Kibaha. Wananchi wa Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani, wameanza kunufaika na huduma mbalimbali za masuala ya ardhi zinazotolewa bila malipo kupitia Kliniki ya Ardhi inayoendelea kufanyika kwa siku sita kuanzia Machi 2 hadi Machi 8, 2026.
Kliniki hiyo ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yatakayofikia kilele chake Machi 8, mwaka huu.
Huduma zinazotolewa katika kliniki hiyo ni pamoja na utoaji wa elimu na ushauri kuhusu masuala ya ardhi, utoaji wa hati miliki papo kwa hapo, makadirio ya kodi ya pango la ardhi pamoja na uhuishaji wa miliki za ardhi zilizoisha muda wake.
Lengo ni kuwasaidia wananchi kupata huduma kwa urahisi na kutatua changamoto zinazowakabili bila kulazimika kusafiri umbali mrefu au kutumia gharama kubwa.
Baadhi ya wananchi walionufaika na huduma hizo akiwamo Habiba Rashid, ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuweka maofisa ardhi kuanzia ngazi ya kata ili kurahisisha utoaji wa elimu na usimamizi wa masuala ya ardhi, hasa wakati wa ununuzi wa viwanja, ili kupunguza vitendo vya utapeli.
Habiba amesema uwepo wa maofisa hao ngazi za chini utasaidia kupunguza migogoro na matukio ya utapeli yanayotokana na baadhi ya wananchi kutegemea wenyeviti wa mitaa au watendaji wasiohusika moja kwa moja na masuala ya ardhi.
Kwa mujibu wake, hali hiyo imechangia watu wengi kuingia mikataba isiyo rasmi na baadaye kujikuta wakipoteza fedha zao.
“Baadhi ya wananchi wamenunua ardhi kupitia watu wasiokuwa waaminifu, hali iliyosababisha migogoro isiyo ya lazima lakini tukiwa na wataalamu wa ardhi karibu na sisi wananchi wanaweza kutupatia mwongozo sahihi na kuzuia madhara hayo mapema,” amesema Habiba.
Kwa upande wake, Ahmed Abdalah amesema kliniki hiyo ni msaada mkubwa kwa wananchi ambao wanashindwa kufika katika ofisi za ardhi au kufuatilia haki zao wanapodhulumiwa. Amesema upatikanaji wa huduma hizo kwa karibu utawasaidia wananchi wengi kupata suluhisho la changamoto zao kwa wakati.
Naye Joshua Mwanga amesisitiza umuhimu wa Serikali kuwekeza zaidi katika utoaji wa elimu ya ardhi kwa wananchi ili waweze kuelewa taratibu rasmi za ununuzi na umiliki wa ardhi.
Amesema ukosefu wa uelewa wa kutosha umekuwa chanzo cha watu wengi kutapeliwa kwa kuuziwa ardhi na watu wasiokuwa waaminifu.
“Watu wengi wanatapeliwa kwa sababu hawajui utaratibu sahihi wa kununua ardhi. Ni muhimu Serikali ikawafikia wananchi kwa kuwapatia elimu ya kutosha ili wajilinde na matapeli,” amesema Mwanga.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kliniki hiyo leo Jumatatu, Machi 2, 2026, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Pwani, Rugambwa Banyikila amesema Serikali imejipanga kuhakikisha wananchi wanapata huduma zote muhimu za ardhi kwa ukamilifu bila kutozwa gharama yoyote katika kipindi hicho cha kliniki.
Amehimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo muhimu ili kutatua changamoto zao za ardhi na kupata nyaraka halali zitakazowasaidia kuepuka migogoro ya baadaye.
Amesema Serikali itaendelea kubuni mbinu za kuwafikia wananchi kwa karibu zaidi ili kuboresha usimamizi wa masuala ya ardhi na kulinda haki zao.