Mbinu za usafiri wa bodaboda zinavyohatarisha maisha

Dar es Salaam. Ni jioni yenye msongamano Jijini Dar es Salaam, wakati ambao kila mtu akihangaika kurudi nyumbani kwa kutumia usafiri wa umma, na hapo pikipiki ‘bodaboda’ inaonekana kama njia ya haraka.

Bodaboda zinaonekana suluhisho kutokana na kuweza kupenya maeneo mbalimbali, hivyo kutokaa foleni kama ilivyo kwa vyombo vingine kama magari na bajaji.

Hata hivyo, madereva wengi sasa wameanza kubeba abiria wawili kwa wakati mmoja, wakivunja sheria za usalama barabarani huku bila kofia ngumu inayowalinda endapo kutatokea ajali.

Japokuwa ni njia ya kuongeza kipato katika nyakati ngumu za kiuchumi, lakini kwa upande mwingine ni hatari inayotishia maisha ya abiria na watumiaji wengine wa barabara.

Hali hii imekuwa ikionekana zaidi katika maeneo mbalimbali ya jiji, mathalani Mbagala, Kimara, Kariakoo na Tabata, ambako abiria wamekuwa wakitozwa kati ya Sh1,000 hadi Sh3,000 kulingana na umbali wa safari husika.

Mfano maeneo kama Mbagala Rangi Tatu wakati wa jioni, bodaboda wanasimama  eneo maalumu kuita wateja, na hapo mtu huchagua anataka kwenda Ubungo, Mwenge, Kariakoo, Posta na wengine Mbezi.

Aina hiyo ya usafiri ni sawia na ukienda Mwanza, Arusha, Moshi mkoani Kilimanjaro au Dodoma, ambako kubebwa “mshikaji” imekuwa jambo la kawaida.

“Kaa dada, tusubiri mwingine tuondoke, chombo haina foleni, hii tunafika haraka unakokwenda. Wapi unaenda, Ubungo au Mwenge?” anasikika bodaboda mmoja akizungumza na abiria.

Kwa mujibu wake, njia hiyo imekuwa rahisi kwake kupata kipato cha uhakika badala ya kusubiri abiria vijiweni, na wakati mwingine ni ngumu kupata kiwango cha fedha kinachoweza kutosheleza mahitaji ya kila siku.

“Ukikaa kijiweni hadi ufikishe Sh20,000 si rahisi, kwani abiria ni wa kubahatisha, na huwezi kupakia mara zote peke yako, inabidi mpakie kwa foleni ili kila mtu apate. Lakini huku nina uhakika, kwa sababu nikibeba abiria kwenda Ubungo mmoja Sh3,000, na wanakuwa wawili.

“Hao si wote wanaofika Ubungo, kuna wakati wanaishia Tabata, wanakupa Sh2,000 kila mmoja. Unaitia tena pale kwenda Mwenge kwa Sh2,000 kila mmoja. Hivyo hadi nirudi huku Mbagala nakuwa nimepata hadi Sh20,000. Nikienda mara tatu, narudi kulala nikiwa na uhakika wa maisha,” amesema dereva huyo.

Kauli yake inaungwa mkono na Meshack Mashaka anayesema safari moja ya kwenda Mwenge kutokea Mbagala hadi anarudi, ana uhakika wa kupata kuanzia Sh15,000.

“Japokuwa si rahisi, huko barabarani unakutana na vikwazo vingi, ikiwemo kutokuheshimiwa na madereva wa magari wanaotuona wasumbufu, wengine wanaweza kukutishia kukugonga kwa makusudi,” amesema.

Hata hivyo, hali hiyo ni hatari kwa afya, kwani wengi wao huendesha pikipiki hizo bila kuvaa kofia ngumu, jambo linalowaweka hatarini kuumia zaidi inapotokea ajali.

