BAADA ya hekaheka za Dabi ya Kariakoo iliyopigwa jana usiku kwenye Uwanja wa New Amaan visiwani Zanzibar, uhondo wa Ligi Kuu Bara umehamia katika miji ya Mwanza na Singida wakati mechi mbili za Ligi Kuu zikitarajiwa kupigwa leo.
Simba na Yanga ziliumana juzi katika pambano la kwanza la Ligi Kuu kwa msimu huu ambapo bila shaka matokeo mmeyasikia kutoka visiwani na sasa kazi inahamia CCM Kirumba, Mwanza wakati Pamba Jiji itakapovaana na Azam FC kuanzia saa 10:00 jioni, huku mapema saa 8 mchana Singida Black Stars itaikaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa Airtel, mkoani Singida.
Pambano la jijini Mwanza linasubiriwa kwa hamu kutokana rekodi ya mechi mbili zilizopita baina yao msimu uliopita, ambapo Pamba ikiwa nyumbani Kirumba iliizima Azam kwa bao 1-0, baada ya awali kutoka suluhu katika mechi ya duru la kwanza kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Timu hizo zinakutana kila moja ikitoka kushinda nyumbani katika mechi ya Ligi Kuu iliyopita, Azam ikiifumua Mtibwa Sugar mabao 3-0, huku Pamba ikizima Namungo kwa bao 1-0, lakini zikiwa zimetenganishwa katika msimamo kwa tofauti na pointi moja tu.
Pamba ipo nafasi ya tatu kwa sasa katika msimamo ikiwa na pointi 23 kutokana na mechi 14, wakati Azam ikiwa nyuma yao na alama 22, lakini ikicheza mechi pungufu ikishuka mara 10 tu, lakini kila mmoja ikiwa na matokeo ya kujivuna kwa msimu huu.
Katika mechi tano zilizopita kwa wenyeji Pamba, imeshinda mbili mfululizo baada ya kutoka sare moja na kupoteza pia mbili zilizokuwa za mfululizo, wakati Azam katika mechi tano zilizopita za Ligi Kuu imeshinda zote na imetoka kushiriki michuano ya CAF ikiweka rekodi ya aina yake.
Azam ilikuwa ikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika na kumaliza ikishika nafasi ya tatu katika Kundi B ikivuna pointi tisa, zikiwa ni nyingi zaidi kw msimu huu iliyoshiriki makundi kwa mara ya kwanza kwa timu zote za Tanzania zilizoiwakilisha nchi , ikiwamo Simba, Yanga na Singida BS.
Itashuka Kirumba ikisaka ushindi wa kwanza mbele ya Pamba, lakini ikitaka kuendeleza rekodi ya kuwa miongoni mwa timu mbili ambazo hazijapoteza mechi hadi sasa katika Ligi Kuu ikiwamo na Yanga inayoongoza msimamo.
Ikiwategemea nyota kama Feisal Salum ‘Fei Toto’ mwenye mabao manne na asisti nne, Idd Seleman Nado mwenye mabao matano na washambuliaji Japhte Kitambana na Jean Jacques Ngita, Azam itakuwa na kazi ya kulinda isipoteza kwa mara nyingine kwa wababe hao wa Mwanza.
Hata hivyo, huenda haitakuwa rahisi kutokana na rekodi tamu za Pamba ikiwa nyumbani na kwa mechi za msimu huu chini ya kocha Mkenya, Francis Baraza huku ikiwategemea kina Peter Lwasa, Mathew Momanyi, Kelvin Nashon, John Nakibinge, Mohammed Yottah Camara kuibeba nyumbani.
Kwa aina ya soka za timu zote ni wazi wakazi wa Mwanza watapata burudani ya aina kwa dakika zote 90, lakini kubwa ni kila timu kusaka pointi tatu zitakazoiweka pazuri.
Pamba ikiibuka na ushindi itafikisha pointi 26, wakati Azam itafikish 25 na kuzidi kujikita katika Tano Bora ya Ligi Kuu iliyoingia ngwe ya lala salama baada ya duru la pili kuanza kushika kasi.
Mapema mchana Singida itaonyeshana kazi na Wagosi wa Kaya kila moja ikitoka kuambuli sare katika mechi ya mwisho zilizopita za ligi hiyo.
Singida ilitoka sare ya 1-1 ugenini mbele ya Namungo kama ilivyokuwa kwa Coastal ilipoumana na JKT Tanzania, huku rekodi zikionyesha mwisho kwa timu hizo kukutana katika mechi ya Ligi Kuu, ilikuwa ni Aprili 10, 2025 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Wagosi kushinda mabao 2-1, yaliyofungwa na Josaphat Arthur Bada aliyeanza kwa kujifunga dakika ya 47.
Bada anayeichezea kwa sasa JS Kabylie ya Algeria, alianza kujifunga kisha bao lingine la Coastal likafungwa na Bakari Msimu dakika ya 82, huku la Singida likifungwa na Jonathan Sowah anayeichezea Simba msimu huu kwa penalti dakika ya 76.
Singida inaingia katika mechi hiyo ikiwakosa nyota wawili, waliowasimamisha ambao ni kipa, Amas Obasogie kwa tuhuma za upangaji wa matokeo na kiungo, Khalid Aucho kwa utovu wa nidhamu, huku wote wakisimamishwa kwa kipindi cha miezi mitatu.
Katika msimamo, Singida iko nafasi ya 10 na pointi 16, baada ya kucheza mechi 10, ikishinda minne tu, ikitoka sare minne na kupoteza miwili, huku Coastal ikiwa nafasi ya 12 na pointi 15, ikishinda mitatu, ikitoka sare sita na kuchapwa sita.
Kocha Mkuu wa Pamba, Francis Baraza amesema ushindi walioupata katika mechi mbili zilizopita kwenye uwanja huo zinawapa morali, licha ya kukiri ugumu wanaoenda kukutana nao dhidi ya Azam, kutokana na ubora mkubwa wa wachezaji wa timu hiyo.
“Nidhamu tuliyoionyesha dhidi ya Coastal Union na Namungo ndio ambayo tunapaswa kuiendeleza kwa Azam, tumekuwa na wiki zaidi ya mbili za maandalizi tangu mechi yetu ya mwisho, hivyo, tupo tayari kuendelea pale tulipoishia,” amesema Baraza.
Kwa upande wa Kocha wa Azam FC, Florent Ibenge, amesema licha ya ugumu anaoenda kukutana nao ila katika mechi mbili za hivi karibuni amefurahishwa na viwango vya wachezaji wa timu hiyo, hususani kwenye utumiaji wa nafasi za kufunga mabao.