Dar es Salaam. Mashambulizi mapya ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yanahofiwa kusababisha athari kwa Tanzania, kutokana na ukanda wa Mashariki ya Kati kuwa na mchango katika mnyororo wa usambazaji wa mafuta katika soko la dunia.
Hivyo, kuathirika kwa eneo hilo kutasababisha kupaa kwa bei ya mafuta, kutakakotokana na kupungua kwa usambazaji wake katika soko la dunia, ikizingatiwa kuwa mashambulizi yanahusisha mataifa mengine ya jirani.
Jana, Februari 28, 2026, Marekani na Israel zilianzisha mashambulizi yao kwa Iran, yaliyosababisha vifo vya kiongozi mkuu wa taifa hilo, Ayatollah Ali Khamenei, pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Iran.
Kufuatia mauaji hayo, Iran imeapa kulipiza kisasi huku ikiyashambulia mataifa ya Kiarabu ya Ghuba ambako kuna mali za Marekani, jambo ambalo limeifanya vita hiyo kuwa ya ukanda mzima wa Mashariki ya Kati.
Anga lote la Mashariki ya Kati limefungwa, mashirika makubwa ya ndege yamesitisha kufanya safari zao katika ukanda huo, meli za mafuta hazitoki kila kitu kimesimama kufuatia mashambulizi hayo yaliyoingia siku ya pili leo Jumapili.
Makombora ya Marekani na Israel yaliyopigwa Iran yamesababisha vifo vya mamia ya wananchi, wakiwamo watoto.
Moja ya maeneo yaliyoshambuliwa ni shule ya msingi ya wasichana mjini Minab, katika mkoa wa Hormozgan, kusini mwa Iran, ambapo takribani watu 148 wamepoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa.
Wakati huohuo, zaidi ya wakazi 200 wamehamishwa kutoka kwenye makazi yao na kupelekwa katika hoteli tatu mjini Tel Aviv, Israel, baada ya takribani majengo 40 kuharibiwa katika mashambulizi ya Iran jana Jumamosi.
Mbali na athari zilizojitokeza katika ukanda wa Mashariki ya Kati, athari za mzozo huo pia zinatarajiwa kushuhudiwa katika bara la Afrika, hususan Tanzania, ambapo wachambuzi wa diplomasia na uchumi wanaangazia athari hizo zitakazochochewa na kupaa kwa bei ya mafuta.
Usafirishaji wa mafuta kukwama
Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Salim Ahmed Salim, Innocent Shoo amesema mzozo unaoendelea kati ya Marekani, Israel na Iran umeibua wasiwasi mkubwa kimataifa, ukifungua ukurasa mpya wa taharuki katika siasa za kimataifa.
Mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa na Marekani na Israel dhidi ya malengo ya Iran yameongeza hatari ya vita pana zaidi katika eneo la Mashariki ya Kati eneo ambalo si tu kitovu cha siasa za nguvu za dunia, bali pia moyo wa usambazaji wa nishati duniani.
Kuhusu athari za mzozo huo kwa Afrika, Shoo amesema njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani, Hormuz, iko karibu na Iran. Hivyo, endapo kutakuwa na usumbufu wa usafirishaji wa mafuta katika eneo hilo, amesema bei ya mafuta duniani itapanda kwa kasi.
Kwa Tanzania, taifa linaloagiza sehemu kubwa ya mafuta yake kutoka nje, amesema kupanda kwa bei za mafuta kutamaanisha kuongezeka kwa gharama za usafiri, kupanda kwa bei za bidhaa na huduma, shinikizo la mfumuko wa bei, na kupungua kwa uwezo wa wananchi kumudu maisha.
“Kwa maneno mengine, hata kama risasi hazisikiki Dar es Salaam, athari zake zinaweza kuonekana kwenye bei ya petroli, na hatimaye kwenye bei ya chakula sokoni,” amesema mwanazuoni huyo.
Amesema migogoro ya kimataifa mara nyingi husababisha wawekezaji kuwa waoga, mitaji huhama kutoka masoko yanayoibukia kwenda kwenye mali zinazochukuliwa kuwa salama.
Ameongeza kuwa Afrika, ikiwa ni pamoja na Tanzania, inaweza kushuhudia kupungua kwa mtiririko wa uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni (FDI) au kucheleweshwa kwa miradi mikubwa ya maendeleo.
