NYUMBU NA MSEMO WA ‘TAHADHARI NA ADUI KIUMBE’

Msanii kutoka Zanzibar Bi Fatma Issa aliimba tahadhari na adui kiumbe, daima asikusibu na Mungu akuepushie.

Nyumbu wakiwa wanazaliwa katika eneo la Ndutu huomba sana Mungu awaepushie adui kiumbe kama Fisi, Simba, chui na mbweha ambao nao msimu huo huhamia katika eneo la Ndutu hifadhi ya Ngorongoro ili kuwavizia Nyumbu na watoto wao.

Hata hivyo kwa kuwa  Mungu ni wa wote, huwaepusha nyumbu na adui hao kwa kuwa katika  safari ya nyumbu, kuanzia wanapozaliwa Ndutu na kuanza mzunguko wa kuhama kila mwaka kuelekea  Kenya, hukabiliana na changamoto nyingi za kuliwa na wanyama wala nyama lakini wengi husalimika.

Kila nyumbu mzima (adult) ni ushahidi wa ustahimilivu mkubwa kwamba alinusurika hatari wakati wa kuzaliwa, akapita salama katika mito yenye mamba na wanyama wanaokula Nyama (Predators) katika maisha ya kila siku. Kuishi hadi utu uzima kwa nyumbu ni matokeo ya ushindi dhidi ya vikwazo vingi vya asili vilivyojaa taabu, chuki, hila na madhila.