Ajali ya ambulensi yaua mgonjwa, wanne wakijeruhiwa Korogwe

Tanga. Mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Zaharia Abraham (41), mkazi wa Goha wilayani Korogwe, mkoani Tanga, amefariki dunia kufuatia ajali ya gari la wagonjwa lililokuwa likimsafirisha kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo kwa ajili ya matibabu, kugongana uso kwa uso na gari la mizigo.

Ajali hiyo imetokea leo Jumapili, Machi Mosi, 2026, katika eneo la Saruji, wilayani Tanga, kwenye barabara ya Tanga–Segera.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, watu waliokuwa wakimsindikiza mgonjwa huyo wamejeruhiwa katika ajali hiyo.

Kamanda huyo amewataja majeruhi hao ni pamoja na Zainab Mdoe, Seleman Mdoe, Naiman Msofe na Hatibu Denis ambaye ni muuguzi.

“Wote walikuwa abiria wa gari hilo la wagonjwa na wamekimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo kwa matibabu,” amesema Kamanda Mchunguzi.

Amesema ajali hiyo imehusisha gari aina ya Toyota Land Cruiser Ambulance lenye namba za usajili STM 7202, mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, lililokuwa likitoka Mombo kuelekea Tanga mjini, likiendeshwa na dereva Alfonce Alfan, mkazi wa Korogwe.

“Gari la mizigo lililohusika ni aina ya Scania lenye namba za usajili T628 DSG likiwa na trela namba T637 DSG, lilikuwa likitokea Tanga kuelekea Arusha, likiendeshwa na John Pilipo mkazi wa Arusha,” amesema.

Hata hivyo, Kamanda Mchunguzi amesema uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari la wagonjwa kushindwa kulimudu gari kutokana na mwendokasi, hali iliyosababisha gari hilo kuhama kutoka upande wake wa kushoto na kuingia upande wa kulia wa barabara kabla ya kugongana uso kwa uso na lori hilo.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo kwa uchunguzi wa kitabibu na taratibu nyingine zinazofuata.

Gari la mizigo lililogongana  uso kwa usi ma gari la wagonjwa. Katika eneo la  Saruji jijini Tanga. Picha na Mbonea Herman



Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limetoa wito kwa madereva wote kuzingatia sheria za usalama barabarani, kuepuka mwendokasi na uzembe, pamoja na kufanya maamuzi sahihi wanapokuwa barabarani, likisisitiza kuwa usalama ni jukumu la kila mtumiaji wa barabara.