Aidha, usumbufu katika usafirishaji wa kimataifa unaweza kuongeza gharama za mizigo, kuathiri biashara ya kimataifa, na kuathiri mapato ya bandari na sekta ya usafirishaji.
“Kuna haja ya kuimarisha usalama wa nishati, kuongeza uwekezaji katika nishati mbadala na vyanzo vya ndani ili kupunguza utegemezi wa mafuta ya nje na kulinda uchumi wa ndani, na kuweka mikakati ya kudhibiti mfumuko wa bei na kulinda kaya zenye kipato cha chini,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wauzaji wa Mafuta Tanzania (Taomac), Raphael Mgaya, amesema mnyororo wa usambazaji wa nchi umeunganishwa kwa karibu na wazalishaji wa mafuta wa Ghuba.
“Takribani asilimia 100 ya bidhaa zetu za petroli zinatoka katika ukanda wa Mashariki ya Kati,” Mgaya ameliambia Mwananchi.
“Mgogoro wa muda mrefu utaathiri kwa kiasi kikubwa bei za mafuta kwenye pampu za ndani.”
Hata hivyo, amebainisha kuwa Watanzania hawapaswi kutarajia kupanda kwa bei mara moja.
“Mzigo wa Machi na Aprili tayari ulinunuliwa kwa makubaliano ya bei ya awali, hivyo, athari ya haraka ni ndogo,” amesema.
“Lakini kuanzia Mei na Juni 2026, tunatarajia marekebisho ya kupanda kwa bei iwapo misukosuko itaendelea.”
Amesisitiza kuwa mafuta ni bidhaa inayouzwa kimataifa. “Bei za dunia zinapopanda, zinaathiri kila mtu. Hata ukinunua kutoka soko lingine, kama Marekani, bei rejea bado huakisi hali halisi ya soko la dunia.”
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Kariakoo, Severine Mushi, amesema athari tayari zinaanza kuonekana miongoni mwa wafanyabiashara wadogo na wa kati.
“Kwa sasa, tuna wafanyabiashara waliokwenda Dubai kwa ajili ya manunuzi na wamekwama. Hatujui watarudi lini wala vipi,” amesema.
Ameonya kuwa eneo la Ghuba ni miongoni mwa washirika wakuu wa biashara wa Tanzania kwa bidhaa za rejareja.
“Ukanda tunaofanya nao biashara kwa kiasi kikubwa ndiyo huohuo unaoingia kwenye mgogoro sasa. Athari zitakuwa kubwa.”
Ameongeza kuwa hata biashara na China inaathirika kwa njia isiyo ya moja kwa moja, kwa sababu minyororo mingi ya usambazaji hupitia njia za usafiri za Mashariki ya Kati.
“Tunatarajia ucheleweshaji wa mizigo na kupanda kwa gharama za usafirishaji,” amesema.
Mabadiliko ya njia za meli, kuongezeka kwa bima ya usafiri wa baharini, na muda mrefu wa safari vinaweza kuongeza gharama za kuingiza bidhaa kama nguo, vifaa vya kielektroniki, vipuri, na bidhaa za matumizi ya nyumbani.
Mchambuzi huru wa masuala ya fedha, Oscar Mkude, amesema kwa watu wenye kipato chenye ukomo, wakiwamo wafanyakazi wenye mishahara na wastaafu, kupanda kwa bei ya mafuta na bidhaa kunamaanisha kupungua kwa uwezo wa kununua.
“Mafuta yanapopanda, gharama za usafiri huongezeka. Hilo linaathiri usambazaji wa chakula, uzalishaji viwandani, na bei za rejareja,” ameeleza Mkude.
“Wenye kipato chenye ukomo, hasa wafanyakazi na wastaafu, huhisi shinikizo mapema kwa sababu mapato yao hayapandi moja kwa moja kulingana na mabadiliko ya bei.”
Zaidi ya athari za haraka za soko, Mkude ameonya kuwa ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na nchi za Mashariki ya Kati unaweza pia kuathirika kwa njia isiyo ya moja kwa moja.
“Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imeimarisha ushirikiano wa kiuchumi na baadhi ya nchi za Ghuba,” amesema.
“Iwapo ukanda huo utaingia katika mgogoro wa muda mrefu, nchi hizo zinaweza kubadili vipaumbele vyao vya ndani. Hilo linaweza kuchelewesha au kupunguza kasi ya mikataba ya kiuchumi na mtiririko wa uwekezaji wa pande mbili.”
