Kauli ya Nchimbi kuhusu migogoro yazua mjadala

Dar es Salaam. Kauli ya Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, aliyoitoa katika maziko ya Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, akisema hapendi migogoro ya vyama vya siasa, imeibua mijadala huku wasomi na viongozi wa dini wakimpongeza.

Katika hotuba hiyo aliyoitoa jana Jumamosi, Februari 28, 2026, Dk Nchimbi alikemea ugomvi wa vyama vya siasa na kusisitiza umuhimu wa mshikamano wa kitaifa, akisema hapendi kabisa migogoro ya kisiasa inayosababisha mgawanyiko miongoni mwa Watanzania.

“Nchi hii kila mtu ana nafasi na wajibu wa kuitumikia. Katika utumishi wa nchi yetu tusitegeane. Kila mtu atumikie nchi yake kwa nguvu zake zote. Mimi hata mambo ya kugombana kivyama sipendi kabisa. Ni ujinga tu. Nchi yetu ni moja. Ninyi mnagombana nini?” alisema katika mazishi hayo yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam.

Kauli hiyo imesambaa kwa kasi mitandaoni na kuzua mjadala mpana, huku baadhi wakimpongeza kuwa amesimamia ukweli, na wengine wakihoji muktadha na uhalisia wa kauli hiyo katika mazingira ya kisiasa nchini Tanzania.

Wakati mjadala huo ukishika kasi, Mwananchi limezungumza na wadau kutoka makundi mbalimbali, wakiwemo wasomi, wachambuzi wa siasa, viongozi wa dini, wanasiasa na asasi za kiraia, ambao wameeleza maoni yao kwa mitazamo tofauti.

Mchambuzi wa siasa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Sabatho Nyamsenda, amesema kauli ya Dk Nchimbi ina sura tatu, akifafanua kwa msingi wa hali ya kisiasa nchini na mamlaka aliyonayo kama Makamu wa Rais.

“Kauli ya Dk Nchimbi kuhusu vyama vya siasa ina sura tatu. Kwanza, katika zama ambazo kumekuwa na madai ya ukandamizaji wa vyama vya siasa, kauli yake imekuwa kama tone la maji katika ardhi yenye ukame wa haki za kisiasa na kiraia,” amesema na kuongeza:

“Kwa upande huo, anapaswa kupongezwa kwa kusimama upande wa siasa za maelewano na upatanishi, ambapo nguvu ya hoja na si mabavu ya dola ndiyo huamua mustakabali wa chama cha siasa”

Msomi huyo ameongeza kuwa kwa wanafunzi wa sayansi ya siasa, kauli hiyo ni malighafi katika uchakataji wa mwenendo wa chama kilichopo madarakani.

“Na hapo ndipo tunapata sura ya pili ya kauli hiyo. Tunaweza kuifahamu zaidi sura hiyo iwapo tutajiuliza, je, maoni hayo yanaakisi na kushabihiana na kauli za viongozi wenzake waandamizi katika chama chake na serikali?” amehoji.

“Sitaki kutoa jibu, lakini ingekuwa inashabihiana basi isingezua gumzo kwa sababu asingekuwa amezungumza kitu kipya,” ameeleza msomi huyo.

Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa nchini, Faraji Mangula, amesema hotuba hiyo inaashiria kuwa Dk Nchimbi alielewa matukio yaliyojitokeza kanisani hapo, hivyo akaamua kusimama na ukweli wa nafsi yake.

“Viongozi walioshangiliwa sana ni Majaliwa Kassimu, Waziri Mkuu mstaafu, na Dk Philip Mpango, Makamu wa Rais mstaafu, kwa kufanya kazi kwa weledi, na licha ya kuwa na nafasi ya kugombea tena hawakufanya hivyo,” amesema Mangula.

“Na baadaye yametokea machafuko wakati wa uchaguzi uliofuata. Hotuba hii maana yake hali huko ndani sio shwari na pia viongozi wengine wa kisiasa wanafunguliwa kesi na kuwekwa gerezani kama Tundu Lissu.

“Ameonesha kuwa hafurahii na ameonesha kwa vitendo kuanzia alivyokuwa Katibu Mkuu wa CCM (Chama cha Mapinduzi),” amefafanua mchambuzi huyo.

Kauli za viongozi wa dini

Sheikh Hamis Mataka amesema, kwa aliyoyasema, Makamu wa Rais ametoa nasaha muhimu kwa wanasiasa kwa kuzungumza ukweli kwa wakati sahihi.

