Utitiri wa bandari kavu Dar unavyochochea kero ya foleni

Dar es Salaam. Fikiria unatoka katikati ya jiji la Dar es Salaam, labda umetoka kazini au una shughuli zako binafsi, umechoka na unahitaji kufika nyumbani Mbagala. Unapita Barabara ya Kilwa ukiwa na matumaini kwamba leo mambo yatakuwa nafuu, lakini safari inaanza kwa majaribu.

Unapofika eneo la Uhasibu kuelekea Mtoni kwa Aziz Ally, magari yamesimama kama msafara usio na mwisho. Hapa hakuna mwendo, kuna kusogea. Dakika zinakatika, injini zinawaka, viyoyozi vinapiga kazi kupambana na joto la pwani. Abiria wanatazama saa, madereva wanavuta pumzi ndefu, bodaboda wanapenya kwa tahadhari katikati ya magari.

Foleni imeanza kama mzaha, lakini haraka inageuka kuwa adhabu.

Unaposhuka kilima cha Mtoni Mtongani, pale kwenye daraja linalokatiza reli, moyo unapata nafuu kidogo. Gari linaachia, upepo wa bahari unapiga dirishani, unahisi kama umevuka mtihani, lakini nafuu hiyo ni ya muda mfupi. Unapopandisha Misheni, mwendo unarudi kuwa wa kusuasua, si kusimama kabisa, bali ni mwendo wa kuvuta pumzi na kuiachia.

Halafu unafika Mbagala Kipati. Hapo ndipo unagundua kuwa safari haijaanza kweli. Foleni inaanza kujibana, magari yanapishana kwa tabu, malori makubwa yanachukua nafasi yao kana kwamba hayana haraka, huku daladala zikisimama na kuondoka kila baada ya hatua chache. Kadri unavyosogea kuelekea Mbagala Zakhem, hali inazidi kuwa nzito. Dakika 35 hadi saa moja kupita kipande kifupi tu cha barabara si jambo la kushangaza tena, ni kawaida.

Unapokaribia Mbagala Rangi Tatu, tayari umechoka kisaikolojia. Hii si foleni ya asubuhi pekee, wala si ya jioni pekee. Ni foleni ya kudumu, ipo kama kivuli cha barabara. Asubuhi, mchana, jioni hadi usiku, inapungua, lakini haimaliziki.

Cha kushangaza zaidi, katikati ya mateso hayo, kila uchao unaona mabango mapya ya Bandari Kavu (ICD) yakichipuka. Maeneo yaliyokuwa mbali kidogo na barabara sasa yamehamia karibu kabisa na njia kuu. Malori ya makontena yanaingia na kutoka, yakiongeza uzito kwenye barabara ambayo tayari inalemewa.

Mtumiaji wa kawaida wa barabara hiimfanyakazi, mama wa nyumbani, mwanafunzi, dereva wa daladala anabaki kuwa mwathirika wa hali isiyobadilika.

Katika mazingira hayo, safari ya kutoka mjini kwenda Mbagala si tena umbali wa kilomita pekee, ni safari ya subira, ya kuvumilia, na ya kuhesabu dakika kama siyo saa.

Hili ni moja ya maeneo ambayo wakazi wa Dar es Salaam wanakumbana na kero ya foleni ambayo, pamoja na mambo mengine, inachochewa na uwepo wa ICD.

Ukuaji wa shughuli za ICD katika Jiji la Dar es Salaam umeibua malalamiko kutoka kwa wakazi wa maeneo ya pembezoni mwa barabara kuu na mitaa ya makazi, wakidai uwekezaji huo unafanyika bila kuzingatia kikamilifu mipango miji, athari za mazingira na ushirikishwaji wa wananchi.

Bandari kavu ni vituo vya kupokea na kusafirisha makasha (makontena) nje ya bandari kuu, vikilenga kupunguza msongamano bandarini na kurahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka na kwenda mikoani au nchi jirani.

Hata hivyo, baadhi ya wakazi wamesema ongezeko la vituo hivyo katikati ya makazi limegeuka kero, licha ya Serikali kuhimiza upanuzi wa miundombinu ya usafirishaji ili kuharakisha biashara.

Akizungumza Februari 19, 2026, wakati wa kikao cha pamoja na wamiliki wa ICD, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, amewataka wafanye kazi saa 24 ili kuendana na kasi ya utoaji wa huduma za forodha.

Amesema anatambua umuhimu wa ICD na mchango wao katika makusanyo ya kodi, kwa kuwa wamekuwa wakiwezesha na kurahisisha biashara ndani na nje ya nchi.

