Haya ndio madhara ya kukacha mikutano ya shule

Dar es Salaam. Wazazi waliobahatika kuuanza mwaka 2026 wakiwa na watoto katika hatua mbalimbali za masomo, mnapaswa kutambua kuwa huu ni mwaka wa mabadiliko chanya katika ushiriki wenu, hususan katika masuala yanayohusu elimu ya watoto wenu.

Ni mwaka unaopaswa kuwa wa kujitathmini na kubadili mtazamo kuhusu wajibu wa mzazi katika safari ya elimu ya mtoto.

Moja ya maeneo yanayohitaji msisitizo mkubwa ni mahudhurio ya mikutano ya wazazi shuleni. Kwa muda mrefu sasa, nimeendelea kushuhudia namna baadhi ya wazazi wanavyoichukulia mikutano hiyo kama jukumu la ziada au shughuli isiyo na tija ya moja kwa moja kwao.

Mtazamo huu umesababisha wazazi wengi kuamua kuwatuma wawakilishi, au kutojihusisha kabisa, kwa hoja kwamba shughuli zao binafsi ni muhimu zaidi.

Hata hivyo, kwa mtazamo mpana na wa kina, mikutano ya wazazi na walimu shuleni, ni nguzo muhimu katika ujenzi wa mazingira bora ya elimu na malezi ya mtoto.

Mikutano hii si ya bora liende, hapana! bali ni chombo muhimu cha kuimarisha ushirikiano kati ya shule na familia.

Kwanza ni vema wazazi au walezi wakatambua kwamba mikutano ya wazazi hutoa fursa ya kipekee ya mawasiliano ya moja kwa moja kati ya wazazi na walimu.

Kupitia vikao hivi, mzazi hupata taarifa sahihi kuhusu maendeleo ya kitaaluma ya mtoto wake, hali ya nidhamu, mahudhurio darasani pamoja na changamoto mbalimbali anazokutana nazo.

Kwa mfano, mzazi anayehudhuria mkutano anaweza kubaini mapema kuwa mtoto wake ana changamoto ya kusoma au kuandika na kwa kushirikiana na mwalimu, anaweza kuweka mikakati ya pamoja ya kumsaidia kabla tatizo halijakomaa.

Bila mikutano hii, mzazi anaweza kuchelewa kufahamu hali halisi ya mwanawe, jambo linaloweza kuathiri mustakabali wake wa kielimu.

Pili, mikutano ya wazazi ni jukwaa muhimu la ushirikishwaji katika uamuzi unaohusu shule. Maamuzi mengi yanayohusu michango ya maendeleo, utekelezaji wa miradi ya ujenzi, ununuzi wa vifaa vya kujifunzia au hata marekebisho ya sera ndogo za shule hupitishwa katika mikutano hiyo.

Hivyo, mzazi asiyeshiriki hukosa sauti katika uamuzi unaomgusa moja kwa moja mtoto wake. Mfano hai ni pale shule inapopendekeza ujenzi wa maabara au maktaba; wazazi wanaohudhuria wana nafasi ya kutoa maoni, kupendekeza vipaumbele au kubuni mbinu mbadala za kuchangia.

Hivyo, ushiriki huu huongeza uwazi, uwajibikaji na umiliki wa pamoja wa maendeleo ya shule.

Lakini pia mikutano ya wazazi huchangia kwa kiasi kikubwa kuboresha nidhamu ya wanafunzi.

Mtoto anapofahamu kuwa mzazi wake anawasiliana mara kwa mara na walimu na kushiriki kikamilifu mikutano ya shule, hujenga hali ya uwajibikaji na hofu ya kupoteza imani ya wazazi wake.

Mzazi unapaswa kutambua kwamba mikutano hiyo ya shule na wazazi ni chanzo muhimu cha kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora za malezi.

Hivyo, kupitia mijadala hiyo, mzazi anaweza kujifunza mbinu mpya za kumsaidia mtoto katika masomo ya nyumbani, kumjenga kimaadili au kumsaidia kukabiliana na mabadiliko ya kisaikolojia yanayotokana na umri.

Mfano mzuri ni mzazi anayejifunza kutoka kwa mzazi mwenzake kuhusu namna ya kudhibiti matumizi ya simu janja kwa watoto bila kuathiri masomo yao.

Mikutano hiyo ya wazazi huimarisha pia uwajibikaji wa uongozi wa shule.

Walimu na viongozi wa shule wanapokutana ana kwa ana na wazazi, hulazimika kutoa taarifa kuhusu utendaji wao, matumizi ya rasilimali na mipango ya baadaye.

Hali hii hujenga uaminifu kati ya shule na jamii inayozunguka shule. Kwa mfano, mzazi anaweza kuuliza maswali kuhusu matumizi ya michango ya shule au hatua zilizochukuliwa kuboresha ufaulu, jambo linalosaidia kuondoa sintofahamu na migongano isiyo ya lazima.

Kwa maana nyingine, mikutano ya wazazi ni sehemu muhimu ya kulea kizazi chenye misingi imara ya ushirikiano na uwajibikaji.

Mtoto anayekulia katika mazingira ambayo mzazi wake anashiriki kikamilifu masuala ya shule, hujifunza kwa vitendo umuhimu wa kushiriki katika shughuli za jamii na kutoa maoni kwa maslahi ya pamoja.

Kwa kuzingatia faida hizi zote, mwaka 2026 unapaswa kuwa mwaka ambao wazazi wanajipa ahadi ya kutokosa mikutano ya shule bila sababu za msingi.