Vyombo vya habari vya Serikali ya Iran vimethibitisha kuwa Kiongozi Mkuu wa taifa hilo, Ayatollah Ali Khamenei ameuawa katika ofisi yake kufuatia mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya Iran, baada ya taarifa za awali kutoka kwa maofisa wa Marekani na Israel kudai kuuawa kwake.
Kwa mujibu wa Al Jazeera, kipindi cha maombolezo cha siku 40 kwa kiongozi huyo wa muda mrefu wa Iran kimetangazwa.
Rais wa Marekani, Donald Trump aliandika katika mtandao wake wa Truth Social mapema leo kuwa Khamenei mwenye umri wa miaka 86 aliuawa katika mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel yaliyoanza jana Jumamosi, Februari 28, 2026.
“Hakuweza kuepuka mifumo yetu ya kijasusi na ufuatiliaji wa hali ya juu sana, na kwa kufanya kazi kwa karibu na Israel, hakukuwa na jambo lolote ambalo yeye, au viongozi wengine waliouawa pamoja naye, wangeweza kufanya,” Trump ameandika.
“Hii ndiyo fursa kubwa zaidi kwa watu wa Iran kurejesha nchi yao,” amesema. “Tunatumaini IRGC (Jeshi la Ulinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu) na Polisi wataungana kwa amani na wazalendo wa Iran.”
Ingawa mamlaka za Iran kwa muda mrefu zimekuwa na mpango iwapo Khamenei angeuawa katika tukio la vita na Marekani na Israel, kuuawa kwake kunaongeza hali mpya ya sintofahamu katika mzozo unaoendelea, ambao tayari umeibua hofu ya kupanuka na kuongezeka kwa mapigano.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, pia, hapo awali alidai kuwa kulikuwa na “dalili zinazoongezeka” kuwa Khamenei ameuawa.
Aidha, shirika la habari la Reuters, likimnukuu ofisa mmoja mwandamizi wa Israel ambaye hakutajwa jina, liliripoti kuwa mwili wa Khamenei ulikuwa umepatikana.
Khamenei amekuwa kiongozi mkuu wa Iran tangu mwaka 1989, akimrithi Ayatollah Ruhollah Khomeini, mwanzilishi wa Iran ya baada ya utawala wa Shah, aliyeongoza Mapinduzi ya Iran ya mwaka 1979.
Kiongozi mkuu huyo ana mamlaka ya mwisho juu ya mihimili yote ya serikali, jeshi na mahakama, pamoja na kuwa kiongozi wa kiroho wa taifa hilo.
Barbara Slavin, mtafiti mwandamizi katika Kituo cha Stimson kilichopo Washington, DC, ameiambia Al Jazeera kuwa Iran “ina mpango” iwapo kifo cha Khamenei kitathibitishwa.
“Huenda baraza likaundwa kuendesha nchi. Inawezekana tayari limekuwa likiendesha nchi, kadri tunavyojua,” alisema.
Trump aashiria mashambulizi kuendelea
Mashambulizi ya Jumamosi dhidi ya Iran yalilenga mikoa 24 na kuua takribani watu 201, kulingana na vyombo vya habari vya Iran vilivyonukuu Shirika moja la msaada.
Miongoni mwa mashambulizi hayo, Israel ilishambulia shule mbili nchini Iran, na kuua takribani watu 108 katika Shule ya Msingi ya Wasichana ya Shajareh Tayyebeh katika mji wa Minab kusini mwa nchi hiyo, na wengine wawili katika shule moja mashariki mwa mji mkuu, Tehran.
Netanyahu alisema katika hotuba yake kuwa “viongozi wengi waandamizi” wameuawa katika wimbi la mashambulizi yaliyolenga viongozi wa juu, huku Trump akitoa wito wa kuangushwa kwa serikali.
Israel, kwa mujibu wa Netanyahu, imewaua “makamanda wa Jeshi la Ulinzi wa Mapinduzi na maofisa waandamizi wa mpango wa nyuklia. Na tutaendelea.”
Trump aliashiria katika chapisho lake la Truth Social kuwa “mabomu mazito na ya kulenga shabaha maalum” dhidi ya Iran yataendelea “bila kukoma wiki nzima au kwa muda wowote utakaohitajika.”
Mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran Jumamosi yalisababisha mifumo ya ulinzi wa anga kufanya kazi katika nchi kadhaa zenye kambi za kijeshi za Marekani, zikiwamo Kuwait, Qatar, Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain.
Jioni ya Jumamosi, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilisema mawimbi ya tatu na ya nne ya mashambulizi ya “kulipiza kisasi” dhidi ya maeneo ya Marekani na Israel yalikuwa yanaendelea, kulingana na taarifa iliyotolewa na shirika la habari la IRNA.
Guterres atoa wito wa kupunguza mvutano
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amekiambia kikao cha dharura cha Baraza la Usalama kuwa anajutia kwa kina kupotezwa kwa fursa ya diplomasia.
“Hatua za kijeshi zina hatari ya kuchochea mlolongo wa matukio ambayo hakuna anayeweza kuyadhibiti katika eneo tete zaidi duniani,” aliliambia baraza hilo lenye wanachama 15. “Natoa wito wa kupunguza mvutano na kusitishwa mara moja kwa mapigano.”
Akilihutubia Baraza la Usalama, Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Amir Saeid Iravani, amesema Marekani na Israel “wameanzisha vita isiyochochewa na iliyopangwa mapema,” kwa kushambulia “maeneo yenye wakazi wa kiraia katika miji mikubwa kadhaa ya Iran ambako mamilioni ya watu wanaishi.”
“Hii si tu kitendo cha uchokozi, ni uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu,” alisema.
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Mike Waltz, alisisitiza kuwa hatua za kijeshi zilikuwa halali. “Iran haiwezi kuwa na silaha za nyuklia,” alisema. “Hilo si suala la siasa. Ni suala la usalama wa dunia.”
Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa, Fu Cong, amesema Beijing ina wasiwasi mkubwa kuhusu “ongezeko la ghafla la mvutano wa kikanda.”
Balozi wa Urusi, Vassily Nebenzia, amelaani mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel na kutaka Marekani na Israel “zisitishe mara moja hatua zao za uchokozi.”