Kilio cha madawati Shule ya msingi Ziwani chasikika

Tanga. Shule ya Msingi Ziwani, iliyopo Kata ya Pongwe jijini Tanga ambayo awali ilikuwa na madarasa mawili ya darasa la tano na sita ambayo wanafunzi walikuwa wakikaa kwenye mikeka darasani, sasa imepatiwa madawati 100 ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Mbali na shule hiyo, Halmashauri ya Jiji la Tanga imekabidhi jumla ya madawati 2,900 kwa shule za sekondari zilizokuwa na uhitaji na hivyo kufanya idadi ya madawati yaliyogawiwa kufikia 3,000.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Mwananchi kuripoti hali halisi ya Shule ya Msingi Ziwani, kufuatia wanafunzi wa darasa la tano na sita kulazimika kusomea sakafuni.

Ripoti hiyo ilibainisha kuwa licha ya walimu kujitahidi kufundisha kwa bidii, mazingira ya ujifunzaji hayakuwa rafiki kwa wanafunzi hao.

Ugawaji wa madawati hayo umefanyika leo Jumapili, Machi Mosi, 2026, madawati 3,000 yalikabidhiwa kwa shule 29 za sekondari pamoja na Shule ya Msingi Ziwani.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Juma Hamsin amesema mgawo huo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha miundombinu ya elimu katika jiji la Tanga.

“Leo tumegawa madawati 3,000 kwa shule 29 za sekondari na Shule ya Msingi Ziwani. Mwezi uliopita tuligawa madawati 1,000, na Februari 22, 2026 shule ya Ziwani ilipokea madawati 90 ya mwanafunzi mmoja mmoja pamoja na 30 ya wanafunzi watatu watatu,” amesema Hamsin.

Amesema licha ya jitihada hizo, bado shule hiyo inakabiliwa na upungufu wa madawati na vyumba vya madarasa.

“Tunatambua bado kuna changamoto. Shule ya Ziwani inahitaji vyumba vinane vya madarasa. Kama mkurugenzi, nimeahidi kutenga Sh milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vinne katika awamu ya kwanza,” amesema.

Hata hivyo, amebainisha kuwa eneo la shule lina changamoto ya maji kutuama, hivyo maandalizi ya ujenzi yatazingatia ushauri wa kitaalamu ili kuepusha madhara ya baadaye.

“Tumemtaka Mwalimu Mkuu aanze maandalizi ya ujenzi. Pale panapokuwa na changamoto, kupitia madiwani, watendaji wa kata na kamati za shule, tutaendelea kuzishughulikia kwa haraka,” amesisitiza Hamsin.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Pongwe, Baraka Sadi amesema uhaba wa madawati ulikuwa ukiathiri ari na morali ya wanafunzi.

“Ni kweli wanafunzi wetu walikuwa wakikalia mikeka, hasa wa darasa la tano na sita. Ilikuwa hali ya kusikitisha, lakini tunashukuru kwa hatua hii ya Serikali,” amesema Sadi.

Ameongeza kuwa kupokea madawati hayo ni faraja kubwa kwa wazazi na wanafunzi wa kata hiyo.

Dadawati ya kisasa kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya uhaba kwenye shule za msingi na sekondari jijini Tanga.



“Tunaamini kuanzia sasa watoto wetu watasoma katika mazingira bora zaidi na kwa utulivu,” amesema.

Naye Meya wa Jiji la Tanga, Mustapha Selebosi amesema halmashauri imetumia zaidi ya Sh milioni 300 kununua madawati ya kisasa 3,000 yaliyogawiwa kwa shule husika.

“Fedha hizi ni kodi za wananchi wa Tanga. Tumeyatumia madawati haya kutekeleza azma ya kutoa elimu bora kwa vitendo,” amesema Selebosi.

Amesema maboresho hayo yataongeza hamasa kwa wanafunzi na walimu katika shule zilizopokea mgao huo.

“Hii ni hatua ya kuondoa changamoto za miundombinu katika shule zetu na kuijenga Tanga kwa pamoja,” amesisitiza.

Mbunge wa Jiji la Tanga, Kassim Amar Mbaraka amesema ongezeko la wanafunzi wanaojiandikisha shuleni limechangia uhaba wa madawati katika baadhi ya shule.

“Viongozi kazi yetu ni kuona changamoto na kuzitafutia ufumbuzi. Tutaendelea kushirikiana kukabiliana na changamoto mbalimbali katika jimbo letu,” amesema.

Hatua hiyo imepokelewa kwa matumaini mapya na jamii ya Pongwe, huku Serikali ikiendelea kuahidi kuboresha miundombinu ya elimu ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira salama na bora.