WANAWAKE MABACHELA WAITWA KUCHUKUA FOMU YA KULIPIWA MAHARI


 Taasisi ya Al-Hikma imetangaza mpango wa kulipia mahari kwa vijana 130 walio tayari kuoa katika mwaka huu. 

Akizungumza leo Machi 1, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa mashindano ya Kimataifa ya Qur’aan yaliyoandaliwa na taasisi hiyo, Mratibu wa taasisi hiyo Nurdin Sheikh Kishki amesema kuwa lengo ni kuwawezesha vijana kuingia kwenye ndoa kwa urahisi zaidi. 

Amesema hadi kufikia mwaka jana, jumla ya vijana 370 walikuwa tayari wamesaidika na mpango huo tangu kuanzishwa kwake.

“Mwaka huu tuna mpango wa kuwaozesha vijana 130. Sharti jipya ni kwamba mwanamke anayetaka kuolewa ndiye atakayepaswa kuchukua fomu kwa ajili ya kumuwakilisha mumewe katika maombi ya mahari. Machi 5, 2026 tutatangaza utaratibu rasmi,” amesema.

Aidha, Sheikh Kishki ametaja masharti mengine kwa vijana watakaonufaika na mpango huo.

Amesisitiza kuwa mwanaume anayetarajia kulipiwa mahari ni lazima awe na kibarua au shughuli halali inayomuingizia kipato.

Vilevile, ameweka bayana kuwa mwanaume mwenye nia ya kuongeza mke hataruhusiwa kunufaika na mpango huo.

 Amesema lengo la taasisi ni kusaidia vijana wasio na uwezo kuanza maisha ya ndoa, si kwa wanaotaka kuoa wake zaidi.