Kuna misuguano ya chini kwa chini inayoendelea Tanzania Bara, kuhusu nani hasa anapaswa kuteua wajumbe wa kamati ya Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo huku baadhi ya wabunge wakiendesha mfuko huo kama mali yao binafsi.
Lakini ukisoma kifungu cha 10 cha Sheria ya Mfuko wa Jimbo kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2020 na kuchapwa katika Gazeti la Serikali (GN) namba 848 la Oktoba 2,2020, inaeleza wazi muundo wa mfuko na wajumbe wanapatikanaje.
Nionavyo mimi, kuna haja ya Serikali hasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Ofisi ya Bunge, kutoa elimu ya nani mwenye mamlaka ya kuteua wajumbe wa kamati maana katika baadhi ya majimbo watu wanataka kutoana macho.
Licha ya kuwa sheria haimpi mamlaka mbunge ya kuteua wajumbe wa Kamati ya Mfuko wa Jimbo, sasa hivi kuna msuguano mkubwa katika baadhi ya majimbo, kati ya mbunge, mkurugenzi wa halmashauri na madiwani juu ya uteuzi wa wajumbe.
Wapo wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wameenda mbali na kuandika barua za uteuzi kwa maswahiba wao, na wanapoambiwa huo si utaratibu wa kisheria, wanaibua chuki zisizo na msingi.
Hiki ninachokisema kimejitokeza Februari 20, 2026 pale Moshi mjini mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ambapo Waziri mkuu alisema hadi anapoongea, mfuko wa Jimbo hilo ulikuwa haujaundwa.
Nikimnukuu waziri mkuu alisema, “Mheshimiwa mkurugenzi, nimeambiwa hata mfuko wa jimbo haujaundwa. Mnalumbana nani wawe wajumbe.” Kisha akamuuliza Naibu Waziri wa Tamisemi, Reuben Kwagilwa, kuwa sheria inasemaje.
Naibu Waziri akajibu kuwa kamati ya mfuko wa Jimbo haiwezi kuundwa bila kumshirikisha mbunge na ni kutokana na jibu hilo, Waziri Mkuu akamtaka Mkurugenzi, Mwajuma Nasombe, wamwache mbunge auende mfuko wa jimbo.
Nikimnukuu waziri mkuu alisema, “Mkurugenzi, mwacheni mbunge (Ibrahim Shayo), kama mna maoni yenu mpeni ushauri, atakachopitisha ndicho hicho. Mwacheni mbunge aunde mfuko wa jimbo,” msisitizo ni mbunge aunde yeye.
Kwa hiyo hiki kilichojitokeza Jimbo la Moshi mjini huenda kinajitokeza katika baadhi ya majimbo ya ubunge Tanzania Bara na kuibua msuguano usio wa lazima na mgogoro wa kutengeneza wakati sheria ya mfuko huo ipo wazi kabisa.
Sasa ukisoma GN ile namba 848 katika kifungu cha 10(1) inasema kutakuwa na Kamati ya Mfuko wa Jimbo itakayoundwa na kuitishwa na wabunge waliochaguliwa, na kamati hiyo itakuwa na idadi ya juu ya wajumbe saba.
Sasa kifungu kile kidogo cha 1(a) cha sheria hiyo, kinasema mbunge wa kuchaguliwa wa jimbo ndiye atakuwa mwenyekiti na ile (b) inasema ofisa mipango wa wilaya, ndiye atakuwa Katibu wa kamati ya mfuko wa jimbo. Ukienda kifungu kidogo cha 1(c) kinataja kuwa kutakuwa na wajumbe wawili ambao ni madiwani wanaotoka katika jimbo na mmoja awe mwanamke.
Kifungu cha 1(d) cha sheria hiyo kinaelekeza kutakuwa na wajumbe wawili ambao ni watendaji wa kata (WEO) wanaotoka katika jimbo ambalo mfuko unaundwa.
Ukiacha vifungu hivyo, kifungu kidogo cha 1(e) kinaeleza uwepo wa mjumbe anayetokana na Asasi ya Kiraia (NGO) ambayo ni hai iliyopo ndani ya jimbo ambaye atateuliwa sio zaidi ya kikao cha pili baada ya kamati kuzinduliwa.
Sasa sheria hiyo imeweka sharti la lazima na imetumiwa neno la Kiingereza “shall”, kwamba wale madiwani wawili na WEO wawili watateuliwa na madiwani na watendaji wa Kata kwa Tanzania Bara au Sheha kwa Zanzibar.
Hivyo, kwa mujibu wa sheria hiyo, hakuna mahali ambapo sheria inampa mamlaka mbunge kama mbunge, kuteua wajumbe wa hiyo kamati tofauti na dhana potofu iliyojengeka kuwa wana mamlaka na kila kitu na mfuko huo.
Nimeamua kutoa elimu hii ili kusaidia kuondoa misuguano inayojitokeza katika baadhi ya majimbo kwa mbunge kutaka yeye kuteua wajumbe wa kamati ambao wanatokana na madiwani, watendaji wa kata au kutoka katika NGO iliyo hai.
Ni lazima wabunge wajue kuwa nchi yetu inaongozwa kwa utawala wa sheria unaotaka mmoja awajibike kwa sheria, kuanzia Rais wa nchi hadi raia wa kawaida na kila Dola au taasisi hakuna aliye juu ya sheria, wote tuko ndani ya sheria.
Tukiruhusu wabunge kukiuka sheria na kuingiza utashi binafsi katika mambo ambayo yamewekewa utaratibu wa kisheria ni jambo la hatari sana.
Tunasema hakuna mtu au taasisi ambayo iko juu ya sheria au nje ya sheria sasa inakuwaje tunataka kuiweka pembeni sheria ya mfuko wa Jimbo na kutaka kuwapendelea watu fulani fulani waingie katika mfuko kinyume cha sheria.
Tusifanye maamuzi kwa woga kukidhi mahitaji ya kisiasa na wakurugenzi wa halmashauri mnapaswa kusimama kidete kusimamia sheria.
Ukisoma kile kifungu cha 10(2) na (3) cha sheria ya mfuko wa jimbo kinataka katika mwaka mpya wa Bunge, mbunge anapaswa kuitisha vikao katika jimbo kujadili masuala ya maendeleo katika kila kata, jimbo au katika wilaya husika.
Kifungu kidogo cha (4) kinasema kila kata itakuja na orodha ya miradi ya kipaumbele na itawasilishwa katika kamati ya mfuko wa jimbo, lakini utashangaa katika baadhi ya majimbo, mbunge ndiye anakuja na miradi anayoitaka yeye.
Ni muhimu sana kamati za jimbo zikasoma vizuri sheria hii kwani kazi ya kamati kwa mujibu wa kifungu kile cha 11, zina wajibu wa kujadili mapendekezo kutoka kwenye kata na kuyapitisha au kuyakataa, sio kutoka mfukoni mwa mbunge.
Tukiruhusu hili na hasa tukizingatia kuwa katika kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) chenye wabunge zaidi ya asilimia 95, kulikuwa na figisu za kila aina zilizozalisha chuki, hivyo mbunge anaweza kutumia nafasi hiyo kulipa kisasi kwa kata ambazo hazikumpa kura au zilimpa kura kiduchu. Tusiruhusu hili.
Sheria ni msumeno, hukata mbele na nyuma hivyo baadhi ya wabunge wasitumie ushawishi wa kisiasa kupotosha viongozi wa kitaifa na kutengeneza picha kuwa mkurugenzi wa halmashauri anamhujumu wakati anasimamia sheria.