Bandari Kavu ya makasha matupu iliyopo barabara ya Mandela eneo la Veternary, Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam



Wakati Mwenda akieleza hayo, Manka Mushi, mkazi wa Sandali wilayani Temeke, Dar es Salaam, amesema kuibuka kwa shughuli za bandari kavu katika eneo lao kumewaingiza hofu wazazi wengi, hasa kutokana na ongezeko la magari makubwa yanayopita muda wote karibu na shule.

Amesema ndani ya muda mfupi, mazingira ya mtaa huo yamebadilika ghafla na kuwa na pilika nyingi za malori, hali inayotishia usalama wa watoto wanaokwenda na kutoka shule.

“Kwa muda mfupi tumepata mabadiliko ambayo hatukuyatarajia. Hapa tuna shule mbili, ya msingi na sekondari. Tumeingiwa na woga, watoto wanapoondoka kwenda shule au kurudi nyumbani inabidi kuwasindikiza kwa kuhofia usalama wao,” amesema Manka.

Kwa upande wake, Riziki Sharif, mkazi wa Chang’ombe, amesema msongamano wa malori uliokuwa ukiingia na kutoka katika bandari kavu uliwalazimu kuuza nyumba yao na kuhamia eneo jingine.

“Tulikuwa na nyumba jirani na uwanja wa Taifa, lakini kero ya malori ilikuwa kubwa, eneo letu lilikuwa linajaa magari kila wakati, tukalazimika kuondoka kwa ajili ya usalama na utulivu wa familia,” amesema Riziki.

Akizungumza na Mwananchi Februari 27, 2026, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tamstoa), Chuki Shaban, amezilaumu baadhi ya halmashauri kwa kutoa leseni za kuanzisha ICD katikati ya makazi ya watu, akisema hatua hiyo ndiyo chanzo cha msongamano, uharibifu wa miundombinu na migogoro na wananchi.

Chuki amesema ni makosa kuruhusu shughuli nzito za makontena kufanyika kwenye maeneo yasiyo na miundombinu stahiki. “Halmashauri zinatoa leseni za ICD kwenye makazi bila kuzingatia athari zake, leo malori makubwa yanaingia mitaani na kusababisha foleni ya saa tatu hadi tano, kuwa chanzo cha watu kuchelewa kazini na watoto shuleni,” amesema.

Amehoji uhalali wa kutoa vibali kwenye maeneo ambayo hayana hata barabara imara, mitaro wala nafasi ya kuegesha malori.

“Unapewa leseni sehemu ambayo lori haliwezi kuingia, hii ni akili kweli?” amehoji.

Amesema ukosefu wa ubunifu kwa baadhi ya viongozi umechangia tatizo hilo, akipendekeza leseni zote zipitiwe upya na ICD zihamishiwe nje ya miji iliko miundombinu bora.

“Sisi si adui wa maendeleo, tunahitaji tu maeneo sahihi ya kufanya kazi bila kuathiri wananchi,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Sandali, Habibu Ndege, amesema walishangaa kuona ukuta ukibomolewa na makontena kuingizwa, huku malori yakianza kuegeshwa na kufunga njia za kupita.

“Sijui imekuwaje, lakini ghafla tumeona makontena yanaingia na malori yanaegeshwa barabarani. Hapakuwa na tangazo wala kikao cha wananchi,” amesema.

Ndege amesema ofisi ya Serikali ya mtaa haikushirikishwa katika mabadiliko yoyote ya matumizi ya ardhi, hali inayoweka uongozi wa mtaa katika wakati mgumu wanapoulizwa na wananchi kuhusu uhalali wa mradi huo.

Kwa mujibu wa sheria za mipango miji, mabadiliko ya matumizi ya ardhi yanapaswa kutangazwa na wananchi kupewa fursa ya kutoa maoni, lakini kwa wao hawajaona matangazo.

Amesema wakazi wanasema bandari hiyo imesababisha uharibifu wa barabara, vumbi na msongamano wa malori, jambo linalowaathiri wanaotumia njia kuelekea Mchicha na Viwandani.

Hata hivyo, amesema wiki moja iliyopita walifanya kikao ili kutoa malalamiko kuhusu bandari hiyo, wakaelezwa majibu kamili wangeyapata Ijumaa ya Februari 27, 2026.

Banadari kavu iliyopo jirani na makazi ya watu eneo la Sandali, Wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam



Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema bandari kavu zimekuwa nyingi kwa sababu watu wanatafuta maeneo ya kuhifadhi mizigo yao.

Amesema kwa hatua ya kwanza, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, hivi karibuni atafanya ziara kupitia maeneo yote yenye bandari kavu.

“Bandari kavu zinasajiliwa kwa mujibu wa sheria, na bandari kavu itakayobainika kuwekwa kinyume cha sheria, hatua za kisheria zitachukuliwa.

