Marekani na mtindo mpya kung’oa, kuweka watawala

Marekani mbabe wa dunia, mwamuzi wa mustakabali wa taifa lolote. Hivyo ndivyo unaweza kulielezea taifa hilo lenye nguvu kubwa ya kijeshi, kiuchumi na hata kiteknolojia, mambo yanayoifanya kuwa juu zaidi ya nyingine.

Kwa miongo mingi tangu vita ya pili ya dunia, Marekani ilipata nguvu kubwa zilizoiwezesha kufanya uamuzi kwa niaba ya Mataifa mengine, jambo ambalo linapingwa lakini kwa ubabe wake na nguvu za kijeshi, hufanikiwa.

Suala la kubadilisha utawala katika nchi nyingine umekuwa ni utamaduni wa Marekani wa muda mrefu kwani pale inapoona maslahi yake yanazuiwa na watawala kwenye mataifa husika, haisiti kumwondoa madarakani.

Mifano ya hivi karibuni, kinachoendelea Mashariki ya Kati ni mwendelezo wa ubabe wa Marekani. Ilianzisha mashambulizi ya pamoja na Israel dhidi ya Iran na hatimaye kumuua Kiongozi Mkuu wa taifa hilo la Kiislamu, Ayatollah Ali Khamenei pamoja na viongozi wengine 40.

Vilevile, ulimwengu umeshuhudia Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro alichukuliwa na vikosi vya Marekani akiwa chumbani kwake, Ikulu, kisha akapelekwa Marekani na kufunguliwa mashitaka ambayo bado yanaendelea.

Kama haitoshi, mwaka 2003, Marekani ilifanya mashambulizi ya kijeshi nchini Iraq na kumkamata Rais wa nchi hiyo, Saddam Hussein ambaye aliondolewa madarakani, kabla ya kuhukumiwa adhabu ya kifo na kisha kunyongwa mwaka 2006.

Mwaka 1989, Marekani ilimwondoa madarakani Kiongozi wa Kijeshi wa Panama, Manuel Noriega na kuuondoa utawala wake madarakani, ikiwa ni mwendelezo wa mabadiliko ya utawala katika mataifa mengine.

Itakumbukwa kwamba wakati wa vita vya pili vya dunia, ni Marekani ndiyo ilisababisha kugawanyika kwa Korea na kuwa na sehemu mbili za Korea Kusini iliyoungwa mkono na Marekani na Korea Kaskazini.

Pia, Vietnam nayo iligawanywa na kuwa nchi mbili, hata hivyo baadaye iliungana tena na kuwa nchi moja. Ujerumani nayo iligawanywa wakati wa vita baridi na kuwa nchi mbili za Ujerumani mashariki na Ujerumani Magharibi, hata hivyo ziliungana tena na kuwa nchi moja.

Mwenendo huo wa kuondoa watawala madarakani au kuzigawa nchi kwa maslahi yao, ni moja ya kanuni ya marekani kuutawala ulimwengu, jambo ambalo wanadiplomasia wanaeleza kwamba linakiuka makubaliano ya Vienna pamoja na Mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN).

Kutokana na hiki kinachoendelea Iran na Mashariki ya Kati kwa ujumla, wachambuzi wa siasa wameangazia sababu za Marekani kupandikiza viongozi kwenye Mataifa mengine huku wakieleza athari zake ulimwenguni.

Mchambuzi wa siasa za kimataifa, Mussa Lugete amesema kuwa Marekani inakuja na mfumo huo kwa lengo la kuweka viongozi watakaoingia madarakani na kutekeleza matakwa yake ili kulinda maslahi yake ya kitaifa.

“Ukiyatazama mataifa yanayopitia mtihani huo, mengi ni yale yanayotaka kuachana na sarafu ya Marekani na kuanza kutumia sarafu ya China, ambayo kwa sasa inakua kwa kasi,” amesema Lugete.

Amesema yaliyoikuta Libya, Venezuela na hata Iran ni hali hiyo hiyo. Kwa mujibu wake, hatua hizo zinalenga kulinda thamani ya dola ya Marekani isishuke, kwa kuwa wanatambua kuwa China inazidi kuimarika kwa kasi. Ndiyo maana, huwekwa viongozi watakaokuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya Marekani.

“Viongozi wanaowekwa lazima walinde maslahi ya Marekani, na hutumika nguvu kubwa isiyo ya kawaida kuhakikisha hilo linafanikiwa,” anasema Lugete.

