Hali bado tete Mashariki ya Kati, mashambulizi yakiingia siku ya tatu

Mvutano wa kijeshi unaoendelea Mashariki ya Kati umechukua sura mpya leo baada ya Israel kuendeleza mashambulizi dhidi ya kundi la Hezbollah huku hali ya taharuki ikiongezeka katika nchi kadhaa za eneo hilo na hata kuathiri masoko ya dunia.

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz ametangaza hadharani kuwa Katibu Mkuu wa Hezbollah, Naim Qassem, sasa ni shabaha ya kuondolewa kufuatia mashambulizi ya makombora yaliyodaiwa kurushwa na kundi hilo kuelekea Israel.

Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Katz alisema Hezbollah italipa gharama kubwa kwa hatua hiyo, kauli inayotafsiriwa na wachambuzi kama ishara ya kuongezeka kwa makali ya mapambano na uwezekano wa operesheni za moja kwa moja dhidi ya uongozi wa juu wa kundi hilo.

Tayari Israel imeanzisha mashambulizi dhidi ya maeneo yanayohusishwa na wanamgambo wa Kishia wa Hezbollah nchini Lebanon, moja ya washirika wakuu wa Iran katika Mashariki ya Kati, baada ya Hezbollah kudai kurusha makombora na ndege zisizo na rubani kuelekea Israel kulipiza kisasi cha kuuawa kwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei.

Moshi ukiwa umetanda angani katika moja ya maeneo Tehran. Picha na Mtandao



Shirika la habari la serikali ya Lebanon (NNA) lilisema tathmini ya awali inaonyesha watu 31 wameuawa na 149 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo, ambayo Israel ilisema yalilenga vitongoji vya kusini mwa Beirut vinavyodhibitiwa na Hezbollah. Israel pia ilidai kuwalenga wanamgambo waandamizi wa kundi hilo.

Wakati huohuo, Israel imeanzisha mashambulizi zaidi dhidi ya Iran. Milipuko ilisikika katika maeneo mbalimbali ya Tehran, huku shambulio katika mji wa Sanandaj, ulioko mkoa wa Kurdistan magharibi mwa Iran, likisababisha vifo vya takribani watu watatu, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.

Wakati huohuo, athari za mzozo huo zimeanza kuonekana wazi katika uchumi wa kimataifa. Bei ya mafuta ghafi imepanda kwa kasi kufuatia hofu ya kuvurugika kwa usafirishaji wa nishati katika njia muhimu za baharini.

Mafuta aina ya Brent yalipanda kwa zaidi ya asilimia sita na kufikia Dola za Marekani 77.57 (Sh196,735) kwa pipa huku mafuta ghafi ya Marekani yakifikia dola 71.17 (Sh181,839) kwa pipa.

Wakati masoko ya hisa yakidorora, wawekezaji wamekimbilia mali salama kama dhahabu, ambayo nayo imepanda thamani.

Ongezeko hili la bei linaibua hofu ya kurejea kwa mfumuko wa bei duniani na kudhoofisha juhudi za kufufua uchumi katika mataifa mengi yaliyokuwa bado yanajikongoja baada ya misukosuko ya miaka ya karibuni.

Hamad Hussain, mchumi wa masuala ya hali ya hewa na bidhaa katika kampuni ya Capital Economics yenye makao yake Uingereza, amesema kwa uchumi wa dunia, kuendelea kupanda kwa bei ya mafuta kutaongeza shinikizo la mfumuko wa bei.


“Ikiwa bei ya mafuta ghafi itapanda hadi dola 100 kwa pipa na kubaki katika viwango hivyo kwa muda, hilo linaweza kuongeza kwa asilimia 0.6 hadi 0.7 kwenye mfumuko wa bei wa dunia,” alisema, akibainisha kuwa hali hiyo pia itasababisha ongezeko la bei ya gesi asilia.

“Hii inaweza kupunguza kasi ya sera za kupunguza viwango vya riba (monetary easing) na benki kuu hasa katika masoko yanayoibukia, ambako watunga sera huwa makini zaidi kwa mabadiliko ya bei za bidhaa,” ameongeza.

Katika Ghuba ya Uajemi, hali ya wasiwasi imezidi kuimarika. Ubalozi wa Marekani nchini Bahrain umewatahadharisha raia wake kuepuka hoteli katika mji mkuu wa Manama, ukieleza kuwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora kutoka Iran yanaendelea, sambamba na taarifa za mipango ya kigaidi inayoweza kulenga raia wa Marekani bila onyo.

Tahadhari kama hizo zimetolewa pia kwa raia wa Marekani walioko Jordan, zikisisitiza umuhimu wa kuwa macho na kuchukua tahadhari binafsi.

Kwa upande mwingine, Marekani ilithibitisha vifo vya wanajeshi wake watatu katika operesheni zinazoendelea, waliouawa katika kambi moja nchini Kuwait.

Rais wa Marekani, Donald Trump amewaelezea waliouawa kuwa ni wazalendo wa kweli wa Marekani, lakini akakiri kuwa huenda vifo zaidi vikatokea kadri operesheni zinavyoendelea.

Amesisitiza kuwa mashambulizi dhidi ya Iran yataendelea hadi malengo yote yatakapofikiwa, bila kuweka bayana malengo hayo ni yapi hasa. Kwa mujibu wa jeshi la Marekani, zaidi ya shabaha 1,000 ndani ya Iran zimeshambuliwa tangu kuanza kwa mapigano makubwa mwishoni mwa wiki.

Hata hivyo, operesheni hiyo inaonekana kugawanya maoni ndani ya Marekani yenyewe. Kura ya maoni ya Reuters/Ipsos imeonesha kuwa ni takribani robo tu ya Wamarekani wanaunga mkono hatua hiyo, hali inayoweza kuathiri siasa za ndani kuelekea uchaguzi ujao wa Bunge.

Wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanaonya kuwa endapo kampeni ya kijeshi itachukua muda mrefu, inaweza kuibua athari za kisiasa na kiuchumi zisizotarajiwa, si tu kwa Marekani bali pia kwa washirika wake.

Kwa ujumla, mwelekeo wa matukio unaashiria kupanuka kwa wigo wa mzozo, huku kila upande ukionyesha msimamo mkali.

Kadri mashambulizi yanavyoendelea na tahadhari za kiusalama zikiongezeka, dunia inasubiri kuona iwapo juhudi za kidiplomasia zitaweza kupunguza joto la mivutano au kama eneo hilo litaingia katika awamu mpya ya mapigano yenye athari pana zaidi kwa utulivu wa kimataifa na uchumi wa dunia.

Jana, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Leo XIV alisema anafuatilia matukio yanayoendelea baada ya shambulizi la Marekani na Israel dhidi ya Iran kwa wasiwasi mkubwa na ametoa wito wa kusitishwa kwa kile alichokiita ‘mzunguko wa vurugu’.

“Natoa wito wa dhati kwa pande zinazohusika kubeba wajibu wa kimaadili wa kusitisha mzunguko huu wa vurugu kabla haujageuka kuwa shimo lisilorekebishika.

“Utulivu na amani havijengwi kwa vitisho vya pande kwa pande au kwa silaha…bali hujengwa kupitia mazungumzo yenye busara, ya kweli na yenye uwajibikaji,” alisema Papa Leo XIV wakati wa hotuba yake ya kila wiki kwa mahujaji katika Uwanja wa Mtakatifu Petro baada ya sala ya Jumapili.