“Leo Februari 26, 2026, nimezungumza naye (Chalamila), amenieleza hatua ambazo mkoa umezichukua ili kukabiliana na msongamano mkubwa wa magari barabarani, ambao kwa sehemu umechangiwa na bandari kavu zilizowekwa maeneo mbalimbali na magari yakienda kuchukua mizigo yanasababisha usumbufu mkubwa,” amesema.

Msigwa amesema mradi wa bandari unaotekelezwa Kurasini Logistic Park utapunguza uwepo wa bandari kavu katika maeneo mbalimbali kwa sababu wataongeza ukubwa wa eneo la bandari la kuhifadhi mizigo yao.

“Tukitekeleza mradi huu, tutaongeza ukubwa wa eneo la kuhifadhi mizigo la kufikia mita za mraba 210,000, itakayowezesha kuhifadhi makontena 700,000. Maana yake, tutaongeza uwezo mkubwa na bandari kavu zitapungua, na watu wengi wataweka mizigo yao eneo la bandari,” amesema.

Akizungumzia mradi wa Bandari ya Kwala, Msigwa amesema haujakwama bali unaendelea kutoa huduma, ila kinachofanyika ni kuendelea kuhamasisha wadau kuendelea kutumia bandari hiyo.

“Unajua ni jambo jipya na watu wengi wanataka kuja kuchukulia mizigo Dar es Salaam, lakini tunaandaa utaratibu utakaolazimu mizigo hii ikachukuliwe kule,” amesema.

Julai 31, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alizindua mradi wa kimkakati wa Bandari ya Kwala utakaopunguza gharama za usafirishaji, kuondoa msongamano wa malori jijini Dar es Salaam, na kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi mkoani, Rais Samia alisema kituo hicho ni suluhisho la muda mrefu kwa changamoto ya ongezeko la mizigo na meli bandarini.

“Ni wazi kuwa kituo hiki ni jibu la kiu ya muda mrefu ya Tanzania kuwa na bandari kavu ya kisasa nje ya jiji la Dar es Salaam, hiyo kina umuhimu mkubwa,” alisema Rais Samia.

Akieleza takwimu za matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam, Rais Samia alidokeza ongezeko la matumizi ya bandari hiyo kwa wastani wa asilimia 25 hadi 30 kila mwaka na kukua kwa shehena za mizigo kutoka tani milioni 23.69 mwaka 2023 hadi tani milioni 27.76 mwaka 2024, huku idadi ya meli ikiongezeka kutoka 1,860 hadi 1,990.

Ukuaji huo wa shughuli za bandari, alisema, umeongeza msongamano mkubwa wa malori jijini Dar es Salaam na mrundikano wa makasha bandarini, kwa kuwa usafirishaji mwingi wa mizigo hufanyika kwa njia ya barabara, hali inayopunguza ufanisi na ushindani.

Alisema uwekezaji katika kituo cha Kwala kama sehemu ya kupanua bandari kwa kuhamishia shughuli kadhaa kutoka Dar es Salaam kwenda Kwala, hatua itakayoongeza wigo wa huduma na kuboresha kasi ya upakuaji na usafirishaji wa mizigo.

Mmoja wa watumishi katika Kitengo cha Mipango Miji Jiji la Dar es Salaam, ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema wananchi ni sehemu muhimu katika mchakato wa kubadilisha matumizi ya ardhi na kwamba ushirikishwaji wao ni matakwa ya kisheria yanayopaswa kuzingatiwa kabla ya uamuzi wowote kufanyika.

Amesema mamlaka za upangaji, ambazo kisheria ni halmashauri zote kuanzia za miji, manispaa hadi wilaya, zinapaswa kuhakikisha kila hatua ya upangaji, hasa mabadiliko ya matumizi ya ardhi, inafanyika kwa kuzingatia sheria na kwa kuwashirikisha wananchi wanaoishi au kutumia maeneo husika.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji Sura ya 355 ya mwaka 2007, pamoja na Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 na ile ya Ardhi ya Vijiji Na. 5, wananchi wana haki ya kushirikishwa. Halmashauri zimetajwa wazi kama mamlaka za upangaji, hivyo zina wajibu wa kuhakikisha mabadiliko yoyote ya matumizi ya ardhi yanazingatia sheria na masilahi ya umma,” amesema.

Amesema matumizi ya ardhi yanapaswa kutengwa kwa kuzingatia mahitaji mbalimbali kama vile makazi, huduma za kijamii, shule, hospitali, makaburi, miundombinu ya barabara, umeme na maeneo ya viwanda.

Ameeleza matumizi hayo hayawezi kuchanganywa kiholela kwa kuwa yapo ambayo ni rafiki na mengine si rafiki.

