BODI ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) haitaki kuchelewesha mambo. Imetoa ratiba mpya ya kuziba viporo vyote vilivyokuwepo hasa vikihusu Yanga, Simba, Azam FC na Singida Black Stars zilizokuwa zikishiriki michuano ya CAF msimu huu.
Kuanzia jana Machi 1 tuliposhuhudia Dabi ya Kariakoo ya Simba na Yanga, sasa kutakuwa na mechi mfululizo zinazohusisha timu hizo. Unaweza kusema ‘honeymoon’ yao sambamba na Azam na Singida BS zilizokuwa zikishiriki michuano ya CAF, imeisha ndani ya Ligi Kuu kwani timu hizo zimekuwa na viporo vingi.
Kwa mujibu wa ratiba mpya ya Ligi Kuu iliyotolewa na Bodi ya Ligi iliyoboreshwa kwa kuziba viporo, sambamba na ile ya hatua ya 32 bora ya Kombe la Shirikisho (FA) ndani ya Machi pekee, kuna msako wa maana unaozihusu Yanga na Simba, bila kusahau Singida BS na Azam ili kumalizia duru la kwanza.
Ligi hiyo kwa msimu wa 2025-2026, inatarajiwa kufikia tamati Juni 18, 2026.
Kabla ya mechi ya jana katika Dabi ya Kariakoo, Yanga na Simba zilikuwa zimepishana pointi tano. Yanga ikiwa kileleni na pointi 28, Simba ilikuwa na 23 kila moja ikicheza mechi 10. Mwezi huu ndio zinakwenda kukamilisha duru la kwanza.
Msimu uliopita katika duru la kwanza, timu hizo zilimaliza nafasi mbili za juu zikipishana pointi moja, Simba ikiongoza na 40 baada ya kushinda mechi 13, sare moja na kupoteza moja, huku Yanga ikimaliza na 39 kufuatia kushinda mechi 13 na kupoteza mbili, haikuwa na sare.
Msimu huu katika mechi 10 za kwanza, Yanga imekusanya pointi 28, ikishinda tisa na sare moja, haijapoteza ikizifunga Pamba Jiji (3-0), Mtibwa (2-0), KMC (4-1), Fountain Gate (2-0), Coastal (1-0), Mashujaa (6-0), Dodoma Jiji (3-1), Namungo (1-0) na JKT Tanzania (5-0). Pia imetoka 0-0 dhidi ya Mbeya City.
Katika msako wa kuzifikia pointi za msimu uliopita ambao Yanga ilikuwa bingwa, ina mechi sita itakazocheza mwezi Machi pekee kumaliza duru la kwanza na kuanza duru la pili, kati ya hizo, Dabi mbili dhidi ya Simba ikiwa mwenyeji na Azam ikiwa mgeni. Pia itacheza dhidi ya Singida Black Stars.
Mechi hizo sita za Ligi Kuu Bara zipo namna hii; Yanga vs Simba (Machi 1), Singida Black Stars vs Yanga (Machi 5), Tanzania Prisons vs Yanga (Machi 12), Azam vs Yanga (Machi 15, TRA vs Yanga (Machi 18) na Mtibwa vs Yanga (Machi 21). Pia itacheza dhidi ya Polisi Tanzania, Machi 8 katika hatua ya 32 Bora ya Kombe la FA.
Yanga ikishinda mechi zote hizo za ligi, itamaliza duru la kwanza na kuanza la pili ikifikisha pointi 46 na kuvunja rekodi ya msimu uliopita.
Mtihani zaidi unakuja katika mechi za ugenini ambapo kati ya hizo, nne itacheza nje ya Dar es Salaam, ukiachana na ile ya jana iliyopigwa Zanzibar.
Yanga itaifuata Singida Black Stars, Tanzania Prisons, TRA United na Mtibwa Sugar. Dar itacheza dhidi ya Azam ikiwa mgeni.
Jana Simba ilikuwa na mtihani wa kufuta uteja mbele ya Yanga baada ya kupoteza mechi sita mfululizo za Dabi ya Karikoo. Baada ya dabi ya jana, Wekundu wa Msimbazi watakuwa na mechi tano, nne za Ligi Kuu Bara na moja Kombe la FA.
Machi 1 ambayo ni jana, Simba ilikuwa mgeni wa Yanga, baada ya hapo Machi 7 itaikaribisha B19 katika hatua ya 32 Bora ya Kombe la FA. Itaendelea na msako katika ligi Machi 11 kwa kucheza ugenini dhidi ya Singida Black Stars.
Machi 14, Simba itaifuata TRA United, itaenda Mwanza kucheza dhidi ya Pamba Jiji (Machi 19) na Machi 22 itamalizana na TRA United nyumbani. Baada ya hapo, ni mapumziko kupisha kalenda ya FIFA.
Msimu uliopita katika duru la kwanza Simba ikiwa inafundishwa na Fadlu Davids, ilimaliza na pointi 40 kileleni, ikishinda mechi 13, sare moja na kupoteza moja. Msimu huu mechi 10 za kwanza kabla ya jana, imekusanya pointi 23, imeshinda saba, sare mbili na kupoteza moja.
Simba katika mechi saba ilizoshinda msimu huu imezifunga Fountain Gate (3-0), Namungo (3-0), JKT Tanzania (2-1), Mbeya City (3-0), Mashujaa (2-0), KMC (2-0) na Tanzania Prisons (2-0). Ikafungwa 2-0 na Azam, huku sare ikiwa ni dhidi ya Mtibw Sugar (1-1) na Dodoma Jiji (0-0).
Mechi tano za Ligi kwa Simba mwezi Machi, ugenini ni nne dhidi ya Yanga, Singida Black Stars, TRA United na Pamba Jiji. Nyumbani moja pekee dhidi ya TRA United ambayo hii itacheza nayo mara mbili mwezi Machi.
Machi 1: Yanga vs Simba (Ligi Kuu)
Machi 5: Singida BS vs Yanga (Ligi Kuu)
Machi 8: Yanga vs Polisi TZ (FA)
Machi 12: Prisons vs Yanga (Ligi Kuu)
Machi 15: Azam vs Yanga (Ligi Kuu)
Machi 18: TRA United vs Yanga (Ligi Kuu)
Machi 21: Mtibwa vs Yanga (Ligi Kuu)
Machi 1: Yanga vs Simba (Ligi Kuu)
Machi 7: Simba vs B19 (FA)
Machi 11: Singida vs Simba (Ligi Kuu)
Machi 14: TRA United vs Simba (Ligi Kuu)
Machi 19: Pamba Jiji vs Simba (Ligi Kuu)
Machi 22: Simba vs TRA United (Ligi Kuu)
DURU LA KWANZA SIMBA MSIMU ULIOPITA
DURU LA KWANZA YANGA MSIMU ULIOPITA