Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Wanyamapori Duniani, siku maalum inayotambua mchango wa wanyamapori katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kimazingira.
Akizungumzia maadhimisho hayo Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania, Ephraim Mafuru, amesema kuwa, kwa Tanzania wanyamapori si urithi wa asili pekee bali ni sehemu ya utambulisho wa taifa.
“Wanyamapori ni uti wa mgongo wa sekta yetu ya utalii. Ni chanzo cha ajira na kipato kwa maelfu ya wananchi. Ni fahari inayolitangaza taifa letu kimataifa,” amesema Mafuru.
Ameongeza kuwa kupitia rasilimali hizo, Tanzania imeendelea kuwa kivutio kinachoongoza duniani, kikivutia wageni kutoka pande zote za dunia kufurahia vivutio vya asili vilivyopo nchini.
Mafuru amesisitiza kuwa Bodi ya Utalii Tanzania itaendelea kuhamasisha na kukuza utalii endelevu unaolinda mazingira, unaoheshimu bioanuwai, na kuhakikisha wanyamapori wanahifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Maadhimisho ya mwaka huu yameongozwa na kaulimbiu isemayo, “Medicinal and Aromatic Plants: Conserving Health, Heritage and Livelihoods” (Mimea Tiba na Harufu: Kuhifadhi Afya, Urithi na Maisha), inayotukumbusha kuwa utajiri wa bioanuwai ya Tanzania si uzuri wa asili pekee, bali ni chanzo cha afya, maarifa ya jadi, ajira na ustawi wa jamii.
Kaulimbiu hiyo inaweka msisitizo katika umuhimu wa kulinda mimea tiba na rasilimali nyingine za asili kama sehemu ya mkakati mpana wa uhifadhi unaounganisha mazingira, urithi wa kitamaduni na maendeleo endelevu ya taifa.