“Kwa mfano, huwezi kupanga eneo la shule karibu na kiwanda kikubwa kwa sababu hayo ni matumizi yasiyowiana. Hivyo, kama kuna ICD zimejengwa kwenye makazi ya watu, inatakiwa kufuatiliwa kibali chake,” amesema.

Msimamizi wa bandari kavu

Msimamizi wa moja ya bandari kavu, James Masanja, amesema wanapojenga wanapatiwa vibali, na asilimia kubwa huwa ni maeneo yaliyokuwa wazi, na mengine yakifanyiwa shughuli za kilimo cha mboga mboga au ununuzi wa nyumba.

Amesema vibali vya uendeshaji wa ICD vinatolewa na mamlaka husika baada ya tathmini kufanyika, na si kwa kujichagulia tu maeneo.

“Tuna nyaraka zote, hatuingii maeneo ya watu kwa nguvu, bali kwa kufuata utaratibu kutoka kwa wahusika. Pia, hatuwezi kuzuia magari kuja kupakia na kushusha mizigo,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Wamiliki wa Bandari Kavu Tanzania (CIDAT), Meleck Shange, amesema bandari kavu zote zinazojengwa zinafuata utaratibu na kupatiwa leseni, na ukubwa wa eneo linalokidhi vigezo ni mita za mraba 10,000 hadi 20,000 kwa zamani, na kwa sasa ni kuanzia mita za mraba 20,000 hadi 60,000.

Amesema ongezeko la ICD ni kutokana na wingi wa mizigo inayoingia bandari, jambo lililochangia kukosekana nafasi, hivyo kufunguliwa kwa bandari kavu nyingi.

“Hili linalotekea la kuwepo kwa bandari kavu nyingi ni kwa sababu hatukuandaliwa, ndiyo maana tumejikuta kila kukicha zinafunguliwa, na jambo hili limeongezeka zaidi baada ya kuongezwa kwa kina, ambapo meli moja inayoingia inakuwa sawa na meli mbili hadi tatu kwa meli za zamani,” amesema.

Amesema kwa sasa wana jumla ya ICD 90, wakitarajia wiki moja ijayo zitaongezeka nyingine mbili kutokana na uhitaji wa bandari hizo.

Amesema idadi hiyo imegawanyika kwenye makundi manne tofauti, akieleza kwa makontena yenye mizigo zipo 17, zikitarajiwa kuongezeka mbili.

Bandari kavu za magari zipo 11, makasha matupu sita, na za kusafirisha mizigo nje zipo 56, zikiwa zimechanganywa na za Kibaha, mkoani Pwani.

“Hali hii inadhihirisha uhitaji mkubwa wa bandari hizi hapa nchini. Tumekuwa na mfululizo wa vikao na mamlaka zinazosimamia bandari, ambapo kikao cha mwisho kimefanyika Jumatano iliyopita, Februari 18, kujadili changamoto ya ufinyu wa nafasi katika maeneo ya bandari kuu ili kupata ufumbuzi wa kudumu,” amesema Shange.

Pia, Shange amesema utaratibu wa bandari unawapa siku tano tu kuondoa mizigo, hata hivyo, kutokana na mrundikano uliopo, wasimamizi wa bandari wameomba wasishinikizwe kufanya malipo ya papo hapo, badala yake wapewe nafasi ya kuiondoa kwanza ili kupata nafasi, na malipo yakamilishwe baada ya zoezi hilo.

Shange amewaomba radhi wananchi kwa kadhia wanayokutana nayo, akieleza si kusudio lao, bali hawakuandaliwa katika upokeaji wa mizigo baada ya DP World kuingia hadi kufikia hatua ya kuwa na bandari kavu maeneo mengi ya jiji na Serikali kukubali baadhi ya maeneo kuondolewa kwa watu, likiwamo eneo la Kurasini.

Moja ya Bandari Kavu iliyopo eneo la Mchicha, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam



Usajili na uendeshaji wa bandari kavu nchini Tanzania husimamiwa kisheria chini ya Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania Sura ya 415 na Kanuni zake za Ulinzi wa Mizigo na Usalama wa Utendaji Kazi katika Bandari na Bandari Kavu za mwaka 2023.

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inaratibu bandari hizi, zikiwamo za Ihumwa, Fela, Katosho, Kurasini na Isaka. Bandari kavu hufanya kazi kama vituo vya kati vilivyounganishwa na reli, barabara na bandari kuu kwa ajili ya shehena za baharini.

Pia, kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 na Sheria ya Kutwaa Ardhi ya mwaka 1967, eneo la bandari kavu lazima lipatikane kisheria na fidia kulipwa pale inapostahili.