Uwanja wa Mpaka kufungwa kupisha maandalizi AFCON 2027

SERIKALI imetangaza kuufunga Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia mwezi huu ili kupisha awamu ya mwisho ya ukarabati mkubwa, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.

Akizungumza katika mahojiano na gazeti la The Citizen, Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, amethibitisha kuwa ukarabati huo utachukua kati ya miezi sita hadi mwaka mmoja.

Msigwa amebainisha kuwa, awamu hii ya mwisho itahusisha maboresho makubwa kwenye eneo la kuchezea (pitch) na maeneo mengine muhimu ya uwanja huo ili kukidhi vigezo vya kimataifa.

“Huu ni ukarabati wa mwisho ambao utahusisha kazi kubwa kwenye nyasi na miundombinu inayozunguka uwanja. Pindi kazi itakapoanza, uwanja hautatumika kwa mechi yoyote,” amesema Msigwa.

Aidha, aliongeza kuwa iwapo kuna ratiba za mechi zinazoweza kukamilika kabla ya ukarabati kuanza, mechi hizo zitaendelea kama zilivyopangwa. Hata hivyo, alisisitiza kuwa timu zinazoutumia uwanja huo zitalazimika kutafuta viwanja mbadala mara tu kazi itakapoanza.

Kwa mujibu wa maboresho ya ratiba ya Ligi Kuu Bara, mechi tatu kwa msimu huu zimepangwa kuchezwa hapo ambazo ni Azam vs Yanga (Machi 15, 2026), Azam vs Simba (Aprili 5, 2026) na Simba vs Yanga (Mei 1, 2026).

Hatua hii ya kuufunga uwanja huo inatarajiwa kuwa na athari kubwa kwa soka la ndani na kimataifa, ikizingatiwa kuwa Uwanja wa Benjamin Mkapa ndio kitovu kikuu cha mechi kubwa na za kitaifa nchini Tanzania.