Asia Masimba anayewaongoza wanawake 400 wachimbaji madini

Geita. Ujasiri na uthubutu wa Asia Masimba ni simulizi ya kuvunja miiko iliyodumu kwa miongo kadhaa katika sekta ya madini mkoani Geita.

Katika mazingira ambayo wanawake walionekana kuwa mkosi machimboni, Asia alithubutu kuingia duarani, akakubali kutukanwa, kufukuzwa na hata kucharazwa viboko, lakini hakurudi nyuma.

Kwa miaka mitano mfululizo alipambana na imani potofu zilizotamalaki katika jamii ya wachimbaji wanaume. Wakati wengine walimwambia mwanamke hawezi kufanikiwa kwenye uchimbaji wa dhahabu, alisimama imara akisisitiza kuwa mafanikio au mikosi hayana jinsia.

“Oooh! wanawake wana mikosi, nikawaambia hapana. Kama utasema wana mikosi, mkosi unaanzia chumbani kwako unakuja sebuleni kwako kwa mabinti zako unakwenda nje. Nilipambana na jambo hilo, nashukuru Mwenyezi Mungu na Serikali walinisaidia yameisha,” anasema Asia katika mahojiano na Mwananchi.

Asia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wachimbaji Mkoa wa Geita (Gewoma). Anasimulia kuwa alipoanza kujishughulisha na uchimbaji mwaka 2009, wanawake hawakuruhusiwa kuingia katika maeneo ya machimbo. Waliaminika kuleta bahati mbaya katika uzalishaji wa dhahabu.

Licha ya kutambua kuwa ilikuwa mwiko kwa mwanamke kuwa mchimbaji, Asia aliamua kuziishi ndoto zake za tangu utotoni za kuwa mfanyabiashara katika sekta ya madini. Ndoto ambayo alihisi hataitimiza baada ya kushindwa kuendelea na masomo ya sekondari.

Kitaaluma alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Mtakuja iliyopo Manispaa ya Geita. Baadaye alichaguliwa kuendelea na masomo katika Shule ya Sekondari Geita lakini hakuendelea baada ya kusitisha masomo kutokana na changamoto kadhaa, ikiwamo uwezo mdogo darasani.


“Uelewa wangu ulikuwa si mzuri kwa sababu Kiingereza kilikuwa hakipandi. Baada ya kufika form four (kidato cha nne) nikaona niishie hapo niende kutafuta maisha mengine,” anasema.

Anaeleza alianza safari ya kutimiza ndoto zake kwa kujishughulisha na biashara ya kuuza vitumbua, chapati, ndizi na baadaye aliolewa na ukawa mwanzo wa kutimiza ndoto zake kwa kuwa wakati huo mume wake alikuwa akichimba dhahabu.

Anasema alianza kufanya shughuli za madini mwaka 2009, akapata leseni ya uchimbaji madini.

Wakati anaanza shughuli za uchimbaji alikuwa na mtaji wa Sh2 milioni alizotumia kununua magogo (matimba) yenye thamani ya Sh700,000. Yanatumika katika uchimbaji kwenye maduara, wakati huo yakiuzwa kati ya Sh2,000 na Sh3,000.

Kutokana na mtaji aliokuwa nao hakuweza kuwaajiri moja kwa moja vijana waliokuwa wakishuka duarani kuchimba, lakini alitumia mfumo wa kugawana kile kilichopatikana, huku akigharimia chakula na ununuzi wa magogo.

Leo, moja ya mafanikio anayojivunia ni kuelimisha na kuwaunganisha wanawake kupitia Gewoma, chama chenye wanachama zaidi ya 400. Anasema awali wanawake wengi hawakuwa na uelewa kuhusu sekta ya madini, lakini sasa baadhi yao wamejenga nyumba na kuboresha maisha yao kupitia uchimbaji.

Asia anajivunia utayari na usaidizi alioupata kutoka kwa mume wake, akibainisha kuwa ndiye aliyemhamasisha na kumruhusu kuwekeza katika madini.