Anasema mpango uliopo ni kuinyong’onyesha Yuan ya China. Anadai kuwa hata ukiangalia mvutano unaoendelea kati ya China na Taiwani, unaodumu kwa muda mrefu, ni kwa sababu Marekani ipo nyuma ya Taiwan.

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Denis Konga amesema kuwa Marekani haina rafiki wa kudumu bali hutanguliza maslahi yake kwanza. Ameeleza kuwa licha ya kuja kwa sura ya kusaka amani na demokrasia, mara nyingi hatua zake husababisha madhara zaidi.

“Si jambo la kufurahia, kwani wananchi ndio wanaoumia zaidi,” amesema.

Kuhusu Umoja wa Mataifa (UN), amesema si chombo chenye nguvu mbele ya mataifa makubwa na mara nyingi huishia kutoa maazimio bila hatua madhubuti. Ametolea mfano tukio la Libya, akisema walishindwa kufanya lolote la maana.

Ameongeza kuwa katika ukanda wa Afrika Magharibi, watu wengi wanatamani kwenda Ulaya kutafuta maisha bora, jambo linaloonyesha udhaifu wa UN, huku mataifa makubwa yakiwa na ushawishi mkubwa zaidi.

Katika maelezo yake amesema mataifa mengi, hususan barani Afrika, hayana uhuru wa kweli kwa kuwa yamefungwa na utegemezi wa mataifa makubwa, ambayo huingilia pale yanapoona maslahi yao yapo hatarini.

“Mataifa makubwa yakihitaji maslahi huja haraka, na yasipoyaona hayawezi kuja. Venezuela imeathirika baada ya China kuanza kumiliki na kuathiri mfumo wa mafuta,” amesema.

Ameshauri diplomasia itumike kwa upana zaidi, akibainisha kuwa kwa sasa eneo la Mashariki ya Kati limekumbwa na mvutano, huku Irani ikishambulia maeneo yenye ushawishi wa kijeshi wa Marekani.

“Afrika tutapata shida, kwani tutakosa mafuta ya kuendesha mitambo na pia chakula, kwa kuwa tunategemea ngano kutoka Ukraine,” amesema.

Harry Mwinuka, mchambuzi wa siasa za dunia, amesema kuwa vitendo vya Marekani si vya kushangaza, kwani imekuwa ikirudia mwenendo huo mara kwa mara. Matendo hayo yanaiondolea heshima Marekani kwa sababu yanakiuka utaratibu na misingi ya ustaarabu.

“Vitendo hivi vinaonyesha kuwa Marekani inaweza kufanya lolote wakati wowote, na pia vinaashiria kuwa haiheshimu diplomasia. Ikumbukwe kuwa kwa sasa wanapigana na Irani ilhali walikuwa kwenye meza ya mazungumzo,” amesema.

Ameongeza kuwa Marekani inaweka mfano mbaya, ilhali kuna mataifa mengine yenye nguvu kama China, na kwamba hali inaweza kuwa mbaya zaidi endapo China itaivamia Taiwan.

“Marekani inahubiri jambo ambalo haliendani na uhalisia wa diplomasia imekuwa ikiingilia mambo ya ndani ya nchi nyingi, kutaka kulinda maslahi yake,” amesema.

Kuhusu UN, amesema kuwa chombo hicho kimepoteza ushawishi wake kwa sababu mataifa makubwa yenye nguvu yalishiriki moja kwa moja katika kuundwa kwake hivyo hakiwezi kuwa na kauli yenye mashiko.

“Mataifa yenye nguvu ya turufu kama Marekani, Urusi na China, yanapohusika, chombo hicho huwa hakina nguvu ya kusema lolote kwa kuwa kinategemea bajeti ya kujiendesha kutoka kwao. Badala yake, kimebaki kuwa chombo cha kutoa matamko pekee,” amesema.

Amesema kwa hali ilivyo sasa, hakuna njia mbadala ya kumaliza migogoro zaidi ya mazungumzo, huku akionya kuwa madhara yake yataathiri dunia nzima kupitia usafiri wa anga na majini.

“Anga na bahari zinapofungwa huathiri dunia nzima, hasa Afrika ambayo kwa kiasi kikubwa inategemea baadhi ya bidhaa na nishati ya mafuta, jambo litakalosababisha mfumuko wa bei za bidhaa, hususan za chakula,” amesema.