Mwananchi laizindua Serikali, yatangaza mkakati kumaliza foleni ya malori, ICDs Dar

Dar es Salaam. Serikali imeanza kuchukua hatua za kimkakati kukabiliana na msongamano wa malori na bandari kavu (ICDs) jijini Dar es Salaam kwa kusafirisha mizigo kwa njia ya reli kuanzia mwishoni mwa mwezi huu, kwenda Bandari Kavu ya Kwala.

Kauli hiyo imetolewa leo, Machi 2, 2026 na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa na kwamba kwa sasa zaidi ya asilimia 90 ya mizigo inayotoka Bandari ya Dar es Salaam husafirishwa kwa barabara, hali inayochangia msongamano mkubwa wa malori, uharibifu wa miundombinu, na ajali za mara kwa mara.

Waziri Mbarawa amebainisha mkakati huo, ambao si mara ya kwanza kutolewa na Serikali, ikiwa ni siku moja tangu Mwananchi iripoti changamoto kubwa ya foleni jijini humo, chanzo kingine kikiwa ni utitiri wa bandari kavu.

Ukuaji wa shughuli za ICD katika Jiji la Dar es Salaam umeibua malalamiko kutoka kwa wakazi wa maeneo ya pembezoni mwa barabara kuu na mitaa ya makazi, wakidai uwekezaji huo unafanyika bila kuzingatia kikamilifu mipango miji, athari za mazingira, na ushirikishwaji wa wananchi.

Bandari kavu ni vituo vya kupokea na kusafirisha makasha (makontena) nje ya bandari kuu, vikilenga kupunguza msongamano bandarini na kurahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka na kwenda mikoani au nchi jirani.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamesema ongezeko la vituo hivyo katikati ya makazi limegeuka kero, licha ya Serikali kuhimiza upanuzi wa miundombinu ya usafirishaji, ili kuharakisha biashara. Katika habari hiyo, Mwananchi lilionesha kero na adha wanazopata wananchi.

Leo Jumatatu, Machi 2, 2026, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa matanki 15 ya mafuta itakayofanyika kesho Jumanne, Kigamboni, Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi ni Rais Samia Suluhu Hassan, Profesa Mbarawa amesema Serikali imeanza kuimarisha ICD kubwa ya Kwala, mkoani Pwani, kwa lengo la kuhamishia shughuli nyingi za makontena nje ya jiji.

Amesema Serikali imejipanga kuhakikisha kati ya asilimia 70 hadi 80 ya mizigo inayokwenda katika maeneo yenye mtandao wa reli inasafirishwa kwa kutumia reli ya kisasa kupitia miundombinu ya SGR na MGR.

“Mzigo ukisafirishwa kwa reli, tunapunguza msongamano wa malori barabarani, ajali, na uharibifu wa miundombinu, huku tukiongeza ufanisi na kupunguza gharama kwa wafanyabiashara,” amesema.

Amesema mkakati huo ni sehemu ya mpango mpana wa Serikali wa kuimarisha sekta ya uchukuzi na kuongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Profesa Mbarawa amesema awali kulikuwa na utaratibu wa kutoa vibali na leseni nyingi za ICD, hali iliyosababisha vituo vingi kuanzishwa katikati ya jiji na kuongeza msongamano.

“Kuna mdhibiti ambaye anasimamia sheria, na ninaamini wakati anatoa kibali cha leseni alifuata sheria, lakini sasa Serikali tunakuja na utaratibu tofauti, ndipo tulianzisha ICD kubwa kwa sababu tunataka tuondoke na ICDs zilizopo hapa mjini zilizopewa leseni zamani,” amesema Mbarawa.

Profesa amesema Serikali imeanza kuimarisha ICD kubwa ya Kwala, mkoani Pwani, kwa lengo la kuhamishia shughuli nyingi za makontena nje ya jiji.

Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza msongamano wa malori katikati ya Dar es Salaam, kupunguza uharibifu wa barabara, na kuondoa kero kwa wananchi wanaoishi na kufanya biashara jijini humo.

“Tunataka tuondoe msongamano wa makontena hapa mjini, ndiyo maana tunaimarisha ICD ya Kwala na nyingine zilizopo nje ya jiji, ili mizigo ishughulikiwe huko; kwani kule zipo mbalimbali za watu wa Burundi, DRC na wananchi wengine.”

Profesa Mbarawa amesema Serikali imejipanga kuimarisha sekta ya uchukuzi kupitia uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya bandari na reli, hatua itakayoongeza ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam katika ukanda wa Bahari ya Hindi.

Julai 31, 2025, Rais Samia, akizindua Bandari Kavu ya Kwala, alisema inakwenda kupunguza gharama za usafirishaji, kuondoa msongamano wa malori jijini Dar es Salaam, na kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam.

“Ni wazi kuwa kituo hiki ni jibu la kiu ya muda mrefu ya Tanzania kuwa na bandari kavu ya kisasa nje ya jiji la Dar es Salaam, hiyo kina umuhimu mkubwa,” alisema Rais Samia.

Uwekaji wa jiwe la msingi

Profesa Mbarawa amesema Rais Samia anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa matanki 15 ya kuhifadhia mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam yenye ujazo wa 380,000 za mafuta, ambayo yamegharimu Sh678.6 bilioni.

Amesema hafla hiyo itafanyika Kigamboni katika eneo la Mnadani, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuimarisha uwezo wa bandari hiyo kuhudumia shehena ya mafuta na mizigo mingine ya kimkakati.

“Hatua hii inalenga kuongeza uwezo wa nchi katika uhifadhi wa nishati, kupunguza msongamano wa meli bandarini, na kuongeza ufanisi katika upakuaji na upokeaji wa mafuta,” amesema Profesa Mbarawa.

Kwa mujibu wa taarifa ya mradi, kwa sasa baadhi ya meli kubwa za mafuta hulazimika kusubiri kati ya siku sita hadi kumi kabla ya kupakua shehena zao kutokana na uhaba wa miundombinu ya kutosha. Kukamilika kwa matanki hayo kutapunguza muda wa meli kusubiri hadi wastani wa siku tatu kwa meli kubwa, hatua itakayoongeza kasi ya huduma bandarini.