Kwa miaka 10 ya mwanzo, Asia alijikita katika kutoa elimu ya madini kwa wanawake, akishirikiana na taasisi mbalimbali zikiwamo Chama cha Wachimbaji Wanawake Tanzania (Tawoma), Shirikisho la Wachimbaji Wadogo Tanzania (Femata), Gerema pamoja na maofisa madini wa Serikali.

“Wapo wasichana ambao wameshawishika kujiunga na sisi. Tunawataka waendelee kujiunga na Gewoma kwa sababu sisi tunakua ili elimu tuliyonayo tuwaachie wao,” anasema.

Kupitia Gewoma, anasema wanalishukuru Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kuwajengea uzio katika eneo la shamba lao la miti, pia shirika la GGF kwa kuwasaidia kupanda miti kwenye shule mbalimbali ili kudumisha uhifadhi wa mazingira.

Anasema kwa sasa wanamiliki zaidi ya leseni 20 za uchimbaji madini katika maeneo mbalimbali. Vilevile, wanatambua mchango wa Serikali kwa kuwapatia leseni hizo.

“Leseni tatu tulipewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan. Alitukabidhi tunashukuru,” anasema.

Anasema katika kila mwanzo wa jambo hayakosekani maneno na kejeli lakini alijisimamia dhidi ya maneno ya majirani ambao awali walimuona kama vile mzururaji asiye na kazi maalumu, kutokana na muda wake mwingi kuutumia katika usimamizi wa shughuli zake, lakini sasa nao wameshawishika kuingia katika uchimbaji madini.

Anaeleza baadhi yao sasa wana hali nzuri kiuchumi kuliko hata yeye kutokana na kushikwa mkono kifedha na vifaa vya kisasa tofauti na yeye aliyesimama imara mwenyewe na mume wake.

“Muda mwingi nilikuwa barabarani, kwenye machimbo huwezi kumwachia mtu moja kwa moja atakuibia, inabidi kuwa macho,” anasema.

Anaeleza moja ya uamuzi mgumu aliowahi kuchukua ni kuachana na leseni yake binafsi ya uchimbaji na kuungana na wanawake wengine kupitia Gewoma, kwa lengo la kukuza ushirikiano na kuwainua wengine ambao walikuwa wameanza uchimbaji.


Hata hivyo, changamoto bado zipo. Anawaalika wawekezaji na wahisani kuwekeza katika Gewoma ili kuleta mabadiliko chanya kwa kuwa wanatumia zana za kizamani ambazo zimepitwa na wakati.

Vilevile, anasema wana uhitaji wa mitaji mikubwa ili watimize ndoto zao kwa kuwa uchimbaji wa sasa unatumia gharama kubwa tofauti na awali.

“Ukimkomboa mwanamke umekomboa jamii nzima, wanawake si wengi wanaoingia duarani zaidi ni wanaume na hasa vijana wanaotuchimbia,” amesema.

Kwa mujibu wa Asia, wanachama wengi wa Gewoma ni wajane hali inayoathiri utendaji thabiti kulingana na mzigo mkubwa walionao katika utunzaji wa familia, hivyo kushindwa kulipa baadhi ya michango ya chama hicho.

“Ukiangalia wengi wao ni wajane na unakuja kukuta mtu ameachwa na watoto watatu, wanne, watano, mwingine mmoja sasa kwenda kumlazimisha atoe mchango wewe mwenyewe unamuonea huruma kwa sababu sisi tunafahamiana,” anasema.

Anaeleza anatamani kuona wanawake mkoani Geita wanakuwa matajiri wanamiliki magari, wana nyumba nzuri na wanapata mlo mzuri pamoja na familia zao.

Kwa mtazamo wake, Siku ya Wanawake Duniani ni daraja la ukombozi wa mwanamke kutoka zama za ujima kuelekea ustaarabu na maendeleo. Anasema wanawake wengi sasa wanamiliki mali na fedha, lakini anasisitiza heshima na maadili visiachwe nyuma.

Mbali na uchimbaji, amekuwa akitoa elimu ya madini kwa vijana katika vijiwe vya bodaboda, kikiwamo cha Ambassador ambacho yeye ni mjumbe, akiwahamasisha kuona fursa zilizopo katika sekta hiyo.