Jukwaa la vijana lazinduliwa Mtwara, Waziri ahimiza ushiriki wa sekta binafsi

Mtwara. Katika juhudi za kuendelea kuwezesha vijana jukwaa la vijana nchini limezinduliwa mkoani Mtwara limefunguliwa mahususi kutoa elimu ya fedha na mafunzo ya ujasiriamali yatakayowasaidia kujishughulisha kiuchumi na kujiingizia kipato.

Ufunguzi wa jukwaa hilo linalowaunganisha vijana nchi nzima ni mwendelezo wa jitihada za Serikali kwa kushirikiana na CRDB Bank Foundation. Katika uzinduzi huu ulioongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, taasisi ya CRDB Bank Foundation imekabidhi pikipiki 15, bajaji 5 na maguta 5 yenye thamani ya Sh140 milioni.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri Nanauka amesema Serikali peeke haiwezi kuwafikia vijana wote nchini hivyo ushiriki wa sekta binafsi kama CRDB Bank Foundation ni jambo linalohamasisha na uongozi wa Serikali iliyowapa nafasi kubwa vijana katika ajenda ya maendeleo ya taifa. 

“Serikali imeyaweka masuala ya vijana katika kipaumbele cha juu kwenye ajenda ya maendeleo ya taifa letu. Namshukuru Rais wetu, Samia Suluhu Hassan, kwa maono yake makubwa kuhusu vijana wa nchi yetu. Uamuzi wake wa kuunda Wizara ya Maendeleo ya Vijana chini ya Ofisi ya Rais unaonesha dhamira hiyo kwa uwazi zaidi,” amesema Waziri Nanauka.

Waziri amesema hayo ikiwa ni siku chache tangu, Serikali kuidhinisha matumizi ya Sh200 bilioni kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali wakiwemo vijana, fedha zitakazosimamiwa kwa utaratibu maalumu, ili ziwafikie walengwa na kuleta matokeo chanya katika sekta mbalimbali za uchumi.

Baada ya uzinduzi wa jukwaa hilo kitaifa Januari 10, kwa ngazi ya kikanda na mkoa tayari majukwaa kadhaa yamefunguliwa mkoani Mwanza, Singida na Tabora na jana ilikuwa zamu ya Mtwara.

“Napenda kuwahimiza vijana wa mkoa wetu wa Mtwara kuungana na wenzao nchi nzima kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazojitokeza kwenye maeneo yao. Tayari tumezindua jukwaa hili katika mikoa kadhaa na shughuli hii bado inaendelea. Tutafika katika mikoa yote nchini ili kuwapa vijana fursa ya kutekeleza mipango na mikakati yao ya kujikwamua kiuchumi,” amesema Waziri Nanauka.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Meneja Mwandamizi wa Ufadhili wa CRDB Bank Foundation, Baraka Kiyalo amesema wataendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali katika ajenda ya kuwawezesha vijana kiuchumi nchini kote ili kutoa mchango wake wa kukabiliana na umaskini, miongoni mwa changamoto kubwa zinazowasumbua watu wengi.

“Ushirikiano kati ya CRDB Bank Foundation na Wizara ya Maendeleo ya Vijana unalenga kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia programu ya IMBEJU. Tuna uzoefu wa kutosha kufanikisha hili unaosukumwa na dhamira ya dhati tuliyonayo,” amesema Kiyalo.

Meneja huyo amesema mikakati yao ya kuwawezesha vijana kwa mwaka huu imeanza na uzinduzi wa mradi wa Go Green na IMBEJU inayolenga kufadhili miradi ya vijana inayolinda mazingira na akawataka vijana na wajasiriamali mkoani Mtwara kutuma maombi yao kwani dirisha bado lipo wazi mpaka tarehe 12 mwezi huu.

“Kwa sasa dirisha la maombi lipo wazi kwa vijana wote wenye miradi au mawazo ya miradi inayolinda mazingira hivyo mnayo nafasi pia vijana na wajasiriamali wa Mtwara na mikoa mingine ya kanda ya kusini, na taifa zima kwa ujumla, kutuma maombi yenu kidijitali kupitia kiunganishi kilichopo kwenye tovuti ya taasisi ya CRDB Bank Foundation  au mitandao yetu ya kijamii,” amesema Kiyalo.

Naye Meneja wa  Kanda ya Kusini ya Benki ya CRDB, Lusingi Sitta amesema watakilea kikundi cha Imara Youth Saccos kilichopewa mtaji wezeshi kwa misingi imara ya Programu ya IMBEJU kwa kuwajengea wanachama wake uwezo wa kuanzisha na kukuza biashara endelevu, kuongeza kipato binafsi, na kupunguza utegemezi.

“Ushirikiano wetu na Serikali una mchango mkubwa katika kukuza biashara changa na ndogo zinazomilikiwa na vijana, kuongeza ajira, na kuimarisha uchumi wa kaya na jamii nzima kwa ujumla,” amesema Sitta.

Aidha, unaimarisha dhana ya ubia kati ya serikali na sekta binafsi katika kutekeleza ajenda ya maendeleo ya vijana nchini. Ofisi ya kanda ninayoiongoza itashirikiana kwa ukaribu na vijana hawa ili wawe mfano kwa wenzao nao kunufaika uwezeshaji unaofanywa na CRDB Bank Foundation.