Polisi yaipiga ‘stop’ Bawacha Mei 8 Mara, Chadema yajibu mapigo

Musoma. Polisi Mkoa wa Mara imezuia maadhimisho ya siku ya wanawake yaliyoratibiwa na Baraza la Wanawake Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha) yaliyotarajiwa kufanyika Mjini Musoma mkoani humo Machi 8, 2026.

Mkutano huo ilikuwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambapo kitaifa Bawacha walipanga kuadhimisha mjini Musoma mkoani Mara.

Akizungumzia shughuli hiyo ya Bawacha leo Machi Mosi, 2026, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo amesema kuwa kitendo cha baraza hilo kupanga kufanya maadhimisho hayo ni ukiukwaji wa makusudi wa amri ya Mahakama.

Amesema Chadema imezuiliwa kutojishughulisha na masuala ya kisasa hadi kesi yao ya msingi itakapomalizika mahakamani.

Amesema Jeshi la Polisi mkoani Mara linaendelea kutambua amri hiyo ya Mahakama iliyotolewa Juni, 10,2025 kwa maelezo kuwa haijatenguliwa.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara katika wajibu wa kusimamia mnyororo wa sheria imeona picha mjongeo za Bawacha kwenye mitandao ya kijamii zikihamasisha kufanya maadhimisho siku ya wanawake mjini Musoma,” amesema Kamanda Lutumo.

Kamanda Lutumo pia amewataka viongozi wa Bawacha waliofanya kikao cha maandalizi mjini Musoma wiki iliyopita kufika katika ofisi ya mkuu wa upelelezi Mkoa wa Mara Machi 2, 2026 kwa mahojiano.

Kufuatia kauli hiyo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mara, Chacha Heche amesema kamanda wa polisi hana mamlaka kisheria kuzuia shughuli hiyo ambayo maandalizi yake yako katika hatua za mwisho.

Pia, amesema Mahakama haijazuia chama hicho kufanya shughuli zake isipokuwa imemzuia Katibu Mkuu wa chama kutotumia mali za chama.

“Tungekuwa tunatumia gari la chama ama ofisi ya chama hapo ndipo tungekuwa tumekwenda kinyume lakini hata hivyo kesi hiyo tayari imekufa kifo cha kawaida.

“Huyo RPC anapotoa hilo zuio kwa kuegemea uamuzi wa mahakama naomba umuulize yeye ana barua yoyote kutoka mahakamani kuhusu zuio hilo, pia sisi tunavyojua RPC hana uhusika wowote kwenye mambo yetu ya kisiasa kwa mujibu wa sheria za nchi,” amesema.

Heche amesema kitendo alichokifanya kamanda huyo ni kuchagua kupendelea upande mmoja huku akisema hali hiyo ni miongoni mwa mambo yanayoleta migawanyiko katika jamii jambo ambalo ni hatari kwa ustawi wa demokrasia na jamii kwa ujumla.

Amesema shughuli za kisiasa ni halali kufanyika nchini huku akirejea hotuba ya Makamu wa Rais, Dk Emmanule Nchimbi aliyoitoa jana Jumamosi, Februari 28, 2026 kwenye mazishi ya Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Kardinali Polycarp Pengo ambapo alisema kila mtu ana haki ya kufanya siasa na kuchagua upande anaoutaka, kwani ni sehemu ya kuitumikia jamii na Taifa kwa ujumla.

Amesema maadhimisho ya siku ya wanawake duniani hayana mahusiano na mambo ya kisiasa ambapo amesema kundi lolote katika jamii linaruhusiwa kufanya maadhimisho hayo ambayo lengo lake ni kuwatambua wanawake na kuendelea kuwatia moyo, ili waweze kutumika vema katika kuleta na kuchochea maendeleo ya wananchi.