“Kwa maoni yangu, Makamu wa Rais ametoa nasaha muhimu na amezungumza ukweli ambao wanasiasa wengi huufumbia macho. Umuhimu wa kukubali uwepo wa mitazamo tofauti katika kujenga nchi, wanasiasa na vyama vyao wapo kwa mujibu wa Katiba na sheria, wajibu wao ni kushirikiana, kujenga hoja madhubuti na kuleta fikra chanya mbadala kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

“Kinyume chake, kugombana, kulumbana bila hoja za msingi na kuchezeana rafu ni utoto na ujinga,” amesema Sheikh Mataka alipozungumza na Mwananchi na kuongeza;

“Viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kuwaelekeza wanasiasa wanapopotoka, kuwaombea na kuwasaidia wanapolemewa, wakaanguka au wakakata tamaa, na si vyema viongozi wa dini kugeuka wanasiasa.”

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza, amesema kauli ya Makamu wa Rais ni ishara kuwa tatizo kubwa liko ndani ya nchi.

“Tuna tatizo kubwa ndani, lakini viongozi wetu wanakimbilia kutatua tatizo Washington, Geneva, The Hague, Brussels, Addis Ababa na New York, lakini tatizo liko ndani,” amesema Askofu Bagonza.

Askofu huyo amesema alichosema Makamu wa Rais kinatoa wito wa kuangalia na kutatua tatizo la ndani, akisema kufanya hivyo kutarahisisha kukabiliana na jumuia ya kimataifa, Taifa likiwa limeungana.

Ameongeza kuwa, mbali na msiba aliotumia Makamu wa Rais kutoa rai hiyo, wengi wana misiba iliyotokana na migogoro ya kisiasa, hivyo kauli yake ilitoa faraja kwa Taifa.

“Ni kiongozi na alikuwa kwenye msiba tena mkubwa. Msiba ni kipimo cha uongozi kuliko sherehe, lazima kiongozi utoe faraja. Watu wana misiba mingi mioyoni, wanatamani kusikia viongozi wao wanasemaje,” amesema Askofu Bagonza.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashehe na Maaskofu ya Amani na Maadili, Askofu William Mwamalanga, amesema kauli ya Dk Nchimbi imebeba ujumbe mzito ndani ya chama chake (CCM) na Serikali.

“Alichokisema Makamu wa Rais kimeonesha kuwa ndani ya chama na Serikali hawako pamoja,” amesema Mwamalanga.

Akirejea kushangiliwa kwa viongozi wastaafu na wito wa Dk Nchimbi kuwa angetamani nao washingiliwe, Mwamalanga amesema hiyo inaashiria kuwa viongozi wa Serikali pia hawapo pamoja na wananchi, hali inayoonesha hitaji la kutafuta mwafaka wa kitaifa.

Wanasiasa na asasi za kiraia

Mkuu wa Idara ya Habari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Gervas Lyenda, amesema kauli hiyo haiwezi kuangaliwa nje ya muktadha wa kisiasa wa sasa, akigusia migogoro ya kisiasa inayoendelea nchini.

“Kuna kete ndugu Nchimbi anajaribu kuisukuma. Sio bahati mbaya kusema aliyoyasema kwenye msiba wa Pengo. CCM ni wale wale. Mambo yao ni yaleyale,” amesema Lyenda na kuongeza kuwa;

“Kama Nchimbi kweli ni muumini wa haki kwa wapinzani na demokrasia, angeanza kwanza kuukataa ule unaoitwa uchaguzi wa Oktoba 29, 2025.”

“Kama Nchimbi ni muumini wa haki na siasa za kistaarabu, atoke hadharani na kuungana na taasisi za haki, UN, EU na wengine wanaotetea haki.”

Amehoji kuwa: “ikiwa Nchimbi anapenda haki kwa vyama vya upinzani, alikuwa wapi wakati Serikali ya chama chake ilipoweka mapandikizi waliofungua kesi ya kutaka Chadema isifanye siasa kwa kuwafungia shughuli za siasa kwa miezi sita?”

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Fulgence Massawe, amesema kauli ya Makamu wa Rais ni ya kujinyenyekeza na kuwakumbusha viongozi wengine kurudi kwenye misingi ya kutumikia wananchi kwa ajili ya amani ya nchi.

Wakati baadhi wakiona ni wito wa maridhiano ya kitaifa, wengine wanaitazama kama kauli inayopaswa kupimwa kwa matendo katika uhalisia wa siasa za Tanzania, wakihofia kuwa inaweza kuwa kauli ya kisiasa pekee.