Maxime ahofia kitu kwa kikosi chake akiisubiri Fountain Gate

WAKATI Mbeya City ikitamba kuendeleza ubabe Ligi Kuu Bara, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mecky Maxime ameonyesha hofu ya kukaa muda mrefu bila kucheza akidai inaweza kuwaathiri kesho watakapoikabili Fountain Gate.

Pia ameeleza wachezaji wake kuwa fiti baada ya kushinda mchezo uliopita dhidi ya TRA United kwa mabao 2-0 mjini Tabora akidai ni mchezaji mmoja tu, Yacouba Sogne, atakayekosa mechi hiyo kutokana na kuwa majeruhi.

Mbeya City haikuwa na matokeo mazuri chini ya kocha Malale Hamsin aliyeipandisha Ligi Kuu kabla ya uongozi kumvuta kikosini Maxime ambaye anaendelea kuinoa timu hiyo.

Timu hiyo  inawakaribisha Fountain Gate kwenye Uwanja wa Sokoine ikijivunia ushindi katika mchezo wake wa mwisho, Februari 7, huku wapinzani wao wakiwa hawajaonja pointi tatu kwenye mechi sita mfululizo.

Utamu na ugumu wa mchezo huo ni timu zote kuwa nafasi mbaya kwenye msimamo ikiwa wenyeji wamevuna pointi 13 katika nafasi ya 13, ilhali Fountain Gate wakiwa na pointi 12 kwenye nafasi ya 15 baada ya michezo 14 kila upande.

Maxime amesema baada ya kuonja ushindi walioukosa kwa muda mrefu, ari, nguvu na morali kikosini imeongezeka kwa wachezaji na matarajio yao ni kuendeleza walipoishia ili kujiweka pazuri.

Amesema hofu yake ni kukaa muda mrefu bila kucheza hali ambayo inaweza kuwaathiri kwakuwa ili mchezaji au timu iwe bora lazima iwe na michezo mfululizo ili kuwaweka fiti zaidi.

“Tunajua ugumu na umuhimu wa mchezo huu kwakuwa Fountain Gate nao wanahitaji ushindi kama ilivyo kwetu, tutamkosa mchezaji Yacouba aliyeumia tangu mechi iliyopita ila tumejipanga kushinda mchezo huu,” amesema Maxime.

Kipa wa timu hiyo, Soud Dondola amesema wanaiheshimu Fountain Gate kutokana na matokeo iliyo nayo akieleza kuwa matarajio ni kushinda mchezo huo kutokana na morali waliyonayo kwa sasa.

“Tumeimarika na tumeungana kiasi kikubwa uwanjani, hatuna kisingizio chochote na tunaenda kutimiza wajibu wetu kuhakikisha mashabiki wetu wanapata burudani,” amesema Kipa huyo.