Fursa mpya kwa wasomi CUoM ikijenga kituo cha michezo kuuza vipaji Mbeya

ILI kukuza na kuendeleza vipaji na kufungua fursa za uchumi na ajira kwa wasomi, Chuo Kikuu Katoliki Mbeya (CUoM) kimesema kinatarajia kufungua kituo maalumu cha michezo ‘Academy’ mahsusi kwa wahitimu chuoni hapo.

Akizungumza wakati wa fainali ya michezo ya Chuo hicho ‘Interclass’, rais wa serikali ya wanafunzi Lalgus Kilewa amesema ili kuondokana na wahitimu wenye vipaji kusubiri ajira, michezo inaweza kuwa suluhisho kwao.

Amesema wapo wanafunzi wasomi wanaohitimu masomo yao ilhali wana uwezo na vipaji haswa upande wa mpira wa miguu na kufanikisha chuo hicho kufanya biashara kwa kuuza wachezaji.

“Mpira kwa sasa ni fursa kibiashara na ajira, wapo wasomi wenye vipaji hivyo kupitia program hii ya michezo chuoni hapa tunalenga huko mbeleni tuwe na akademi kwa ajili ya kuuza vipaji.

“Kwa hapa Mbeya tunazo timu za Ligi Kuu kama Tanzania Prisons na Mbeya City, wapo KenGold na nyingine madaraja ya chini, tunaweza kutumia fursa hii kutengeneza ajira badala ya kusubiri zile za serikali,” amesema Kilewa.

Kwa upande wake waziri wa michezo wa chuo hicho, Joseph Mlundi, amesema lengo la michezo hiyo ni kuwaweka wanafunzi katika umoja na kuibua vipaji akibainisha kuwa mkakati ni kuendelea kuandaa michuano hiyo.

“Malengo ni kuona vipaji vinavyoonekana vinaendelezwa ndio maana michuano hii tunaiandaa kwa hadhi ya juu, wapo wachezaji wenye uwezo haswa mpira wa miguu, wakisimamiwa na kuendelezwa wanaweza kufika mbali,” amesema Mlundi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, Afisa Tarafa Kata ya Sisimba, John Mboya amesema serikali inatambua na kuthamini michezo, hivyo itaendelea kutoa sapoti kwa kundi hilo.

“Tuwapongeze CUoM kwa maandalizi ya michezo hii, kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa bonasi na sapoti, tunaamini eneo hili litakuwa chachu kwa wasomi wahitimu kufikia malengo yao,” amesema Mboya.