapo imepata ushindi mara sita mfululizo dhidi ya Watani wao katika mechi baina yao za mashindano tofauti. Katika mechi hizo sita mfululizo ambazo Yanga imeshinda, yenyewe imefunga mabao 12 na imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili tu huku ikimaliza bila kufungwa bao katika mechi nne mfululizo.

Kwa Simba hiyo ni mechi ya kumaliza unyonge dhidi ya Yanga kwa muda mrefu lakini pia kudhihirisha kwamba awamu hii imeimarika zaidi kulinganisha na mechi za hapo nyuma ambazo imetoka kupoteza dhidi ya Yanga.

Refa mwenye umri wa miaka 50, Nassoro Mwinchui kutoka Tanga ndiye atachezesha mechi hiyo baina ya Yanga na Simba.

Umri huo wa miaka 50, unamfanya Mwinchui kuwa refa mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kuchezesha Dabi ya Kariakoo.

Ukiondoa kuchezesha kwa mara ya kwanza mechi ya Watani wa Jadi kwenye Ligi Kuu, Mwinchui anakuwa refa wa kwanza asiye na beji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA) kusimama katikati katika mchezo wa Ligi Kuu wa Dabi ya Kariakoo baada ya kipindi cha miaka mitatu na miezi 11 kupita.

Mara ya mwisho kwa refa asiye na beji ya FIFA kuchezesha mechi ya Ligi Kuu baina ya Yanga na Simba ilikuwa ni Julai 3, 2021 ambapo timu hizo zilichezeshwa na Emmanuel Mwandembwa, Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Baada ya hapo, mechi nane zilizofuata zilichezeshwa na marefa ambao walikuwa na beji za FIFA.

Hapana shaka Simba itapaswa kutafuta namna nzuri ya kumdhibiti mshambuliaji wa Yanga, Laurindo Aurelio ‘Depu’ ambaye ameonyesha uwezo mkubwa wa kufumania nyavu tangu alipojiunga na Yanga katika dirisha dogo la usajili.

Kuthibitisha hilo, katika mechi nne alizoichezea Yanga kwenye Ligi Kuu hadi sasa, amefumania nyavu mara tano na mchezaji mwingine ambaye Simba itapaswa imtazame kwa jicho la ziada ni Prince Dube aliyefunga mabao matatu katika mechi nne zilizopita za Yanga kwenye ligi.

Yanga yenyewe itapaswa kuhakikisha inampa uangalizi mkubwa Anicet Oura ambaye ameifungia mabao mawili Simba tangu ajiunge nayo na mwingine ni Libasse Gueye ambaye naye amefunga mawili katika mechi nne zilizopita za Simba kwenye ligi.