Mume wangu ananikataza kufanya biashara ilihali hanitimizii mahitaji yangu na ya familia yangu. Yeye anasaidia kwao kadri Mungu anavyomjalia, ila mimi hanipi msaada wa moja kwa moja kwetu ndiyo maana nataka kufanya biashara.
Ila ananikataza kiasi anaona amekuwa kikwazo cha kuisaidia familia yangu ambapo nilikuwa nikifanya hivyo kabla hajanioa. Nafikiria kuachana naye, kabla sijafanya hivyo naomba ushauri.
Hii ni changamoto baadhi ya wanaume wanakuwa na tabia ya kukataza wake zao kujishughulisha kwa sababu na mitazamo yao. Wengi wanaamini mwanamke akijitegemea kiuchumi anakuwa jeuri na haoni thamani ya ndoa.
Hili suala si la kukubaliana nalo ingawa usitumie nguvu kumuelewesha. Tumia busara ninaamini atakuelewa.
Ila kabla sijakupa mbinu za kutumia ili kumuweka sawa, ngoja kidogo niseme na wanaume wenye tabia hii. Kama unasoma hapa mwanaume badilika, maisha ya kufungiana ndani na kumzuia mwanamke kujishughulisha yamepitwa na wakati na maisha ni magumu bila kusaidiana mtaishia kulaumiana.
Narudi kwako unasema mumeo alikukuta unahudumia familia yako kwa kufanya biashara anapaswa kulithamini hilo na utakapozungumza naye mkumbushe kuwa wewe ndiyo msaada pekee kwa familia yako na umekuwa ukiwasaidia kabla hajakuoa.
Zungumza naye kwa upole na hekima ukimueleza umuhimu wa kujishughulisha kwanza kwenye familia yenu namaanisha wewe na yeye kama wanandoa, kisha kwa familia yako inayokutegemea.
Usiwe mkali na usikate tamaa, unaweza kuzungumza naye siku ya kwanza akakataa, ila kwa busara na upole zungumza naye siku nyingine. Fanya hivyo mara kadhaa mpaka aone una nia ya hilo suala.
Lakini pengine yeye hofu yake ni kuchanganya majukumu, yaani ukianza kufanya biashara utakuwa bize kiasi cha kusahau majukumu yako kama mke. Kama huo ndiyo wasiwasi wake tafuta biashara isiyoingiliana moja kwa moja na majukumu ya mume wako au masuala ya kifamilia. Badala ya kuanzisha mradi mkubwa ambao unaweza kumkera. Mfano, unaweza kuanzisha biashara ndogo nyumbani au mtandaoni, ikiwemo kuuza bidhaa ndogo, chakula, au kutoa huduma ndogo. Njia hii inakuwezesha kutimiza lengo lako la kufanya biashara bila kukwazana na mumeo.
Hakikisha hicho kidogo kunachopatikana kwenye biashara ndogo unayofanya anakiona na kujua fedha zinafanyia nini. Ukipata mafanikio ikiwamo kuongeza mtaji na kuitunza familia yako ataelewa umuhimu wa ulichokuwa unamueleza.
Lakini kama hataki hata ufanye biashara ndogo ndogo ukiwa nyumbani ni vema ukawashirikisha viongozi wa dini au wasimamizi wenu wa ndoa ili atimize wajibu wake wa kukutunza na familia yako.
Maana kama walikuwa wanakutegemea hasa wazazi wako si kosa kwani kimfaacho mtu chake. Mkubaliane kila mwezi awe anawapa kiasi fulani cha fedha au kuwanunulia mahitaji yao ya msingi. Kuliko anavyofanya sasa, hataki ujishughulishe ili usaidie familia yako wakiwamo wazee wako anapaswa kuchukua jukumu hilo yeye tofauti na hapo atakuwa anawanyanyasa.
Nakusisitiza usimtukane wala kumfokea au kutishia usalama wa ndoa yenu, ila usikubali kukaa bila kujishughulisha.