Kufunga kwampa mzuka Adeyum Saleh

BEKI wa kushoto wa Bigman, Adeyum Saleh, amesema siri ya kufunga mabao zaidi kwa sasa katika kikosi hicho ni kutokana na umakini mkubwa aliokuwa nao wa kumalizia nafasi, hususani anapokuwa anatengeneza mashambulizi kutokea pembeni ya uwanja.

Akizungumza na Mwanaspoti, Adeyum aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu baada ya kuachana na Geita Gold, amesemamechi za hivi karibuni amekuwa akifunga mara kwa mara, baada ya benchi la ufundi kumsogeza mbele zaidi, licha ya kucheza beki. “Unapocheza beki haina maana huwezi kufunga kwa sababu zipo nafasi zinatokea na ukiwa makini unaweza kufanikisha hilo, kwangu najisikia furaha kuona nafanya hivyo, jambo linaloongeza motisha kwa kikosi chetu kwa msimu huu,” amesemaAdeyum.

Nyota huyo aliyewahi kuwika na timu mbalimbali zikiwemo za, Yanga, Coastal Union, Stand United, Kagera Sugar na Dodoma Jiji, amesemamwenendo wa Bigman sio mbaya zaidi, ingawa watapambana hadi mwisho wa msimu ndipo watakapojua hatima yao.

Beki huyo kwa sasa anashika nafasi ya pili ya wachezaji wa Bigman waliofunga mabao mengi, baada ya kufunga manne, nyuma ya Mnigeria Collins Kelvin Nwobodo, aliyefunga matano, huku kwa sasa kikosi hicho kikishika nafasi ya saba na pointi 27.