Aliyeshtakiwa kwa mauaji ya bodaboda aachiwa

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Geita, imemuachia huru Bernard Kazoya aliyekuwa ameshtakiwa kwa mauaji ya dereva bodaboda,Patrick Wales, baada ya kubaini kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kesi hiyo bila kuacha shaka yoyote.

Kazoya alishtakiwa kwa kosa la mauaji  kinyume na vifungu vya 196 na 197 vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Marejeo ya mwaka 2023,tukio lililodaiwa kutokea Septemba 11, 2024 katika Kijiji cha Businda, Wilaya ya Bukombe,mkoani Geita.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka,Patrick aliuawa kikatili na mwili wake kutupwa karibu na kilima  katika kijiji hicho.

Hukumu hiyo iliyomwachia huru, imetolewa Februari 27, 2026 na Jaji Griffin Mwakapeje, na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi tisa na vielelezo vinne huku upande wa utetezi ukiwa na mashahidi wawili.

Ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa kwamba marehemu aliyekuwa dereva bodaboda,ambaye mwili wake uligunduliwa baadaye ndani ya kijiji, akiwa na majeraha makubwa ya kichwa.

Ugunduzi wa mwili huo uliripotiwa na shahidi wa kwanza Juma Kuzoleka, ambaye alidai siku ya tukio akiendelea na shughuli zake  shambani, aligundua mwili wa kijana ukiwa umelala karibu na kilima, ukiwa na majeraha yanayoonekana kichwani, na mara moja akamjulisha mwenyekiti wa eneo hilo.

Shahidi wa pili ambaye ni Mwenyekiti wa Mtaa huo, Muhoja Sumuni, alithibitisha kupokea taarifa  hiyo na, alipotembelea eneo la tukio, aliona mwili ukiwa na majeraha kama hayo kabla ya kuripoti jambo hilo kwa polisi.

Shahidi wa tatu , Dk Mbogo Masanja, ambaye aliufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, alieleza Mahakama kuwa chanzo cha kifo hicho ni jeraha kubwa la kichwani lililosababishwa na kupigwa na kitu butu.

Shahidi wa tano, Koplo Waziri alidai kuwa uchunguzi zaidi ulilenga katika kutafuta simu ya mkononi inayoaminika kuwa ya marehemu ambayo ilikutwa kwa mshtakiwa katika mazishi kwenye Kijiji cha Namonge, Oktoba 4, 2024.

Mbele ya shahidi huru, Meshack Joseph (shahidi wa tisa) mshtakiwa alipekuliwa na kupatikana na simu ya Tecno Pop 8 yenye namba za utambulisho (Imei) inayolingana na simu ya marehemu.

Simu iliyopatikana ilikabidhiwa kwa shahidi wa tano, Sajenti Didas, mtunza vielelezo ambaye aliirekodi na kuihifadhi ambapo baadaye alipokea boksi la simu ambalo imei namba zake zinafanana na simu iliyokutwa kwa mshtakiwa.

Kwa upande wake shahidi wa sita ambaye ni shangazi wa marehemu, Getruda Kazige, alitambua simu hiyo kuwa ni ya marehemu, ambaye ndiye alitoa boksi la simu hiyo.

Shahidi wa nane, ofisa mpelelezi, alishuhudia kwamba uchunguzi ulibaini kwamba mshtakiwa na wengine walimkodi marehemu usiku wa tukio hilo na baadaye wakamshambulia na kumnyang’anya pikipiki na simu yake.

Shahidi wa saba, Sajenti Deus aliyeandika maelezo ya onyo ya mshtakiwa, alidai mshtakiwa alikiri kushiriki  mauaji hayo pamoja na wengine.

Katika utetezi wake mshtakiwa, alikana kuhusika katika mauaji hayo na kupinga mazingira ya kukamatwa kwake na madai ya kukiri kosa hilo.

Alidai kukamatwa alipohudhuria maziko ya shangazi yake ambapo maofisa wa polisi walipomkaribia, walimtaka atoe simu yake, na akaikabidhi kwa hiari yake, akieleza kwamba alikuwa ameinunua kutoka kwa Raymond Morris, Septemba 29, 2024.

Alidai kujitolea kuwapeleka polisi kwa muuzaji, lakini walishindwa kumfuatilia na kukana kwamba shahidi yeyote huru alikuwepo wakati wa upekuzi na kudai akiwa chini ya ulinzi wa polisi aliteswa na kulazimishwa kusaini taarifa, na kulazimishwa kukiri kosa ambalo hajafanya na kuomba aachiwe huru kwani alinunua simu tu ila hajahusika na mauaji hayo.

Shahidi wa pili wa utetezi, Rhoda Kazoya, ambaye ni dada wa mshtakiwa alidai kushuhudia polisi wakimchukua ndugu yake kwenye maziko kwa madai ya kumiliki simu iliyoibiwa.

Alishuhudia zaidi kwamba alipoenda kumwona baadaye katika Kituo cha Polisi cha Bukombe, alikuwa katika hali mbaya ya kimwili, akiwa na miguu iliyovimba na dalili za kupigwa.

Katika hukumu yake, Mahakama ilisisitiza kanuni ya msingi ya sheria ya jinai kwamba mzigo wa kuthibitisha shtaka unabaki kwa upande wa mashtaka wakati wote, na kiwango kinachotakiwa ni kuthibitisha bila shaka yoyote ya msingi.

Mahakama ilikubaliana kuwa kifo kilithibitishwa  na kuwa vilitokana na kitendo cha jinai. Hata hivyo, hoja kuu ilikuwa iwapo mshtakiwa ndiye aliyesababisha kifo hicho.

Jaji alieleza kuwa ingawa kupatikana kwa simu ya marehemu kwa mshtakiwa kunazua tuhuma, muda wa karibu mwezi mmoja kati ya tukio na kupatikana kwa simu hiyo, unaacha uwezekano kuwa simu hiyo inaweza kuwa ilibadilishwa kutoka mikono kadhaa.

Mahakama ilibaini kuwa hakuna shahidi aliyemwona mshtakiwa akiwa na marehemu siku ya tukio, wala hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja au wa kimazingira unaomuweka karibu na eneo la tukio.

Kuhusu maelezo ya onyo, Mahakama ilieleza kuyatilia  shaka kutokana na tuhuma za kulazimishwa na kukosekana kwa ushahidi wa kuthibitisha kuwa yalitolewa kwa hiari.

Vilevile, mahakama iliona kuwa upande wa mashtaka haukufanya jitihada za kumtafuta au kumleta mahakamani mtu aliyedaiwa kumuuzia mshtakiwa simu hiyo, jambo lililoacha pengo katika ushahidi.

Baada ya kupitia ushahidi wote, Mahakama ilihitimisha kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha bila shaka yoyote kuwa Bernard ndiye aliyemuua Patrick na kuamuru aachiliwe huru mara moja isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali.

“Baada ya tathmini ya makini na kamili ya ushahidi wote uliorekodiwa, Mahakama hii inaona kwamba upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kesi yake dhidi ya mshtakiwa bila shaka yoyote.Ninaamuru aachiliwe mara moja isipokuwa kama ameshikiliwa kwa sababu zingine za kisheria,” amesema.