Kabla ya dabi, Yanga na Simba zatofautiana tena namba

WAKATI ikisubiriwa kwa hamu leo mechi ya ‘Kariakoo Derby’ itakayopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, rekodi zinaonyesha wachezaji wa Yanga wamefanya vizuri zaidi katika mechi 10 za msimu huu, tofauti na watani zao Simba.

Katika mechi hizo 10, ambazo kila timu imecheza msimu huu kwenye Ligi Kuu Bara, wachezaji tisa wa Yanga wamechukua tuzo ya mchezaji bora, huku kwa upande wa watani zao wa jadi Simba, ikishuhudiwa ni nyota saba tu, walioondoka na tuzo hiyo.

Kwa wachezaji wa Yanga, Maxi Mpia Nzengeli amebeba tuzo mbili ambazo ni za mechi ya ushindi wa timu hiyo wa mabao 3-0 dhidi ya Pamba Jiji, Septemba 24, 2025, huku nyingine ni ya Yanga ilipoifunga Namungo FC bao 1-0, Februari 22, 2026.

Nyota mwingine ni Prince Dube aliyechukua pia mbili, akianza na ya ushindi wa Yanga wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union, Desemba 7, 2025, huku nyingine ni ya kikosi hicho kilipoichapa maafande wa JKT Tanzania mabao 5-0, Februari 25, 2026.

Waliochukua tuzo mojamoja ni Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, wakati Yanga ilipoifunga Mtibwa Sugar mabao 2-0, Oktoba 28, 2025, mwingine ni Pacome Zouzoua katika mechi dhidi ya KMC FC, Yanga ikishinda mabao 4-1, Novemba 9, 2025.

Nyota wengine ni Duke Abuya aliyechukua katika ushindi wa kikosi hicho wa mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate, Desemba 4, 2025, kisha Mudathir Yahya, wakati Yanga iliposhinda mabao 6-0 mbele ya Mashujaa FC, Januari 19, 2026.

Mshambuliaji, Laurindo Dilson Maria Aurelio ‘Depu’, aliyejiunga dirisha dogo la Januari 2026, akitokea Radomiak Radom FC ya Poland, ameshinda pia tuzo moja dhidi ya Dodoma Jiji, wakati kikosi hicho kikishinda kwa mabao 3-1, Januari 27, 2026.

Depu raia wa Angola, amekuwa na mwendelezo mzuri hadi sasa tangu ajiunge na kikosi hicho, ambapo amechangia mabao sita katika Ligi Kuu, baada ya kufunga matano na kuasisti moja, akiwa ni nyota tisa waliotwaa tuzo ya mch ezaji bora wa mechi.

Kwa upande wa Simba, wachezaji wawili wametwaa tuzo mbili kila mmoja kati ya saba, ambao ni beki wa kati, Rushine De Reuck, aliyeanza katika ushindi wa timu hiyo wa mabao 3-0 dhidi ya Namungo FC, Oktoba 1, 2025.

Tuzo nyingine aliyochukua ni ya ushindi wa Simba wa mabao 2-0, dhidi ya Tanzania Prisons, Februari 22, 2026, akifuatiwa na nyota mpya, Msenegali Libasse Gueye, aliyechukua wakati timu hiyo ilipoifunga Mashujaa mabao 2-0, Januari 29, 2026.

Gueye aliyejiunga na Simba katika dirisha dogo la Januari 2026, akitokea Teungueth FC ya kwao Senegal, ameshafunga mabao mawili, huku akichukua tuzo nyingine ya mchezaji bora wakati kikosi hicho kilipoichapa KMC FC 2-0, Februari 11, 2026.

Wachezaji wengine waliochukua tuzo mojamoja ni Morice Abraham, wakati Simba ilipoifunga Mbeya City mabao 3-0, Desemba 4, 2025, sawa na beki wa kati, Wilson Nangu, katika ushindi wa kikosi hicho wa 2-1 dhidi ya JKT Tanzania, Novemba 8, 2025.

Mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025, Jean Charles Ahoua aliyefunga mabao 16, ambaye kwa sasa anacheza CR Belouizdad ya Algeria, alichukua pia tuzo moja, wakati Simba ilipoifunga Fountain Gate FC mabao 3-0, Septemba 25, 2025.