CHONGOLO ASISITIZA ULINZI MRADI WA UMWAGILIAJI MKOMBOZI KWA MANUFAA YA WATANZANIA WOTE

 NIRC Iringa

Waziri wa Wizara ya Kilimo, Daniel Chongolo, amesisitiza ulazima wa kulindwa kwa Mradi wa Umwagiliaji Mkombozi uliopo Pawaga mkoani Iringa, akieleza kuwa uwekezaji huo wa serikali unalenga kuongeza uzalishaji wa mpunga, kuinua kipato cha wakulima na kuchangia usalama wa chakula kwa manufaa ya Watanzania wote.

Chongolo ameyasema hayo Februari 27 baada ya kutembelea mradi huo wa Umwagiliaji Mkombozi uliopo Pawaga mkoani Iringa na kusisitiza kuwa mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Taifa wa kuimarisha sekta ya kilimo kupitia matumizi ya teknolojia na miundombinu bora ya Umwagiliaji, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi, hususani wakulima wa eneo hilo, kushiriki kikamilifu katika kuutunza na kuutumia kwa tija ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu.

Aidha Chongolo amesema serikali haitavumilia biashara ya ardhi ndani ya mradi huo kwa kuwa lengo lake ni kuwainua wakulima kiuchumi kupitia kilimo cha kisasa na chenye tija.

“Mtu anayeuza au kununua ardhi ndani ya mradi huu anapoteza muda wake, ni marufuku na hatutamvumilia,” amesema Chongolo.

Naye Mkurugenzi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Raymond Mndolwa amesisitiza kuwa mifugo haitaruhusiwa kuingizwa ndani ya eneo la mradi kwa kuwa imekuwa chanzo cha uharibifu wa mifereji na kingo zake.

“Mifugo ikiingia ndani ya skimu inaharibu miundombinu tuliyoijenga kwa gharama kubwa, hivyo katazo hili ni kwa ajili ya matumizi endelevu ya mradi,” amesema Mndolwa.

Akieleza utekelezaji mradi, Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Iringa, Peter Akonaay amesema mradi wa Skimu ya Umwagiliaji Mkombozi unahusisha vijiji sita kati ya vijiji kumi na tano vya Tarafa ya Pawaga na ni uwekezaji mkubwa wa kimkakati.

“Mradi huu unatarajiwa kuongeza eneo la Umwagiliaji kutoka ekari 4,500 hadi kufikia ekari 15,000 na kuongeza uzalishaji wa mpunga kutoka tani 2 hadi tani 5 kwa hekta,” amesema.

Akonaay ameongeza kuwa pamoja na mafanikio yanayotarajiwa, changamoto kama uelewa mdogo wa matumizi sahihi ya miundombinu, mafuriko na mchanga kujaa kwenye mifereji zimekuwa zikiathiri utekelezaji, huku wakulima wakihimizwa kusafisha miundombinu mara kwa mara ili kulinda mradi.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Benjamin Sitta amesema Serikali ya mkoa itaendelea kusimamia nidhamu katika mradi huo ili uweze kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

“Hatutaruhusu uharibifu wa miundombinu wala uvunjifu wa taratibu, kila mmoja atawajibika kulinda mradi huu,” amesema Sitta.

Kwa ujumla Viongozi hao wamewataka wakulima na wafugaji kushirikiana na serikali katika kulinda miundombinu ya Umwagiliaji, wakieleza kuwa mradi huo una manufaa makubwa kwa uchumi wa kaya na taifa iwapo utasimamiwa kwa nidhamu na uzalendo.

Baadhi ya wakulima wa Pawaga wamesema wanaunga mkono agizo hilo wakiamini litapunguza migogoro ya umiliki wa mashamba na kuleta utulivu katika uzalishaji.

Mkulima Tesha Mlenga kutoka Pawaga amesema,

“Kama serikali itasimamia kwa haki, katazo hili litatusaidia sisi wakulima halisi kunufaika na mradi lakini pia tunaiomba serikali itupatie elimu ya matumizi sahihi ya mradi ili tunufaike zaidi na sio kuharibu,”