Kuelekea siku ya wanyamapori miti zaidi ya 2,700 yapandwa Arumeru

Arusha. Kuelekea maadhimisho ya siku ya Wanyamapori duniani yanayofanyika kila mwaka, Machi 3, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameendelea na wiki maalum ya shughuli za uhifadhi wa mazingira, ikiwemo upandaji wa miti ya dawa na ya manukato.

Maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika Kitaifa kesho mkoani Arusha, yataongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji.

Leo Machi 2, 2026, akizungumza akiwa katika Shule ya Sekondari Mringa, wilayani Arumeru, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Alexander Lobora, amesema kuanzia Februari 25 2026, wamekuwa wakitoa elimu kuhusu uhifadhi wa wanyamapori, mimea na misitu.

Amesema lengo la wiki hiyo ni kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa mazingira kwa maisha ya wanyamapori na binadamu kwa ujumla.

“Tumekuja hapa kwa sababu mnajali na kutunza mazingira. Wanyamapori hawawezi kuishi bila mimea ambayo ni chakula chao. Ndiyo maana mwaka huu tunahamasisha upandaji wa miti ya dawa na mimea manukato,” amesema

Mkurugenzi huyo amesema kuwa katika shule hiyo yenye wanafunzi 2,700, wanatarajiwa kushiriki katika upandaji miti, huku akisisitiza kuwa uwekezaji wa elimu ya uhifadhi na mazingira kwa watoto ni msingi wa kudumisha uhifadhi wa mazingira nchini.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri), Dk Ernest Mjingo, amesema taasisi hiyo ina jukumu la kufanya tafiti za kisayansi zinazosaidia uhifadhi na kukuza utalii.

“Bila mazingira, wanyamapori hawapo. Elimu ya sayansi ni muhimu sana kwa kizazi cha sasa, hasa wanafunzi, ili waelewe kwa mtazamo wa kisayansi umuhimu wa kutunza mazingira,” amesema Mjingo.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri), Dk Ernest Mjingo, akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Machi 2, 2026 katika Shule ya Sekondari Mringa, wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha.



Amesema kuwa miti na wanyamapori haviwezi kutenganishwa, kwani viumbe hai wadogo huchangia uchavushaji wa mimea na uzalishaji wa chakula.

Kuhusu Tanzania,amesema iko mstari wa mbele barani Afrika katika uhifadhi wa wanyamapori, ikiongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya simba na kushika nafasi ya tatu kwa kuwa na nyati wengi.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, aliwataka wanafunzi kuwa mabalozi wa utunzaji wa mazingira.

“Tunaamini kupitia elimu mtakayotoa hapa italenga kuimarisha ushiriki wa jamii katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,”amesema

Mmoja wa wanafunzi hao, Vaileth Lazaro,amesema elimu ya mazingira ni muhimu katika makundi mbalimbali ya jamii ili kila mmoja awe mtunzaji.

“Tuna vilabu vya mazingira hapa na tunahamasisha upandaji wa miti kwani ina umuhimu katika mazingira na uhifadhi kwani tusipolinda mazingira yetu tutapata madhara mbalimbali ikiwemo ukame,hivyo tunaomba elimu hii itolewe katika makundi mengine ya kijamii,” amesema