Mkude pia ameonya kuwa athari za kiuchumi zinaweza kuwa kubwa zaidi zikichanganyika na mishtuko mingine ya kimataifa.
“Iwapo mzozo huu utaambatana na misukosuko mingine kama vile kurejea kwa vitisho vya kiafya duniani, kama tahadhari tunazoziona kuhusu kuongezeka kwa maambukizi ya Covid-19 athari ya pamoja inaweza kuwa kubwa zaidi,” amesema.
Mishtuko mingi kwa wakati mmoja huongeza shinikizo kwa sarafu, hupunguza ukwasi, na kudhoofisha imani ya wawekezaji katika masoko yanayoibukia na yale ya mipakani.
Wachambuzi wamesema mgogoro huo unaoendelea umeonesha udhaifu wa kimuundo katika mfumo wa uchumi wa Tanzania hasa utegemezi mkubwa wa mafuta yanayoagizwa kutoka nje.
“Ni lazima tubadilishe muundo wa uchumi wetu,” amesema Mkude, na kuongeza: “Na tunahitaji kuwekeza kwa dhati katika vyanzo mbadala vya nishati kama umeme na gesi asilia ili kupunguza utegemezi wa mafuta ya kuagiza na kupunguza gharama za muda mrefu.”
Tanzania ina akiba kubwa ya gesi asilia na imeongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme katika miaka ya karibuni. Kuharakisha matumizi ya vyanzo vya ndani vya nishati kunaweza kusaidia kupunguza athari za mishtuko ya nje siku zijazo.
Mafuta ndiyo kipimo kikuu cha mvutano wa Mashariki ya Kati, ambapo nchi hizo zinategemea uchumi wa mafuta huku zikitegewa katika kusambaza mafuta katika mataifa mengi duniani, hasa Afrika.
Iran ni mzalishaji mkubwa wa mafuta na ipo mkabala na Rasi ya Uarabuni yenye utajiri wa mafuta, ikitenganishwa na mlango wa bahari wa Hormuz, ambako takribani asilimia 20 ya usambazaji wa mafuta duniani hupita.
Mzozo huo unaweza kupunguza kiwango cha mafuta yanayoingia katika soko la dunia na kusababisha bei kupanda.
Kwa mujibu wa Reuters, Ijumaa iliyopita mafuta ghafi yalikuwa yanauzwa kwa takribani Dola za Marekani 73 (Sh185,484) kwa pipa, yakiwa tayari yamepanda kwa takribani asilimia 20 tangu mwanzoni mwa mwaka huu.
Baadhi ya kampuni kubwa za mafuta na wafanyabiashara wakubwa walisitisha usafirishaji wa mafuta ghafi na bidhaa za mafuta kupitia mlango wa bahari wa Hormuz kutokana na mashambulizi hayo, vyanzo vinne vya biashara vilisema Jumamosi.
William Jackson, mchumi mkuu wa masoko yanayoibukia katika kampuni ya Capital Economics, amesema hata kama mzozo huo utadhibitiwa, bei ya Brent inaweza kupanda hadi takribani dola 80 (Sh203,270) kwa pipa, kiwango kilichofikiwa wakati wa vita vya siku 12 nchini Iran Juni, mwaka jana.
Mashambulizi hayo yaliyoanzishwa na Marekani na Israel huenda yakachukua muda zaidi, kutokana na viongozi wa mataifa hayo kueleza kwamba wataendelesha mashambulizi huku Iran ikiahidi kulipa kisasi kufuatia vifo vya viongozi wake.
Rais wa Marekani, Donald Trump, ameashiria katika chapisho lake la Truth Social kuwa “mabomu mazito na ya kulenga shabaha maalumu” dhidi ya Iran yataendelea “bila kukoma wiki nzima au kwa muda wowote utakaohitajika.”
Wakati huohuo, Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema kulipiza kisasi kufuatia kuuawa kwa Kiongozi Mkuu, Ayatollah Ali Khamenei, na viongozi wengine waandamizi wa Iran, ni wajibu na haki halali kwa nchi hiyo.
“Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaona kuwa kutafuta haki na kulipiza kisasi kutoka kwa watenda makosa na wale walioagiza kosa hili la kihistoria ni wajibu wake na haki halali, na itatumia nguvu zake zote kutimiza jukumu hili kubwa na wajibu huu,” amesema Rais huyo wakati akitoa salamu za rambirambi kufuatia vifo vya viongozi hao.