Kitendo hiki ni kinyume na Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168 ya mwaka 2019; kifungu cha 70 kinakataza kupakia abiria zaidi ya mmoja kwenye pikipiki, na kifungu cha 45(12) kinataka dereva kuvaa kofia ngumu.

Hali hiyo imekuwa ikileta usumbufu kwa wamiliki wa vyombo vya moto, ambao wanadai kulazimika kuongeza umakini barabarani kutokana na bodaboda kutofuata sheria.

“Ukiwa barabarani unajifunza kutoangalia alama pekee, bali na bodaboda, kwani wakati mwingine unaweza kuwa umeruhusiwa na taa uende, bodaboda anakukatisha ghafla mbele yako. Kama hujamuona, unasababisha ajali,” amesema Mesiah Masha, dereva wa daladala.

Amesema kutozingatia sheria za usalama barabarani kunakofanywa na bodaboda kumekuwa chanzo cha ajali nyingi, jambo alilotaka liangaliwe zaidi ili kudhibiti hali hiyo na kunusuru vijana wengi.

“Sheria iangaliwe wapi kuna shida, udhibiti uongezeke, hasa katika matumizi ya kofia za kujikinga,” amesema.

Abiria wanaonesha kupata ahueni ya usafiri, kwani zimekuwa zikiwarahisishia safari zao.

“Badala ya kutumia saa mbili kutoka Mbagala Rangi Tatu hadi Ubungo, dakika 30 zinatosha, kwani hukai foleni wala kuhangaika na joto kwa kubanana,” amesema Mariam Mshana, mkazi wa Mbagala.

Lawrence Lewis amesema uwepo wa bodaboda umeleta ahueni kwao kuwahi kazini na kurudi nyumbani, kwani hawalazimiki kusubiri daladala kwa muda mrefu.

“Sisi ambao tunapandia njia mara nyingi, magari yanakuja yamejaa. Ukiendelea kusubiri, unaweza kuchelewa, lakini kwa pikipiki au bajaji ni rahisi kufika kazini na kurudi nyumbani kwa wakati,” amesema.

Joseph John, mkazi wa Tegeta, amesema usafiri wa bodaboda ni hatari, hasa mkibebwa zaidi ya mtu mmoja, lakini kwa hali ya usafiri na foleni inawalazimisha kupanda ‘mishikaki’ ili kuwahi wanapokwenda.

Wakati Masha akieleza hayo, takwimu za Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) mwaka 2023/2024 zinaonesha kuwapo kwa ongezeko la leseni za bodaboda zilizotolewa kwa asilimia 44.5 mwaka wa fedha 2023/2024 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Ongezeko la bodaboda zilizopewa leseni ya kufanya shughuli zake nchini kumeibua mitazamo tofauti kutoka kwa wadau na vijana, huku ukosefu wa ajira ukitajwa kuwa moja ya sababu.

Ripoti hiyo ya Latra inabainisha kuwa ilitoa leseni 46,146 (D1) za pikipiki katika kipindi kilichoripotiwa, ikiwa ni ongezeko kutoka leseni 31,937 zilizotolewa kipindi kama hicho mwaka wa fedha 2022/2023.

Leseni zilizotolewa kwa pikipiki zilichangia takribani asilimia 54.1 ya leseni zote zilizotolewa kwa magari ya kubeba abiria binafsi.

Kadhalika, ripoti hiyo inaeleza kuwa idadi kubwa ya leseni za pikipiki zilitolewa eneo la kusini, ambapo kanda hiyo ilibeba asilimia 39.1, zikifuatiwa na maeneo ya kati na ziwa, ambapo kila moja ilikuwa na asilimia 17.8.

Eneo la mashariki lilichangia asilimia 16.4, wakati eneo la kaskazini lilikuwa na sehemu ndogo zaidi ya asilimia 8.9.

Takwimu za hali ya uhalifu na matukio ya usalama barabarani 2023 zinaonesha katika kipindi cha Januari hadi Desemba jumla ya matukio 435 ya ajali za pikipiki yaliripotiwa, ikilinganishwa na matukio 448 katika kipindi kama hicho mwaka 2022.

