Happyness alivyoyaepuka mateso ya ndoa na kuangukia udereva

Dar es Salaam. Huenda baadhi ya changamoto wanazokumbana nazo wanawake katika ndoa, ikiwemo kuachika, zikawafanya waone dunia imewatupa na hawana namna tena ya kuendelea kuishi, lakini hali haikuwa hivyo kwa Happyness Aloyce (35), dereva wa mabasi ya mwendokasi, aliyeamua kugeuza maumivu yake kuwa nguvu ya kusonga mbele.

Katika mahojiano yake na Mwananchi, Happyness anaeleza safari yake ya maisha tangu alipoanzia hadi kufikia hatua aliyonayo sasa.

Akiwa mtoto wa tano kati ya wanane wa mzee Aloyce, Happyness anasema baada ya kumaliza masomo ya sekondari mwaka 2012 na kutofaulu, alikaa nyumbani kwa mwaka mmoja kabla ya kuolewa kwa ndoa ya kimila na kuhamia mkoani Kigoma kuishi na mumewe.

Ndani ya ndoa hiyo walibarikiwa kupata mtoto wa kiume. Hata hivyo, ndani ya mwaka mmoja tu, anasema mumewe alianza kubadilika kitabia, ikiwemo kushindwa kumhudumia yeye na mtoto wao.

“Pamoja na yote hayo, mume wangu hakutaki afanye kazi yoyote kwa kile alichodai ningeenda kupata wanaume wengine,” anasema dereva huyo anayefanya kazi katika kampuni ya Mofat.

Dereva wa mabasi ya mwendokasi Happness Aloyce akiwa kazini katika safari ya Mbagala- Gerezani jijini Dar es Salaam.



Anasema hali hiyo ilimfanya aishi kwa kuomba misaada ya chakula kwa majirani na wakati mwingine, mumewe alipomkuta akiomba msaada, alikuwa akimpiga mbele za watu na kumburuza hadi nyumbani.

Baada ya kushindwa kuvumilia manyanyaso hayo, mwaka 2014 alitoroka. Nauli aliipata baada ya kupewa Sh20,000 kama zawadi na jirani yake aliyemuomba awe akimkanda maji ya moto mkewe aliyekuwa amejifungua.

“Baada ya kumaliza uzazi, alinipa asante ya Sh20,000, pesa ambayo niliificha kwa sababu kwa miaka miwili sikuwa nimewahi kushika fedha,” anasema Happyness.

Anaendelea kusimulia kuwa alipofika stendi ya Gungu, hakujua ni gari gani apande, hivyo alisimama pembeni ya barabara akiwa na mtoto wake mgongoni.

“Nikiwa hapo, ghafla akatokea mtu mwenye tatizo la afya ya akili akiwa ameshika jiwe. Nilipokuwa sijui nifanyaje kujiokoa, akatokea mama mmoja akaniambia nisiogope kwa kuwa yule mtu huwa hadhuru watu. Hapo ndipo mama huyo akaanza kuniuliza mimi ni nani, kwa mtoto na naenda wapi. Nilimpa maelezo lakini hakuridhika, hivyo akanichukua hadi kituo cha polisi akihofia huenda nimeiba mtoto,” anasema.

Happyness anaeleza kuwa kituoni alikaguliwa na kuombwa vyeti vyake vya kuzaliwa pamoja na kadi ya kliniki ya mtoto. Baada ya kuvichunguza, walithibitisha kuwa ndiye mama halali wa mtoto huyo.

Baada ya kuthibitishwa, yule mama aliyemuokoa alimchukua na kumhifadhi nyumbani kwake kwa wiki mbili, akisubiri atumiwe nauli kutoka kwa mama yake.

Taarifa za mateso aliyokuwa akiyapitia zilimfikia mama yake kupitia dada yake, kwa kuwa mama hakuwa na simu wakati huo. Baadaye walimtafuta mtu wa kumpelekea simu ili kuzungumza naye moja kwa moja.

Dereva wa mabasi ya mwendokasi, Happness Aloyce akikagua gari lake kabla ya kuanza safari ya mbagala Gerezani jijini Dar es Salaam.



Aliporejea kwao, Happyness hakutaka kubaki nyumbani bila kufanya kazi. Aliomba kazi ya usafi katika maabara iliyokuwa karibu na nyumbani kwao, kazi aliyofanya kwa mwaka mmoja.

