WAZIRI ULEGA AZINDUA BODI YA USHAURI TBA, AITAKA KUJENGA NYUMBA ZA GHARAMA NAFUU

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, leo Machi 2, 2026, amezindua Bodi ya sita ya Ushauri ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na kuutaka wakala huo kuongeza juhudi katika ujenzi wa nyumba za gharama nafuu ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kumudu makazi bora.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri Ulega amesisitiza umuhimu wa kuzingatia ujumuishi katika miradi ya ujenzi kwa kuhakikisha miundombinu inakuwa rafiki kwa makundi yote ya jamii, ikiwemo watu wenye mahitaji maalum, pamoja na kuzingatia uwajibikaji wa kifedha, thamani ya fedha (value for money) na ufanisi katika utekelezaji wa miradi.

Amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka mkazo katika kuboresha sekta ya ujenzi, na kwamba Serikali imelenga kufikia ujenzi wa makazi bora 50,000 ifikapo mwaka 2030. Katika lengo hilo, TBA inatarajiwa kusimamia ujenzi wa nyumba 4,500, kuendelea na ukarabati wa majengo ya Serikali na usimamizi wa mali za umma.

Aidha, ameipongeza TBA kwa utekelezaji wa mradi wa kibiashara wa nyumba za makazi wa Canadian uliopo Masaki, jijini Dar es Salaam.

Awali, Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro, amesema wakala unaendelea kuendeleza maeneo 149 yaliyoiva kwa uwekezaji kwa kushirikiana na sekta binafsi, kufuatia kukamilika kwa upembuzi yakinifu na marekebisho ya sheria ya TBA.