Idadi hiyo ni pungufu ya matukio 13, sawa na asilimia 2.9. Hata hivyo, katika kipindi hicho, idadi ya vifo vya ajali za barabarani iliongezeka kwa vifo 44 kutoka vifo 332 vilivyoripotiwa mwaka 2022 hadi vifo 376 mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 13.3.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, ajali hizo husababishwa na ukosefu wa elimu ya usalama barabarani kwa baadhi ya watumiaji wa vyombo vya moto na kutofuata sheria za usalama barabarani.

Akizungumzia suala hili, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (Darcoboa), Shifaya Anaselema, amesema “athari zipo nyingi kwa sababu wenye mamlaka hawafanyii kazi hili suala. Si bodaboda tu, hata bajaji, unakuta anapakia Tandika Sh500, na si ya kukodi auu bodaboda anapita mbele ya askari amepakia watu wawili bila kofia, hachukuliwi hatua.

“Imefika wakati wanaopaswa kusimamia kanuni wasimamie kama zilivyowekwa kwa mujibu wa sheria ili kuweka uwanja wa biashara sawa.”

Walipotafutwa Latra kupitia Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano, Salum Pazzy, amesema bodaboda na bajaji wanatakiwa kutambua leseni zao ni za usafiri wa kukodi, si za kukusanya abiria njiani kama daladala.

Amesema kwa mujibu wa sheria na kanuni za usafiri wa kukodi pamoja na kanuni za mamlaka, pikipiki na bajaji hupewa leseni kwa ajili ya kutoa huduma ya kukodishwa pekee, hivyo hawaruhusiwi kuingilia huduma ya daladala kwa kusimama vituoni au kukusanya abiria njiani kama vyombo vya usafiri wa njia maalumu.

“Ni kosa kisheria kwa bodaboda au bajaji kufanya kazi kama daladala. Kitendo hicho si tu kinavunja sheria, bali pia kinaharibu mpangilio na ufanisi wa utoaji wa huduma za usafiri mijini,” amesema Pazzy.

Amesema daladala zinaruhusiwa kubeba idadi kubwa ya abiria kwa nauli iliyopangwa na Serikali, jambo linalosaidia kupunguza gharama kwa wananchi na kupunguza msongamano wa magari mijini. Ametoa mfano kuwa daladala moja linaweza kubeba zaidi ya abiria 50 kwa nauli ya chini, tofauti na bajaji inayobeba abiria watatu kwa gharama kubwa zaidi.

“Abiria anaweza kulipa Sh600 au Sh700 kwa daladala, lakini kwa bajaji akalazimika kulipa Sh1,500 hadi Sh2,000 kwa safari hiyo hiyo. Hii inaongeza gharama kwa mwananchi na pia huathiri mfumo mzima wa usafiri wa umma,” ameongeza.

Kuhusu hatua zilizochukuliwa, Pazzy amesema Latra kupitia wakaguzi wake inaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, na pale inapobainika chombo kinatoa huduma kinyume na leseni yake, huchukua hatua ambazo ni kutoa elimu kwa wahusika, kutoza faini na kukamata vyombo vinavyotoa huduma bila leseni halali.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Boniphace Mbao, amesema bodaboda wengi wamekuwa wakifanya makosa ya kubeba abiria zaidi ya mmoja, huku wakiwa hawajavaa kofia ngumu.

 “Tumekuwa tukitoa elimu kwao kuhakikisha chombo kinakuwa kizima, kina bima, akiendesha atumie kofia ngumu. Hayo tumesema maeneo mengi, lakini tatizo hilo limekuwa likiendelea kufanyika, hali inayofanya sasa tumekuwa tukiwakamata, kuwapiga faini za papo kwa papo na wengine kuwapeleka mahakamani ili kuzuia hali hii,” amesema.