VIWANGO vya nyota wapya wa Simba, Libasse Guaye na Anicet Alain Oura, ambao wamesajiliwa katika dirisha dogo la Januari 2026, vimeanza kuvutia katika safu ya ushambuliaji ya wekundu wa Msimbazi huku kocha Steve Barker akitaka kuona muendelezo kutoka kwa wachezaji hao.
Guaye amefunga mabao mawili katika mechi tano za Ligi Kuu Bara, huku Oura akifunga mawili katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Tangu walipotua Msimbazi, nyota hao wameingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha Barker.
Nyota hao wameongeza kasi na nguvu katika maeneo ya pembeni, jambo linaloifanya Simba kuwa na makali zaidi safu yao ya ushambuliaji.
“Wameanza vizuri sana. Napenda jinsi wanavyoshirikiana na wachezaji wengine, mimi ni muumini sana wa kiwango cha timu na jinsi wanavyoweza kubadilika kutokana na mipango tofauti ya mechi ambayo tumekuwa nayo,” alisema Barker.
Guaye, mwenye umri wa miaka 22, hadi sasa ametumika katika mechi saba kati ya tisa za mashindano yote sawa na dakika 508, huku Oura, 26, akitumika katika mechi nane sawa na dakika 663, akicheza mechi tano mfululizo kwa dakika 90, ikiwemo moja ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Stade Malien ambapo alifunga bao ambalo liliifanya Simba kushinda mechi ya kwanza na pekee katika hatua ya makundi msimu huu.
Barker aliongeza kuwa: “Ni muhimu sana kwa wachezaji wapya kuonyesha ari ya ushindani, naamini tupo kwenye mwelekeo sahihi, ni suala la kuendelea kujitoa na kupambania matokeo katika mechi zinazofuata.”
Katika mechi iliyopita ya Ligi, nyota hao walikuwa mwiba kwa Yanga wakati Simba ikiwagomea watani zao kupoteza mechi ya saba mfululizo katika mashindano yote.
Baada ya kumalizana na Yanga huko Unguja, Zanzibar kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, kituo kinachofuata kwa Simba ni mechi ya Kombe la Shirikisho (FA) hatua ya 32 Bora dhidi ya B19 itakayochezwa Machi 7, mwaka huu.