Uongozi Kanisa la Wasabato wapata hisia mseto ukaguzi wa CAG

Dar es Salaam. Uongozi wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) Tanzania, umevunja ukimya juu ya tuhuma za ubadhirifu wa mali huku ukifichua kwamba mgogoro huo una zaidi ya miaka mitano.

Uongozi huo umekwenda mbali zaidi na kueleza kwamba si kawaida waumini wake kupeleka malalamiko kwenye vyombo vya Serikali na si kawaida Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua makanisa, ukidai yanayotokea kuhusu tuhuma hizo si ya kawaida.

Hivi karibuni mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Frank Kanyusi alikaririwa na vyombo vya habari akieleza kuivunja bodi ya wadhamini ya kanisa hilo kufuatia tuhuma ya ubadhirifu wa mali na kushindwa kutekeleza majukumu kwa mujibu wa sheria.

Alisema Rita imechukua hatua hiyo baada ya kupokea ripoti maalumu ya CAG, iliyobaini mapungufu makubwa katika usimamizi wa mali za kanisa.

Ukaguzi huo ulifanyika kufuatia malalamiko ya wanachama waliodai kuwepo kwa ukiukwaji wa pamoja wa wajumbe wa bodi, ikiwemo matumizi mabaya ya rasilimali za taasisi na ripoti kuonyesha udhaifu wa kiutawala na kisheria.

Rita pia imesisitiza kuwasilisha ripoti hiyo kwa vyombo vingine vya dola kwa hatua zaidi za kisheria, na kanisa kupewa siku saba kuwasilisha majina ya wajumbe 10 watakaounda kamati ya muda kusimamia shughuli hadi bodi mpya itakapoteuliwa.

Akizungumza na Mwananchi leo Machi Mosi, 2026, Katibu Mkuu wa Kanisa hilo Tanzania, Unioni ya Kusini, Mchungaji Magulilo Mwakalonge amesema kabla ya ukaguzi wa CAG, vyombo vya ukaguzi vya ndani vilifanya ukaguzi na kutoa ripoti ambayo kanisa iliifanyia kazi.

“Pamoja na hayo, Serikali iliona kuna haja ya kukagua tena, katika hili kuna mengi yasiyo ya kawaida,” amesema mchungaji huyo.

Amesema Rita iliwaeleza kuona viashiria vya ubadhirifu, japo kama kanisa waliona ripoti hiyo ikikabidhiwa na CAG kwa wakala huyo siku walipoitwa.

“Huenda Rita waliisoma kabla, sisi hatufahamu, ingawa tuliona ikikabidhiwa hapo kwa mara ya kwanza na tuliambiwa ni taarifa ndefu yenye kurasa zaidi ya 100.

“Siku hiyo ililiripotiwa kwa dakika 25 kwa kifupi, kama kanisa hiyo ripoti hatujaisoma ili kujua huo ubadhirifu unaosemwa unaashiriwa kwenye nini hata hatua iliyofuata ilikuwa bold (nzito), tumeambiwa ni viashiria lakini vimepelekea kufanya huo uamuzi alioufanywa,” amesema.

Amesema wakiipokea ripoti ya CAG wataisoma na waumini wake watajulishwa kile ambacho kimeelezwa ndani ya ripoti hiyo.

Amesema kama kanisa halijafanya uamuzi wowote kwa kuwa nalo halijaipitia hiyo ripoti na kubainisha kwamba kukubaliana au kutokubaliana kwao kutategemea hicho ambacho kimeandikwa katika ripoti hiyo.

“Jambo ambalo limetushangaza ni uamuzi kutolewa kabla taarifa haijasomwa kwa uangalifu, hii inatuweka kwenye wakati mgumu ku-relate (kulinganisha) na uamuzi uliotolewa,” amesema.

Amesema kama kanisa wana hisia za uwezekano wa kuwepo kwa nia isiyo safi, japo amekiri kuwepo kwa baadhi ya waumini wao ambao wanadai walipeleka malalamiko.

“Hata siku hiyo tulikutana nao ambao wanadai walipeleka hayo malalamiko, japo kama kanisa tuna utaratibu wa ndani panapotokea vitu hivyo na kushughulikia, mfano ni suala la wizi.

Amesema kwenye suala la wizi wa fedha ni rahisi kushughulikia kwa ushahidi wa kiasi gani kimeibiwa na kimeibwa na nani.

“Kama kanisa sio mara ya kwanza kuibiwa na huwa tunafuatilia hadi mwisho  na kuwawajibisha wanaotuibia, katika ili tumeomba ushahidi ni wizi ambao umesimuliwa na kusemwa muda mrefu bila ushahidi na tunahisi ni kitu cha kufikirika,” amesema.

Akiuzungumzia sitofahamu ya wizi huo, Mchungaji Mwakalonge amesema ukaguzi ulifanyika miaka zaidi ya mitano iliyopita.

“Azimio la kwanza la kufanya ukaguzi lilifanyika mwaka 2020 na awamu kadhaa za uongozi zimepita, tuliposikia hayo vyombo vya ukaguzi vya kanisa vilifanya kazi na ikatoa mapendekezo ambayo kanisa iliyafanyia kazi.

“Ndio tunasema pamoja na hayo, Serikali iliona kuna haja ya kukagua tena, ndiyo sababu tunasema kuna mengi yasiyo ya kawaida katika hili,” amesema akisisitiza kwamba uongozi upo thabiti kuhakikisha mali za kanisa zipo salama akibainisha siku saba ambazo wamepewa na Rita bado hazijakwisha.