Msifanye ndoa zenu kuwa maabara

Canada. Neno maabara si geni masikioni mwa wengi. Ni mahali pa majaribio, pa kupima nadharia, kutengeneza nyenzo na kuthibitisha uhalali wa jambo kabla halijapelekwa kwenye matumizi halisi. Mara nyingi, maabara huanzishwa kwa lengo maalumu; zikishatimiza kusudi au zikishindwa kufikia malengo, hufungwa.

Ni katika taasisi za kisayansi pekee ambapo maabara huendelea kuwapo kwa sababu ya asili ya kazi yake majaribio yasiyoisha.

Swali la kujiuliza ni hili: kwa nini baadhi ya watu wanaigeuza ndoa zao kuwa maabara?

Leo tunadurusu tabia ya wanandoa wanaoingia kwenye ndoa, kuitoka, kuingia nyingine na kuendelea na mzunguko huo kana kwamba wanajaribu nadharia mpya kila safari.

Kwa baadhi ya jamii za Pwani, neno “chuo” hutumika kwa mizaha kuashiria idadi ya ndoa alizoingia mtu. Utamsikia mtu akiulizwa, “Hiki chuo cha ngapi?” akimaanisha ndoa ya ngapi. Kichekesho hiki kinaficha uhalisia mchungu yaani  ndoa imegeuzwa majaribio.

Ingawa kuoa, kuolewa na hata kuachana ni sehemu ya maisha, si jambo jepesi kwa binadamu.

Talaka na kuvunjika kwa ndoa huacha majeraha ya kihisia, kiuchumi na kijamii. Watoto huathirika, familia hutikisika, na jamii hupoteza uthabiti wake. Je, ni nini chanzo cha “umaabara” huu wa ndoa?

Kwanza, ni kuingia kwenye ndoa bila maandalizi ya kina.

Wapo wanaoingia kwa msukumo wa mapenzi ya ghafla au presha ya jamii bila kuielewa falsafa, majukumu na miiko ya ndoa. Zamani, jamii nyingi za Kiafrika zilikuwa na taasisi maalumu za kuwaandaa vijana kwa maisha ya ndoa—jando kwa wavulana na unyago kwa wasichana.

Taasisi hizi, licha ya tofauti za kimila, zilikuwa na lengo moja: kuwafundisha vijana uwajibikaji, heshima, uvumilivu na misingi ya familia.

Ni kweli, baadhi ya desturi kama ukeketaji zilikuwa na madhara makubwa na hazina nafasi katika zama hizi. Lakini ndani ya taasisi hizo kulikuwapo mafunzo ya maisha yaliyowajenga vijana kuwa wake na waume wenye ufahamu wa wajibu wao.

Leo, nafasi hiyo imechukuliwa na mitandao ya kijamii—mahali ambako ushauri hutolewa bila uwajibikaji, na mara nyingi kwa lengo la kuvutia wafuasi badala ya kujenga familia imara.

Pili, ni mabadiliko ya kijamii yanayokwenda kasi kuliko uwezo wa watu kuyachuja. Baadhi ya maadili ya jadi yalisisitiza stadi za maisha kama heshima, usiri wa mambo ya familia, uvumilivu na bidii ya kazi za nyumbani. Leo, stadi hizi mara nyingine huonekana kama za kizamani. Hata ujuzi wa kupika au kuendesha nyumba kwa ufanisi unachukuliwa kama jambo lisilo la lazima.

Lakini ukweli ni kwamba ndoa ni muunganiko wa hisia na vitendo; mambo madogo hujenga au hubomoa.

Tatu, ni kukua kwa teknolojia. Mtandao umeleta manufaa mengi, lakini pia umefungua milango ya matarajio yasiyo halisi kuhusu ndoa. Watu wanaona picha za maisha “kamili” mtandaoni na kulinganisha na uhalisia wao. Wanapokutana na changamoto za kawaida za ndoa, hukata tamaa haraka wakidhani wamekosea chaguo—na hivyo kuanza “jaribio” jingine.

Ni muhimu kusisitiza kuwa si kila ndoa inapaswa kuendelea kwa gharama yoyote, hasa pale penye ukatili au unyanyasaji. Lakini pia si busara kuigeuza ndoa kuwa uwanja wa majaribio ya kihisia. Ndoa inahitaji maandalizi, uvumilivu na kujifunza kila siku.

Jamii inapaswa kurejea katika misingi ya maandalizi ya vijana kwa ndoa—si kwa kuiga kila mila ya zamani, bali kwa kuchukua yaliyo bora na kuyaendana na wakati.

Viongozi wa dini, wazazi na walezi wana wajibu wa kutoa mwongozo thabiti badala ya kuwaachia vijana wafundishwe na mitandao.

Ndoa si maabara. Si mahali pa kujaribu bahati kila inaposhindikana. Ni taasisi inayohitaji utulivu, maarifa na dhamira ya dhati.

Tukiendelea kuigeuza maabara, tutajenga jamii ya majaribio ambayo haidumu. Lakini tukiiimarisha kwa maandalizi na maadili, tutajenga familia imara na taifa lenye mizizi thabiti.