Bei za mafuta juu, dizeli ikiongezeka bei mara mbili

Dar es Salaam. Watimiaji wa bidhaa za mafuta Tanzania wataendelea kuugulia maumivu ya ongezeko la bei baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kutangaza bei kikomo zitakazotumika Machi mwaka huu.

Katika bei hizo, watumiaji wa mafuta ya dizeli wameshuhudia ongezeko la bei mara mbili zaidi ikilinganishwa na wale wa petroli na mafuta ya taa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ewura, ongezeko hili la bei litagusa mafuta yanayoingia kupitia bandari zote za Tanga, Dar es Salaam na Mtwara.

Kuanzia leo Machi 4, 2026, bei ya rejareja ya petroli jijini Dar es Salaam imeongezeka hadi Sh2,864 kwa lita kutoka Sh2,788 ya Februari, ikiwa ni ongezeko la Sh76.

Dizeli imepanda kwa kasi zaidi ikiwa na ongezeko la  Sh157, ambapo itauzwa  Sh2,858 kutoka Sh2,701, huku mafuta ya taa yakiongezeka kwa Sh186 ambapo itauzwa Sh2,932 kutoka Sh2,746.

Hali kama hiyo imeonekana Tanga, ambapo petroli imeongezeka hadi Sh2,925 kwa lita Machi kutoka Sh2,849 Februari ongezeko la Sh76.

Dizeli imepanda kwa Sh157 ambapo itauzwa Sh2,919 kutoka Sh2,762, na mafuta ya taa yameongezeka kwa Sh186 ambapo yatauzwa Sh2,993 kutoka Sh2,807.

Mtwara pia imefuata mwenendo huo ambapo Petroli imeongezeka kwa Sh75 sasa itauzwa Sh2,956 kutoka Sh2,881 huku dizeli imepanda kwa Sh157, ikiuzwa  Sh2,951 kutoka Sh2,794, na mafuta ya taa yamepanda kwa Sh187  bei kikomo ikiwa Sh3,025 kutoka Sh2,838.

Taarifa hiyo ya Machi inaonyesha ongezeko la jumla katika bandari zote, huku dizeli na mafuta ya taa yakipanda mara mbili zaidi ya ongezeko lililoonekana kwenye petroli.

Katika taarifa yake ya bei, Ewura imesema bei rejareja katika soko la Ghuba ya Uarabuni zimeongezeka kwa asilimia 6.2 kwa petroli, asilimia 9.8 kwa dizeli na asilimia 7.4 kwa mafuta ya taa Machi.

Taarifa hii iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Andilile inaonyesha gharama za uagizaji bidhaa za mafuta kupitia Bandari ya Dar es Salaam zimekuwa na ongezeko la wastani asilimia 0.07 kwa petroli, asilimia 10.76 kwa dizeli na upungufu wa asilimia 5.41 kwa mafuta ya taa.

Hata hivyo, hakukuwa na mabadiliko ya bei katika bandari za Tanga na Mtwara huku mabadiliko ya kiwango cha ubadilishaji wa fedha kikiongeza shinikizo zaidi.

Hiyo ni baada ya kiwango cha ubadilishaji kinachotumika Machi kuongezeka kwa asilimia 8.54.

Licha ya vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati jambo linalofuatiliwa kwa karibu katika masoko ya mafuta duniani, Ewura imesema nchi ina akiba ya kutosha ya mafuta ya petroli kuendeleza shughuli za kijamii na kiuchumi.

Mamlaka hiyo pia imeonya wauzaji wa rejareja na jumla kuhakikisha wanazingatia kikamilifu bei kikomo mpya zilizotangazwa, ikisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayekiuka muundo wa bei uliopitishwa.

“Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika. Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani,” imeelezwa.

Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja na adhabu kali itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika.

“Wauzaji wa bidhaa za mafuta ya petroli wanatakiwa kutoa stakabadhi za mauzo kutoka kwenye Electronic Fiscal Pump Printers (EFPP) na wanunuzi wahakikishe wanapata stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita,” imeelezwa.

Stakabadhi hizo zitatumika kama ushahidi kwa wanunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo, au kuuziwa mafuta yasiyo na kiwango cha ubora unaotakiwa. Stakabadhi hizo pia zitasaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi za Serikali zitokanazo na mauzo ya bidhaa za mafuta ya petroli.