Mwaka 2015, aliona tangazo la nafasi za kazi ya ulinzi katika kampuni ya KK Security. Aliomba na kufanikiwa kuchaguliwa. Baada ya mafunzo ya muda mfupi, alianza kazi rasmi jijini Dar es Salaam.

Akiwa mlinzi, alipangiwa kulinda kiwanda cha Saruji Wazo. Huko, alikuwa akiiona wanawake waliokuwa wakiendesha malori makubwa ya kubeba saruji hadi tani 36, wakisafirisha kwenda nchi za Rwanda, Congo na Burundi. Taswira hiyo ilimvutia na kuanza kuota ndoto ya siku moja kuwa dereva kama wao.

Ili kutimiza ndoto hiyo, aliwaomba madereva hao wamfundishe. Taratibu, wakaanza kumpa mazoezi katika eneo la maegesho ya magari walipokuwa wakisubiri zamu ya kupakia mizigo.

“Walipoona nina juhudi za kujifunza, waliniunganisha kwenye makundi yao ya WhatsApp ya madereva. Nikiwa huko, walinishauri kuwa ili kufikia ndoto zangu ni vyema nianze kusomea udereva wa magari madogo na mabasi kwanza. Hapo ndipo nilipojiunga na chuo cha udereva kilichopo Tegeta,” anasema Happyness.

Anasema alikuwa akisoma asubuhi na jioni kuingia kazini, huku mtoto wake aliyekuwa na miaka miwili akimuacha na mfanyakazi wa nyumbani.

Ili kumudu gharama za masomo, kumlipa mfanyakazi wa nyumbani na mahitaji mengine, alianzisha biashara ndogo ya kuuza mkaa ili kujiongezea kipato.

Katika mafunzo yao ya vitendo, walikuwa wakienda katika vituo vya mabasi kama Kibaha na kuomba vibali kwa wakaguzi wa usalama barabarani ili kufanya mazoezi ya kuendesha mabasi.

Baada ya kuitumikia kampuni ya KK Security tangu 2015, aliachana nayo mwaka 2021 alipopata ajira katika Kampuni ya Uendeshaji Mabasi ya Haraka (Udart), akiwa miongoni mwa wanawake 20.

Siku ya kwanza kwenye basi

Happyness anakumbuka siku yake ya kwanza kuendesha basi la mwendokasi, alipangiwa safari ya kwenda kituo cha Mabasi Magufuli.

“Nakumbuka nilikuwa natetemeka kwa sababu sikuwahi kubeba abiria, lakini baada ya kufika mwisho wa safari, abiria walinipongeza na kunikubali,” anasema.

Kuhusu changamoto barabarani, anasema hukutana na vikwazo mbalimbali, ikiwemo baadhi ya waendesha bodaboda kutokuzingatia sheria za usalama barabarani. Hata hivyo, anasema kwa upande wa abiria, wengi huonesha furaha wanapoona wanaendeshwa na mwanamke.

Kuhusu matarajio yake ya baadaye, Happyness anasema anatamani kufungua chuo kitakachowafundisha wanawake wenye ndoto za kuwa madereva.

Akizungumzia Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa kila Machi 8, 2026, anatoa ujumbe: “Wanawake tunaweza. Tusikubali kukatishwa tamaa hata kama tumeachika au tumepitia changamoto katika ndoa. Maisha lazima yaendelee, kama ilivyokuwa kwangu,” anasema.

Naomi Boniface, mkazi wa Mzinga, aliyekuwa mmoja wa abiria katika basi aliloendesha Happyness, anasema alijisikia fahari kumuona mwanamke akiendesha basi.

“Nilivyoingia ndani ya basi na kuona dereva ni mwanamke, nilijisikia vizuri. Inadhihirisha kuwa wanawake wana uwezo wa kufanya mambo makubwa na kwamba kazi haina jinsia,” anasema.

Valerian Haule, mkazi wa Kisemvule, anasema zamani ilikuwa nadra kuwaona wanawake wakiendesha magari makubwa, lakini sasa hali imebadilika.

Anawashauri wazazi na walezi kuwaacha watoto wa kike wachague kazi wanazozipenda, mradi ziwe halali na zisizokiuka maadili ya jamii.

Naye Yahaya Nassoro, mkazi wa Mbagala Majimatitu, anasema anaona faraja kuona wanawake hawachagui kazi siku hizi. “Bila hata kuwezeshwa sana, mwanamke anaweza. Tatizo ni jamii kuwachukulia ndivyo sivyo kwa sababu ya jinsi yao,” anasema.